Kwenye maisha, maumivu na kushindwa ni sehemu ya kawaida kabisa ya maisha. Siyo mambo yote yanakwenda kama sisi tunavyotaka yaende, au kama tulivyodhani yatakwenda.
Lakini kuna kitu ambacho siyo lazima kiwepo, na kitu hicho ni kuteseka. Japo tunaoanisha maumivu au kushindwa na kuteseka, siyo vitu ambavyo lazima viende pamoja. Bali ni vitu ambavyo watu wanachagua kuvipeleka pamoja.
Japokuwa kuumia ni sehemu ya maisha, kuteseka ni hali ambayo mtu unachagua. Na kuteseka kunatokea pale unapoanza kuyachambua maumivu, pale unapojiambia hukustahili maumivu hayo, pale unapowaangalia wengine na kusema mbona mimi tu?
Hivyo ndivyo wengi wamekuwa wakikazana na mateso ya maisha, kitu ambacho kinawafanya washindwe kupiga hatua zaidi.

Japokuwa kuteseka kunaweza kuwa haki yako, unahitaji pia kuangalia kipi unakipata kwa mateso unayojitengenezea. Kwa sababu matokeo ya mateso siku zote ni kukata tamaa na kushindwa zaidi.
SOMA; UKURASA WA 357; Maumivu Na Mateso.
Pamoja na matokeo hayo mabaya, lakini bado watu wanang’ang’ana na mateso ya kujitengenezea. Yaani ni sawa na mtu kujua ukila chakula fulani tumbo huwa linauma, lakini unaendelea kula chakula hicho na kusema ni sawa kuendelea kuumwa na tumbo.
Mambo yanatokea, tofauti na tulivyofikiri, wale tuliofikiri watakuwa upande wetu wanakuwa kinyume na sisi, wale tuliofikiri watakamilisha walichoahidi hawakamilishi, na wale tuliojua watatulipa kadiri ya walivyoahidi hawafanyi hivyo. Lakini yote haya hayapaswi kuwa mateso kwako, unapaswa kuyaona kama sehemu ya maisha na kuendelea kupiga hatua zaidi kuelekea mafanikio.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog