Upo usemi ambao umekuwa unatumika kama utani kwamba simu ina nguvu ya kuwaleta karibu walio mbali, na kuwaweka mbali walio karibu. Yaani mtu anapokuwa na simu anaweza kuwasiliana na yeyote, lakini watu wawili walio na simu wanapokuwa pamoja, kila mtu anakuwa kwenye simu yake.
Sasa kauli hii inakwenda ndani zaidi. Na ni kwamba kwa sasa simu inaweza kukuunganisha na wengine, lakini ikakutenga na wewe mwenyewe. Tumekuwa tunatumia sana simu zetu, hasa kwenye mitandao ya kijamii, kiasi kwamba tumekuwa hatuna muda na sisi wenyewe.

Kila tunapopata nafasi ya kuwa sisi wenyewe, hatuwezi kuitumia badala yake tunakimbilia kwenye simu, kuangalia nini kinaendelea, nini kinatupita.
Hii ni hali hatari kwa afya yetu ya kiroho kwa sababu kukosa muda na sisi wenyewe ni jambo hatari kwetu wenyewe. Hii ndiyo hali inayotengeneza msongo wa mawazo na hata kupelekea wengi kuingia kwenye sonona. Hatupati muda wa kuyatafakari maisha yetu, na kujaribu kupata maana ya kila kinachoendelea.
Ubaya zaidi hatupati muda wa kufikiri kwa kina kwa jambo lolote kwenye maisha yetu. Badala yake tunakatisha katisha mawazo yetu kwa kugusa hili na kuacha na kwenda kugusa jingine. Hatukamilishi jambo lolote kwa uhakika na hatuelewi chochote kwa undani.
SOMA; UKURASA WA 932; Ukimya Na Kujidhibiti…
Ambacho kinakuwa kibaya zaidi ni kwamba kwa sasa tunaihudumia dunia masaa 24 na siku saba za wiki. Muda wowote katika hali yoyote tupo tayari kupata chochote kinachoendelea duniani.
Sasa hivi, simu ikiisha chaji ni jambo la dharura kuliko mtu akikosa chakula au hata kuumwa. Hata linapotokea jambo ambalo watu wanahitajika kutoa msaada, watakimbilia kwanza kwenye simu zao kabla ya kutoa msaada unaohusika.
Simu ni nzuri, mitandao ya kijamii ni mizuri, lakini kama matumizi yake yatadhibitiwa. Kama mtu hutaweza kujiwekea ukomo kwenye matumizi ya vitu hivi, vitakuwa chanzo kikubwa cha matatizo kwenye maisha yako. Utaendelea kuungana na dunia wakati unatengana na wewe mwenyewe. Utaendelea kuijua dunia wakati wewe mwenyewe hujijui vizuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog