Habari za leo rafiki yangu?

Heri ya mwezi mpya, ule mwaka tuliokuwa tunashangalia 2018 kwamba ni mpya, unazidi kuzeeka na kuisha. Hivi unaweza kuamini tupo mwezi wa tatu sasa? Ila hilo siyo swali, swali ni je kwenye miezi miwili iliyopita, ni hatua zipi umepiga kuelekea kwenye malengo yako ya mwaka huu 2018?

Hilo ni swali muhimu unalopaswa kujiuliza kila mwezi na kila wiki ili uweze kuona unakwendaje.

Moja ya mambo muhimu ambayo nimekuwa nakusisitiza rafiki yangu ni usomaji wa vitabu. Na nimekuwa nakusisitiza hili kwa sababu najua umuhimu wake na yeyote ambaye amewahi kusoma vitabu, ameona umuhimu wake.

Hivyo kila mwezi nimekuwa nakupendekezea vitabu unavyoweza kusoma, na haya kama huna muda kabisa, basi nimekuwa nakukaribisha kwenye PROGRAMU YA KUSOMA KURASA KUMI KILA SIKU, ambapo ndani ya mwezi utasoma kurasa zipatazo 300 ambazo zitakuwa zaidi ya kitabu kimoja.

Mwezi huu Machi 2018 nimekuandalia vitabu viwili vizuri sana ambavyo unapaswa kuvisoma. Vitabu hivi vinalenga wewe kufanya kazi bora zaidi na pia kuacha tabia ya kuahirisha mambo.

Changamoto kubwa ya zama tunazoishi sasa ni usumbufu ambao unawafanya watu kuwa bize, kuchoka sana lakini mwisho wa siku hawaoni kipi kikubwa wamefanya. Kadhalika kwa ubize huo, kinachotokea ni kuahirisha kufanya yale mambo ambayo ni muhimu kwako. Hivyo unashangaa siku zinakwenda lakini hakuna kikubwa ambacho mtu unakuwa umefanya.

Hivyo mwezi huu nimekuandalia vitabu hivi viwili;

Kitabu cha kwanza; DO MORE GREAT WORK.

Mwandishi wa kitabu hichi, Michael Stanier anatushirikisha njia sahihi za kuepukana na kazi ambazo siyo muhimu na zinazotuchosha, na kuweza kuweka nguvu zetu kwenye kazi ambazo ni bora kabisa.

Kwa mfano, mwandishi anatuambia kwenye kazi tunazofanya, tunaweza kuzigawa kwenye makundi matatu kulingana na namna tunavyozifanya kazi hizo.

Kundi la kwanza ni kazi mbovu. Hizi ni kazi ambazo hazina maana kwetu wala kwa yeyote yule. Ni kazi ambazo kitendo cha kuzifanya tu ni kuamua kupoteza muda, na maisha pia, kwa sababu hakuna chochote ambacho kazi hizi zinaongeza kwenye maisha yetu. Hizi ni kazi ambazo mtu unapaswa kuziacha mara moja.

Kundi la pili ni kazi nzuri. Hizi ni zile kazi zetu za kawaida, zile ambazo tunafanya kila siku na kupitia kazi hizi tunatekeleza yale majukumu ya kila siku. Ni kazi ambazo mara nyingi tunazifanya kwa mazoea na wakati mwingi wala hatuhitaji kufikiri sana. Kazi hizi hazina shida, ila hatupaswi kuweka muda wetu mwingi kwenye kazi hizi pekee, kwa sababu hazitusukumi kwenda mbele.

Kundi la tatu ni kazi bora. Hizi ni zile kazi za kipekee sana ambazo tukizifanya tunapata matokeo makubwa na ya kipekee kabisa matokeo yake yanaongeza thamani kubwa kwetu na wale wanaozitegemea. Kazi hizi siyo rahisi, na pia hazina uhakika, unahitaji kufanya mambo ambayo hujazoea kufanya, na yenye hatari ya kushindwa. Hizi ndiyo kazi zinazokufikisha kwenye mafanikio makubwa. Unahitaji kuweka muda wako kwenye kazi hizi ili kufanikiwa.

Kama unataka mafanikio kwenye kazi au biashara unayofanya, basi unapaswa kusoma kitabu hichi, kwa sababu kitakusaidia sana kuondokana na kazi zisizo na matokeo bora na kuweza kufanya yale yenye matokeo bora.

do more great work

Kitabu cha pili; EAT THAT FROG.

Kitabu cha pili ambacho nakushauri sana wewe rafiki yangu ukisome mwezi huu wa machi ni kitabu EAT THAT FROG ambacho kimeandikwa na Brian Tracy. Kitabu hichi kinatupa njia 21 za uhakika za kuondokana na tabia ya kuahirisha mambo.

Ni mambo mangapi umekuwa unapanga kufanya, lakini unapofika wakati wa kufanya unasema nitafanya kesho? Usifikiri hilo ni jambo la kawaida, hiyo ni tabia sugu ya kuahirisha mambo, ambayo huwezi kuiondoa kirahisi. Unahitaji mikakati sahihi ya kuiondoa.

Brian anasema kwamba kama kila siku unapaswa kumla chura, haina maana kusubiri muda mrefu ukifikiria unamlaje chura huyo, kwa kufanya hivyo unajichelewesha na kujisumbua zaidi. Hivyo Brian anatuambia, cha kufanya ni kumla chura huyo mapema kabisa ili uendelee na mambo yako mengine.

Sasa kwenye kazi zetu, chura tunayepaswa kumla ni yale majukumu makubwa ya kazi yetu, ambayo ni magumu au hayavutii kufanya, ila lazima tuyafanye. Sasa unapoanza siku yako kwa kufanya mambo hayo, unajiondoa kwenye nafasi ya kuahirisha mambo hayo.

Soma kitabu hichi na zipo mbinu 21 za kukuwezesha kuondokana na tabia ya kuahirisha mambo, ikiwepo sheria nzuri ambayo nimewahi kukushirikisha ya PARETO, ambayo inasema asilimia 80 ya matokeo mazuri inatokana na asilimia 20 ya juhudi unazoweka.

Kitabu EAT THAT FROG ni kitabu unachopaswa kukisoma, na kama umeshakisoma, rudia tena kukisoma, ili mwaka huu 2018 usiingie kabisa kwenye kuahirisha mambo.

eat that frog

UTARATIBU MZURI WA KUSOMA VITABU HIVI VIWILI.

Kitabu cha DO MORE GREAT WORK kina kurasa 124 na kitabu EAT THAT FROG kina kurasa 117 hivyo jumla inakuwa kurasa 241. Sasa kama kila siku utasoma kurasa 10 tu za kitabu, ndani ya siku 25 utakuwa umemaliza kabisa vitabu hivi viwili.

Hivyo basi, kama umekuwa unapenda kusoma vitabu lakini huna muda, au hupati vitabu vya kusoma, ninayo program nzuri sana kwako. Program hii inatatua changamoto zako zote kwenye usomaji wa vitabu. Unapata vitabu vya kusoma, kwa mfano hivi viwili utavipata kwenye program hii.

Pia program hii inakupa mpango mzuri wa kusoma, kwa kusoma KURASA KUMI ZA KITABU KILA SIKU. Pia unapata hamasa ya kusoma, kupitia wasomaji wengine.

Program hii inaitwa KURASA KUMI ZA KITABU, ni kundi la wasap ambapo unapata vitabu vya kusoma, utaratibu mzuri wa kusoma na pia hamasa ya kusoma kutoka kwa wasomaji wengine.

Ili kujiunga na program hii unahitaji vitu vitatu tu;

Cha kwanza kuwa unatumia mtandao wa wasap.

Pili kulipa ada ya tsh 10,000/= ada hii unalipa mara moja tu.

Tatu uwe tayari kusoma na kushirikisha yale unayojifunza.

Kama unapenda kusoma vitabu, kama unapenda kupata vitabu zaidi vya kusoma, basi karibu kwenye program hii.

Kujiunga, tuma ada, tsh 10,000/= kwa namba 0717396253 au 0755953887 kisha nitumie ujumbe kwa wasap namba 0717396253 ujumbe uwe na majina yako kamili na maneno KURASA KUMI. Ujumbe uwe kwa njia ya wasap na ukishakamilisha malipo. Hapo nitakuweka kwenye program na kukupa maelekezo zaidi.

Usomaji

Kosa kila kitu kwenye siku yako, lakini usikose kusoma kurasa kumi za kitabu. Karibu sana tusome kwa pamoja.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog