Slavery takes hold of few, but many take hold of slavery. – Lucius Annaeus Seneca
Hongera mwanamafanikio kwa siki hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni fursa bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora .
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UTUMWA HAUSHIKI WATU, BALI WATU WANASHIKA UTUMWA…
Watu wamekuwa wanalalamika kushikwa kwenye utumwa fulani kwenye maisha yao.
Labda ni tabia fulani ambayo mtu ameshindwa kuiacha kama vile ulevi.
Au ni kile anachotegemea kwenye maisha kama vile ajira.
Vipo vitu ambavyo kwa wengi vimeshakuwa utumwa, na wao wanaona utumwa umewashikilia na hawana cha kufanya.
Lakini ukweli ni kwamba, utumwa haumshikilii mtu yeyote, bali wati ndiyo wanashikilia utumwa.
Tabia yoyote ambayo imeshakuwa mzigo kwa mtu, hakuna aliyemlazimisha kuianza, mtu alianza mwenyewe, kisha tabia ikajenga mizizi.
Ni mtu amechagua na kuendelea kushikilia utumwa huo, na siyo utumwa umemshikilia mtu.
Kadhalika, vile vitu ambavyo mtu unajiambia huwezi kuishi bila hivyo, ni utumwa ambao mtu umechagua kuushikilia. Ikishakuwa huwezi kuishi bila ya kitu fulani cha nje, tayari umekubali kuwa mtumwa wa kitu hicho.
Amua sasa kuacha kuwa mtumwa wa mambo uliyochagua kuwa mtumwa.
Achilia yote unayoshikilia, hasa kifikra ili kuwa huru.
Chochote unachojiambia huwezi kuishi bila ya kitu hicho, jua ya kwamba unajidanganya, hakuna chochote cha nje ambacho huwezi kuishi bila kuwa nacho.
Wewe upo huru kwa kiwango unachoamua kuwa huru.
Na utakuwa mtumwa kwa kadiri utakavyochagua utumwa wako.
Ni imani yangu utachagua uhuru na siyo utumwa.
Siku yako iwe bora leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha