The things hardest to bear are sweetest to remember. – Lucius Annaeus Seneca

Habari za asubuhi ya leo rafiki?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri na ya kipekee sana leo.
Ni fursa nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Kwa mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa mwaka huu 2018.

Asubuhi hii tutafakari TUNAKUMBUKA MAGUMU…
Huwa hatupendi mambo na hali ngumu tunazopitia.
Huwa tunatamani hali hizi zisingekuja kwenye maisha yetu na kama zinakuja basi zipite haraka sana.

Lakini kila tunapokaa na kukumbuka nyuma,
Kila tunapokaa na kusimuliana tulipotoka,
Tunayoyakumbuka na kujivunia nayo ni yale magumu tuliyoyavuka.

Tunakumbuka yale yaliyotusumbua, yaliyotupa ugumu na changamoto kubwa.
Tunakumbuka yale ambayo tulifikiri yangetushinda lakini tumeyashinda.
Tunakumbuka na kujivunia jinsi ambavyo tumeweza kuvuka hayo magumu.

Hivyo mwanamafanikio, unapokutana na ugumu, usiukimbie wala kuugopa, bali ukubali ukijua huo ndiyo unaotengeneza historia, ndiyo unatengeneza hadithi za baadaye.
Jua kwa kutatua ugumu huo, utakuwa na kitu cha kusema baadaye, kitu cha kukupa hamasa ya kuendelea zaidi.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kwenda kufanya magumu ili kutengeneza hadithi za siku zijazo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha