Sisi binadamu huwa tunajiita ni viumbe wa kufikiri, kwamba ukilinganisha sisi na viumbe hai wengine, sisi tuna uwezo wa kufanya maamuzi kwa kufikiri kwa kina.

Japo hili ni kweli, lakini siyo kweli mara zote. Kuna nyakati ambazo tunafanya maamuzi bila hata ya kufikiri kabisa. Kuna nguvu au hali fulani ambazo zinatusukuma kufanya maamuzi bila ya kufikiri kwa kina.

Mambo yasingekuwa mabaya kama nguvu hizi zingekuwa siri au hazijulikani. Lakini ubaya ni kwamba, nguvu hizi siyo siri, hivyo wapo watu ambao wanajua jinsi ya kutumia nguvu hizi, na kinachotokea ni kwamba wanazitumia kwa manufaa yako.

Yaani iko hivi, nguvu ambazo zinakusukuma mtu kuchukua maamuzi bila ya kufikiri zinatabirika na hivyo watu wanaweza kuzitumia kupata manufaa bila ya kujali wewe unapata nini. Kwa mfano mfanyabiashara anapokuambua pata kitu fulani BURE, usifikiri mfanyabiashara huyo anatoa bure kweli, kuna gharama kubwa utalipa baadaye.

Mwandishi na mwanasaikolojia Dan Ariely ameandika kitabu cha PREDICTABLY IRRATIONAL kutuonesha nguvu hizi zinazotusukuma kufanya maamuzi bila ya kufikiri. Kupitia kitabu hichi tutaona makosa tunayoyafanya na jinsi ya kujizuia kutorudia makosa hayo tena.

predictably irrational

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hichi, tushirikishane yale muhimu ili kuepuka kufanya maamuzi bila ya kufikiri.

UKWELI KUHUSU KUHUSIANISHA VITU; KWA NINI TUNAPENDA KULINGANISHA VITU HATA KAMA HAVIHUSIANI.

Huwa tunafanya vitu kwa kulinganisha na vitu vingine, na hili limekuwa linatumika kuwafanya watu waamini wanachagua kwa kufikiri, kumbe wanachagua kwa kusukumwa na wengine.

 1. Hatuwezi kuchagua kitu kama hatuna cha kulinganisha.

Binadamu huwa tuna tabia ya kuchagua kitu baada ya kulinganisha na vitu vingine. Hivyo tunapokuwa na kitu kimoja cha kuchagua, tunashindwa kufanya maamuzi. Kwa mfano ukiambia bei ya nguo fulani ni elfu kumi, kama hujawahi kununua nguo kabisa, huwezi kujua kama hiyo ndiyo bei sahihi au la. Lakini unapokuta nguo nyingine inauzwa elfu 9, na nyingine elfu 15 hapo sasa una njia ya kulinganisha na kujua ipi uchague.

Hali hii imekuwa inatuingiza kwenye matatizo, hasa pale watu wanaotaka tuchague kitu fulani wanatuwekea vitu vya kulinganisha ambavyo hata haviendani. Lengo ni wewe uone unachagua kitu ambacho ni bora kwako, kumbe unaingizwa kwenye mtego wa kuchagua kile ambacho watu wanataka uchague.

 1. Mara zote weka machaguo mengi ya kulinganisha.

Kutumia dhana hii ya kulinganisha vitu kwa manufaa yako, kwenye kile unachofanya, kama unataka watu wachague kitu fulani, basi hakikisha unawawekea vitu vingine ambavyo siyo bora kama unachotaka wachague, hilo litawasukuma wachague kile unachotaka wachague. Kwa mfano kwenye biashara, unaweza kuwa na bidhaa ambayo ni bora kabisa na bidhaa nyingine ambayo siyo bora. Lengo lako siyo kuuza bidhaa isiyo bora, bali kuwafanya wateja wachague bidhaa bora.

Pia kwenye bei dhana hii ya kulinganisha ina matumizi yake. Kwa mfano unaweza kwenda kwenye mgahawa, ukakuta orodha ya vyakula vilivyopo inaanza na vyakula vya bei kubwa sana, halafu kule chini kuna vyakula vya bei ndogo kwa kulinganisha na vile vya juu, lakini ni kubwa ukilinganisha na bei za kawaida. Wewe ukiangalia orodha ile na kuona vyakula vya bei ghali, ukifika kwa vile vinavyoonekana ni vya bei rahisi utaona ni sahihi kwako kulipa, hata kama nje ya hapo vinauzwa bei rahisi zaidi.

 1. Acha kuangalia uwanja mpana.

Kuepuka kuingia kwenye gharama na kusukumwa kufanya maamuzi bila ya kufikiri sawa sawa kwa njia hii ya kulinganisha, unahitaji kuacha kuangalia uwanja mpana. Acha kuangalia vitu vya kulinganisha kwenye kila unachofanya. Kama kuna kitu unataka, angalia thamani yake na siyo kulinganisha na vitu vingine.

TATIZO LA NGUVU YA UZALISHAJI NA UHITAJI.

Kwenye uchumi, huwa tunaamini nguvu ya soko ndiyo inaendesha vitu, kupanga bei na hata uzalishaji na uhitaji. Kwamba kama kitu kinahitajika sana, basi bei yake inakuwa juu, uzalishaji unaongezeka pia. Na uzalishaji ukiwa mkubwa sana bei inashuka.

Hii ni kweli kwenye kufikiri, lakini katika uhalisia, zipo nguvu zinazodhibiti uzalishaji na uhitaji na hata bei ukiacha nguvu ya uchumi.

 1. Bei ya kwanza inapangwa kuweka alama.

Mara nyingi bei ya kwanza tunayoisikia kwenye kitu, huwa ndiyo tunaamini ni thamani halisi ya kitu hicho. Hivyo wafanyabiashara wamekuwa wakichagua bei fulani ambayo wanaiweka kwenye kitu, hata kama siyo watakayouzia, kwa ajili ya kuweka alama kwenye akili za watu kwamba kitu hicho kina thamani fulani. Kuanzia hapo mtu anakuwa na kumbukumbu kwamba kitu fulani kinagharimu kiasi fulani.

 1. Watengenezee watu hadithi ya thamani.

Umewahi kujiuliza kwa nini mtu akienda kwenye supermarket atanunua embe kwa shilingi elfu mbili na hataomba kupunguziwa, lakini akinunua kwenye kibanda akiambiwa elfu moja atataka apunguziwe? Ni kwa sababu tayari watu wana picha ya bei na thamani kwenye kila wanachofanya. Hivyo kwenye biashara yako na kazi zako, hakikisha unawajengea watu hadithi ya thamani ya kile unachofanya. Wafanye wajue kabisa kwako wanapaswa kulipa kiasi gani na hilo halitawasumbua.

 1. Kila unachofanya, jitafakari.

Socrates alisema maisha ambayo hayatathminiwi hayana maana kuishi. Na hivyo ili kuepuka kuingia kwenye mtego wa kutengenezewa bei ya vitu, unahitaji kuacha kufanya mazoea. Unahitaji kujitafakari kwa kila unachohitaji na kila unacholipia. Je hiyo ndiyo thamani yake kweli au ndivyo kumbukumbu zako zimetengenezwa kuamini?

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Primary Greatness (Nyenzo 12 Za Mafanikio Kwenye Maisha).

GHARAMA YA SIFURI; KWA NINI UNALIPA GHALI UNAPOKUBALI KITU CHA BURE.

Wafanyabiashara wanajua kitu kimoja, watu wanapenda BURE na watu hawachunguzi bure hiyo ni bure kiasi gani. Hivyo wanapotaka kuwasukuma watu kuchukua hatua fulani, wanatumia neno BURE, siyo kwa sababu wanataka kutoa bure, ila wanajua ukitaka watu walipe zaidi, weka hiyo BURE, hata kama siyo ya kweli.

 1. Kila muamala una faida na hasara.

Kinachotusukuma watu kupenda bure ni faida na hasara za kila muamala. Ukitoa fedha kununua kitu, ni kitendo cha hatari, kwa sababu fedha hiyo huwezi kuitumia kufanya kitu kingine, tayari umeshalipa. Lakini pia kile unacholipia huna uhakika kama kitakufaa kama unavyotaka.

Lakini kitu kinapokuwa ni BURE, tunasahau hasara na kuona faida tu. Kwamba unapata kitu bila ya kulipia, kwamba unabaki na hela yako, huu unaonekana ni ushindi rahisi, lakini hapo ndipo hasara kubwa imejificha.

 1. Ukichunguza kila bure siyo bure kweli.

Vitu vingi ambavyo huwa vinapewa ofa ya bure, siyo bure kwa namna yoyote ile. Kwa mfano umeenda kufungua akaunti ya benki, benki moja wanakuambua watakukata kiasi fulani cha fedha kila mwezi, wakati benki nyingine inakuambia ni bure, hakuna makato kabisa. Ni rahisi kukimbilia ile inayokuambia ni bure, lakini sasa unapoanza kutumia, unagundua benki ambayo haina makato ya mwezi, ina makato makubwa kila unapotumia huduma zake, labda kutoa fedha kwenye mashine.

Bure pia inatuzuia kupata kile tunachotaka. Unaweza kwenda kununua kitu ambacho unakitaka, ukakuta kuna kingine ambacho ni bure, lakini ni mpaka ununue kitu kingine usichotaka. Labda unaambiwa nunua mbili upate moja bure, halafu hivyo viwili unavyopaswa kununua hata huhitaji.

Mwisho kabisa, bure huwa inatumia muda wetu mwingi, sasa ukianza kuangalia thamani ya muda wako, utagundua bure ni gharama.

 1. Wape watu kitu cha bure au sehemu ya kitu bure.

Kutumia dhana hii kwa manufaa yako, kama unataka kupata wateja wengi, basi tafuta kitu unachoweza kutoa bure kwa wateja wako. Kwa mfano unaweza kutoa kitu cha ziada kwa manunuzi yanayozidi kiasi fulani, au kulipia nauli na vingine vya aina hiyo. Inapaswa kuonekana kwa mteja ni bure, hata kama mwisho wa siku atalipa kiasi kile kile. Watu wanapenda bure, wape bure na watanunua zaidi.

 1. Kwenye kila bure, jiulize unalipaje?

Kuepuka kuingia kwenye mtego wa bure na baadaye ukahitajika kulipa zaidi, kila penye neno bure usikimbilie tu, bali jiulize unalipaje? Amini kwamba hakuna kitu cha bure, hivyo chunguza kila unachoambiwa ni bure na utaona gharama zilizojificha.

Utakuwa upande salama zaidi kama utaachana na vitu vya bure, yaani ukisikia kitu bure, unakaa mbali kabisa.

GHARAMA YA KANUNI ZA KIJAMII; KWA NINI TUNAPENDA KUFANYA VITU LAKINI SIYO KWA KULIPWA.

Ukialikwa ukweni kwa chakula cha jioni, ukakuta chakula kimeandaliwa vizuri sana, chakula cha gharama, vinywaji vizuri, na hayo yote yameandaliwa na mkwe wako. Mkala na kufurahi, kila mtu akasifia chakula cha jioni kimeandaliwa vizuri, halafu wewe ukasimama na kusema chakula hichi kimeandaliwa vizuri sana, kisha ukatoa pochi yako na kumuuliza mkweo, umetumia gharama kiasi gani kuandaa chakula hichi cha jioni? Nataka nikulipe fedha yako yote. Unafikiri watu watakuchukuliaje? Huenda ikawa ndiyo siku ya mwisho kukaribia kwenye nyumba ya mkwe wako. Japokuwa chakula kimeandaliwa kwa gharama, kujaribu kulipa gharama hiyo kwa fedha hakuna atakayekuelewa.

Zipo gharama za kijamii, ambazo hazilipiki kwa fedha. Na hizi ni muhimu kuzijua kwa sababu zimewaingiza wengi kwenye mtego.

 1. Sheria za kijamii na sheria za soko.

Tunaishi kwenye dunia mbili kwa wakati mmoja. Dunia moja inaendeshwa na sheria za kijamii ambapo hapa gharama ya vitu inaamuliwa kwa uhusiano wa kijamii ambao upo. Dunia ya pili inaendeshwa na sheria za soko ambapo gharama ya vitu inatokana na thamani ya soko.

Gharama za kijamii ni ile misaada ambayo marafiki na jamaa wanatuomba tuwasaidie. Kwa mfano kama una gari na rafiki yako ana gari, halafu gari yake imekataa kuwaka na akakuomba uende na gari yako ukamsaidie kuwasha gari yake, utaenda na hutategemea kulipwa chochote.

Gharama za soko ni zile za kawaida, bei za vitu, mishahara, kodi na vingine vinavyofanywa kwa makubaliano ya malipo.

 1. Matatizo yanaanzia pale kanuni za kijamii na kanuni za soko zinapogongana.

Matatizo mengi kwenye jamii, huwa yanaanzia pale kanuni za kijamii zinapoingiliana na kanuni za soko. Kwa mfano kuwa na makubaliano ya kazi, ambapo upande mmoja unatumia kanuni za kijamii wakati upande mwingine unatumia kanuni za soko. Hapa anayetumia kanuni za soko ataona analipwa kisicho sahihi, wakati anayetumia kanuni za kijamii, dhana ya malipo kwake inaweza kuwa dharau.

Hivyo kwenye mahusiano yako na wengine, jua wapi unatumia kanuni za soko, na wapi unatumia kanuni za kijamii na wapi unatumia kanuni za soko. Ukichanganya hayo mawili, utajiingiza kwenye matatizo.

 1. Wape watu maana na watakuwa tayari kufanya kitu kwa gharama ndogo.

Watu wanapenda kufanya kitu chenye maana kwao na kwa wengine hata kama hawapati malipo makubwa. Ndiyo maana watu huwa wanaweza wakajituma sana kwenye kazi za kusaidia kuliko hata kazi wanazolipwa. Hii ni kwa sababu, watu wanajitoa kusaidia kwa sababu wanachofanya kina maana kwao na kwa wengine pia.

Hivyo hata kwenye kazi au biashara, kama unataka watu wajitoe zaidi, usiwaambie tu kwamba watapata manufaa ya kifedha, bali wafanye waone wanashiriki kwenye kitu chenye maana kubwa, na hilo litawasukuma kuchukua hatua.

 1. Zawadi ni bora kuliko fedha.

Kwenye kanuni za kijamii, tumeona fedha inaweza kuharibu kabisa mahusiano. Kwa mfano tuliotumia hapo juu, labda tuseme gharama za kuandaa chakula cha jioni zilikuwa laki moja, mkwe kulipwa laki moja ataona ni kudhalilishwa. Lakini kama ukimpa zawadi ya gharama hiyo hiyo ataipokea na kufurahi sana.

Hivyo unapotaka kuwalipa watu kwenye kanuni za kijamii, epuka fedha na tumia zawadi. Watu wanafurahia na kupenda zawadi kuliko kuona unawalipa kwa walichokusaidia. Na muhimu zaidi, usiwatajie bei ya zawadi hiyo, wala kuwaonesha umewapa zawadi kwa sababu wamefanya kitu fulani, wewe toa zawadi, itapokelewa na kuimarisha mahusiano.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Psychology Of Selling (Jinsi Ya Kuuza Zaidi, Kwa Urahisi Na Haraka Kuliko Unavyodhani.)

USHAWISHI WA HISIA ZA NGONO; KWA NINI KINACHOONEKANA KIZURI NI KIZURI KULIKO TUNAVYOFIKIRI.

Hisia kali huwa zinazoua akili isifikiri kwa kina. Ndiyo maana watu wanaofanya maamuzi wakiwa na hasira au furaha sana, huja kujutia maamuzi hayo. Lakini zipo hisia ambazo ni hatari sana kwenye kufanya maamuzi, na hizi ni hisia za mapenzi au hisia za ngono na hasa pale mtu anapokuwa anakaribia kufika kwenye kilele cha hisia hizo. Tafiti zilizofanywa na mwandishi, zinaonesha mambo ambayo watu waliyakataa wakiwa na akili za kawaida, waliyakubali wakati wako kwenye msisimko wa ngono.

 1. Huwezi kujua utafanya nini ukiwa kwenye msisimko na hisa za ngono.

Umewahi kujiuliza kwa nini watu wanaweza kufanya ngono ambayo ni hatarishi bila hata ya kutumia kinga? Vipi kuhusu kubaka? Mambo kama hayo kwenye fikra za kawaida kabisa ni ya ajabu. Lakini mtu anapokuwa kwenye mazingira yanayoamsha hisia zake za kingono, anasahau kila kitu na kujikuta ameshatekeleza hisia hizo.

Hivyo kwa kuwa ni vigumu mtu kujua ni maamuzi gani utafanya unapokuwa umetawaliwa na hisia kali za ngono, hakikisha mara zote unaweka mazingira ya kitu kisicho kizuri kutokutokea.

 1. Subira ni njia pekee ya kuepusha hisia kutupeleka pabaya.

Huwezi kufikiri kwa makini ukiwa chini ya hisia kali, iwe ni hisia za mapenzi, hisia za hasira au hata furaha. Hivyo jambo pekee unalopaswa kufanya unapojikuta kwenye hali hiyo, ni kutokufanya lolote. Kuwa na subira, usiamue wala kufanya lolote. Jipe muda na acha hisia zitulie.

Na kwa upande wa hisia za ngono, ambazo ni kali zaidi, unahitaji kujijengea mazingira ambayo yatakuzuia wewe kuchukua hatua ambayo hukupanga kuchukua. Kwa mfano epuka mazingira yoyote ambayo yatachochea hisia za ngono ambazo hukutegemea ziwepo.

TATIZO LA KUAHIRISHA MAMBO; KWA NINI TUNASHINDWA KUFANYA YALE TUNAYOPANGA KUFANYA.

Kupanga siyo tatizo, watu wanapanga sana, ila inapokuja kwenye utekelezaji ndiyo tatizo lilipo. Huwa zinaibuka kila sababu kwa nini ni vyema kuahirisha kufanya kile tulichopanga kufanya. Na pale yale tunayopanga hayaleti matokeo ya haraka, huwa inakuwa vigumu zaidi kufanya. Tunapenda kufanya vile vitu ambavyo vinaleta raha ya haraka, kuliko vile ambavyo vinatutesa sasa, lakini baadaye vinaleta manufaa.

Chukua mfano wa kuweka akiba na kuwekeza kwa ajili ya baadaye. Kila mtu anajua ni vizuri kuweka akiba kwa ajili ya baadaye. Lakini kwenye utekelezaji ndipo ugumu unapoanza. Hii ni kwa sababu fedha unayoweka akiba, ina maana ujinyime eneo fulani la maisha yako, kitu ambacho wengi hawapo tayari kufanya kwa sasa.

 1. Tatizo linaanzia kwenye hisia.

Tunapopanga kwamba tutaweka akiba, tunakuwa kwenye hali ya kawaida, hali tulivu kabisa. Na hapo akili zetu zinakuwa zinafanya kazi vizuri. Lakini tunapokuwa na fedha, na kuona vile vitu ambavyo tunavipenda, akili zetu zinaruka, hisia zinatawala na tunajikuta tukifanya mambo ambayo hata hatukupanga. Naamini umewahi kuwa na mipango mizuri sana ya fedha kabla hujawa na fedha, lakini ulipozipata fedha ukasahau mipango yote.

 1. Tengeneza njia ya kujitawala na kujilazimisha kufanya.

Tafiti zilizofanywa na mwandishi kupitia wanafunzi zinaonesha kwamba, watu wanapopewa amri wanatekeleza zaidi, kuliko wasipopewa amri. Na wale ambao wanapewa nafasi ya kujiwekea amri yao wenyewe, wanatekeleza kuliko wasiokuwa na amri kabisa, lakini hawawafikii wale wanaopewa amri.

Hivyo unachoweza kufanya ili kuacha kuahirisha, ni kujitengenezea amri. Kwa mfano kwenye fedha, tenga kabisa fungu la matumizi, fungu la uwekezaji na kadhalika, na weka mfumo ambao utagawa mafungu hayo moja kwa moja.

Njia nyingine ya kujiwekea amri ni kuweka makubaliano na mtu kwamba utafanya kitu fulani na iwapo hutafanya basi akuadhibu au umpe fedha na asikurudishie.

GHARAMA KUBWA YA UMILIKI; KWA NINI TUNATHAMINI ZAIDI KILE TUNACHOMILIKI.

Katika mauziano, huwa kuna vitu viwili vinaendelea, anayenunua kitu anakipa thamani ndogo na kuona anapaswa kulipa kiasi kidogo cha fedha. Wakati anayeuza kitu anakipa thamani kubwa na kuona anapaswa kulipwa fedha nyingi. Hali hii inaletwa na ile hali ya umiliki, mtu akishajiambia kitu anakimiliki, anakithamini zaidi. Hii imekuwa pia inawafanya watu kutokufanya maamuzi kwa kufikiri.

 1. Sababu tatu kwa nini tunathamini zaidi tunachomiliki.

Kwanza tunakuwa tunakipenda, ukikaa na kitu kwa muda unakuwa unakipenda na hivyo kukipa thamani zaidi.

Pili tunaangalia kile tunachopoteza kuliko tunachopata, hivyo mtu anapouza kitu, anaona kama anapoteza kile anachomiliki na kupenda na siyo kupata fedha ambayo anaweza kuitumia kwa mengine.

Tatu watu hufikiri kila mtu anaweza kuona ile thamani na upekee wa kitu ambao wao wanaona.

Sababu hizi tatu ndiyo zinawafanya watu kurundikana na vitu ambavyo hawavihitaji, lakini hawapo tayari kuviuza kwa bei ndogo.

 1. Umiliki unavyokudanganya kununua.

Wafanyabiashara wanajua kutumia vizuri hali ya umiliki kuuza zaidi. Kwa mfano biashara zinazofanywa kwa mnada, iwe mnada halisi au mnada wa mtandaoni, pale mtu anapotaja bei na akawa wa bei ya juu kabisa, anaanza kuona kile kitu ni chake na anakimiliki. Anapotokea mtu mwingine na kutaja bei ya juu zaidi, inamfanya aone anakipoteza na hivyo kuongeza dau zaidi.

Kadhalika kwenye biashara za vitu vingine, watu wanaweza kupewa nafasi ya kujaribu kabisa wanachotaka kununua. Mfano kuendesha gari kwa majaribio kabla hujanunua. Kitendo cha kuendesha, kinamfanya mtu aone tayari anamiliki gari hiyo na hivyo inakuwa rahisi zaidi kuuziwa.

 1. Hakuna tiba ya umiliki, dawa ni kujikinga.

Biashara zinatumia nguvu nyingi kwenye matangazo kuwaonesha watu kitu kimoja, kwamba wana umiliki wa kitu ambacho hawana. Na hivyo wanakazana kwenda kununua kile ambacho wanaona wanapaswa kuwa nacho.

Hivyo kutibu dhana hii ya umiliki, ambayo inawasukuma wengi kununua vitu kwa bei kubwa huku wakiwa hawavihitaji, ni kujikinga. Kwa chochote unachonunua au kuuza, hakikisha unajiondoa kama mmiliki. Kiangalie kitu kama mtu baki kabisa na kipe thamani yake bila ya kuingiza hisia zako.

Kitabu hichi kinaeleza tabia mbalimbali za binadamu na nguvu zinazoendesha tabia hizi. Haya niliyokushirikisha ni machache na muhimu, yapo mengi zaidi kwenye kitabu. Kwa mfano dhana ya kuwa na machaguo mengi, dhana ya kuwa na mategemeo makubwa na dhana ya uaminifu, kwa nini watu wanakuwa na uaminifu kwenye mambo makubwa lakini wanakosa uaminifu kwenye mambo madogo.

Tabia zetu binadamu zinatabirika na wale wanaoweza kuzitabiri wananufaika sana. Jua nguvu zinazokusukuma kuchukua hatua bila ya kufikiri ili uepuke kutumiwa na wengine kwa manufaa yao kwa kujifunza mambo haya yaliyopo ndani ya kitabu tulichochambua.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji