Kuna tabia moja ya waajiriwa ambayo nimekuwa naona inawarudisha nyuma sana kwenye kupiga hatua kwenye kazi hiyo. Tabia hiyo ni kufanya yale ambayo wanalipwa tu. Kama mtu halipwi moja kwa moja kwa kufanya kitu, basi hakifanyi. Na utawasikia kabisa wakijiambia kwani nalipwa?

Tabia hii nimekuwa naiona pia kwa wafanyabiashara ambao wanashindwa kuzikuza biashara zao. Wafanyabiashara hawa wanafanya kile tu ambacho kinawapelekea walipwe moja kwa moja.

Kama hawalipwi moja kwa moja basi hawafanyi, na hivyo kwa msimamo na mtazamo huu, wanakosa nafasi nzuri ya kujenga mahusiano mazuri na wateja wao.

Kwenye biashara, kuna vitu vidogo vidogo ambavyo unaweza kufanya kwa wateja wako, ambavyo havitapelekea ulipwe moja kwa moja, lakini vinatengeneza thamani ya wewe kulipwa zaidi baadaye.

huduma wateja

Kwa mfano kumweleza vizuri na hata kumshauri mteja ambaye huenda hatanunua kwako, haitapelekea wewe kulipwa moja kwa moja. Lakini mteja huyo atakukumbuka wakati mwingine akiwa na shida unayoweza kuitatua.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kujenga Biashara Kubwa Ya Wateja Wanaolipa Fedha Taslimu Na Siyo Mikopo.

Kuwaambia wateja maneno kama asante, karibu, samahani na tafadhali, kunaweza kusipelekee wewe kulipwa zaidi kwa wakati huo. Lakini ndani ya mioyo ya wateja wako, wanajua unajali na hivyo kupanga kuendelea kuwa wateja wako.

Kumsaidia mteja ambaye amefanya makosa fulani, ambayo hayakuhusu wewe, kunaweza kusikulipe wakati unafanya hivyo, lakini baadaye itakuwa manufaa makubwa kwako.

Chochote unachoweza kufanya kwenye biashara yako kwa ajili ya kuyafanya maisha ya wateja wako kuwa bora, kifanye, iwe unalipwa au hutolipwa. Kama unachofanya ni chema na chenye thamani, dunia itaona na kukulipa sawasawa na unachotoa.

Unapoingia kwenye biashara, usiwe mtu wa kila mara kuangalia napata nini, bali jiulize wewe unatoa nini?

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog