Kwanza tu kitendo cha kutoa lawama siyo sahihi, kwa sababu ni kujaribu kujitoa kwenye hali fulani ambayo umechangia kujiweka kwenye hali hiyo.

Lakini sasa kuna mambo madogo madogo ambayo huwa tumejikuta tumenasa, na hivyo kutoa lawama ndogo ndogo linaonekana kuwa jambo la kawaida.

Kwa mfano mtu anaposema simu yangu inanipotezea muda kweli, au mitandao ya kijamii imekuwa usumbufu kwangu. Kwa hali ya kawaida tunamwelewa, kwa sababu kweli simu zinachukua muda wetu na mitandao ya kijamii, ni kelele kwa kweli.

Mtu pekee

Lakini hebu turudi nyuma kidogo na kuangalia hali kama hiyo imefikaje hapo ilipofika, mpaka mtu kukiri kwamba ni tatizo kwake. Kwamba mtu mwenyewe alichagua kununua simu. Mtu mwenyewe alichagua kuweka program za kufikia mitandao ya kijamii kwenye simu yake. Vitu hivyo amevikaribisha yeye, lakini sasa hawezi tena kuviendesha, bali vinamwendesha yeye.

SOMA; UKURASA WA 979; Kubali, Kisha Chukua Hatua.

Je unafikiri vitu hivyo vinastahili lawama? Yaani kitu ambacho umekitafuta wewe mwenyewe, kisha ukakikaribisha mwishowe kikawa tatizo kwako, unastahili kukilaumu?

Sioni kama hiyo ni lawama sahihi, kulaumu vile vinavyotukwaza. Lawama sahihi zinapaswa kuja kwetu wenyewe, sisi ambao tumechukua hatua mpaka tukafika pale tulipo sasa.

Tujilaumu kwa kushindwa kujidhibiti sisi wenyewe mpaka kutoa nafasi ya kudhibitiwa na vile ambavyo tumevikaribisha kwenye maisha yetu. Hata kama ni watu, ukichunguza kwa makini, unakuta sisi wenyewe tumewapa nafasi wao kufanya kile ambacho tunalaumu wamefanya.

Peleka lawama sehemu inayostahili, na kwa lolote linalotokea kwenye maisha yako, lawama zinapaswa kuanzia kwako. Na dawa pekee ni kujidhibiti wewe mwenyewe, ukishindwa kujidhibiti, kila kitu kitakudhibiti.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog