Kitu pekee ambacho kwa sasa kimekuwa adimu, ambacho hakimtoshi kila mtu, imekuwa siyo fedha kama wengi walivyokuwa wakilalamika, bali imekuwa muda.
Siku za nyuma watu walikuwa wakisema matajiri wana fedha lakini hawana muda, na masikini wana muda lakini hawana fedha. Lakini sasa hivi, mambo yamebadilika, kila mtu hana muda na zaidi, masikini ndiyo hawana muda.
Yote hayo ni kwa sababu ya kuongezeka kwa aina za usumbufu na kelele. Ni rahisi sana kujikuta unahangaika na usumbufu na kusahau yale muhimu. Usumbufu mkubwa unaanzia kwenye simu, mitandao ya kijamii na hata habari mbalimbali.
Kwa usumbufu huo, kila mtu anaona kama muda hautulii, anaona muda unakwenda kasi na mambo hayafanyiki.

Lakini ipo njia ya kuutuliza muda wako na kuhakikisha unakwenda taratibu kama unavyotaka wewe mwenyewe. Kwa njia hiyo, utaweza kukamilisha yale muhimu huku ukiwa na muda wa kupumzika pia.
Njia hii siyo ngeni na wala siyo muujiza, bali ni kupangilia kila dakika ya siku yako.
Tumezoea tu kusema kwamba leo nitafanya hichi au kile, halafu tunajiambia muda ni mwingi na hivyo tutafanya tu. Ni mpaka pale siku inapoisha tukiwa na kujikuta hatujafanya ndiyo tunakumbuka kwamba muda siyo mwingi kama tulivyofikiri.
SOMA; UKURASA WA 1061; Ukiacha Kuangalia Ndoto Zako, Utaona Hichi Kitakachokutisha…
Hivyo panga kila dakika ya siku yako, na muda wa mwanzo wa siku, uweke kwa ajili ya yale ambayo ni muhimu zaidi. Kisha yale ambayo siyo muhimu, yape muda wa baadaye sana kwenye siku yako.
Usikubali usumbufu uwe na kipaumbele kwenye siku yako, badala yake kipaumbele kiwe kwa yale ambayo ni muhimu. Na panga kabisa ni muda upi wa siku utafanya kile ambacho ni muhimu, kisha kwenye muda huo fanya.
Usiruhusu kuvunja kile ulichopanga kirahisi rahisi.
Kwa wale ambao bado hawana uhuru wa kupanga muda wao watakavyo, kwa maana kwamba wameajiriwa na hivyo wanaweza kubadilishiwa kipi wanafanya, ule muda wa kazi, labda saa mbili mpaka saa kumi basi uweke kuwa muda wa kazi. Hapo unaweza kupanga ya kufanya lakini kutoa nafasi ya kupangiwa mengine. Lakini ule muda nje ya kazi, upange wewe kama utakavyo. Kwa mfano muda wa asubuhi, kabla ya kazi na muda wa jioni baada ya kazi, upangilie vizuri kwa yale ambayo ni muhimu kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog