Sisi binadamu tuna tabia ya upendeleo, kuanzia kwenye fikra zetu mpaka kwenye matendo yako. Huwa tunapendelea yale ambayo tunayapenda, na kubagua yale tusiyoyapenda.
Kwa mfano, wengi huamini kile wanachopenda wao ndiyo sahihi na kila mtu anapaswa kukipenda. Hivyo hata kama kuna makosa ya wazi kwenye kile ambacho mtu anapenda, mapenzi yake yanamzuia kuona makosa hayo. Anakuwa na upofu wa kutokuona ubaya wowote au kosa lolote kwa sababu tu anapenda kitu hicho.

Kwa upande wa pili, kama mtu hapendi kitu basi anakiona siyo sahihi, anaona hakifai na kina ubaya. Na chuki zake hizo juu ya kitu, zinamfanya asione hata uzuri ambao upo ndani ya kitu hicho. Kwa kuwa hakipendi basi inakuwa vigumu kwake kuona uzuri wowote ambao upo ndani ya kitu hicho.
SOMA; UKURASA WA 535; Upendeleo…
Tunapaswa kuelewa hili ili kuepuka kuwa kikwazo kwetu wenyewe kuuona ukweli. Unapotaka kujua ukweli wa kitu, hatua ya kwanza ni kuweka mapenzi au chuki zako pembeni. Futa kabisa kila hisia uliyonayo, na jilazimishe kuona kitu kama kilivyo.
Ni zoezi gumu lakini lenye manufaa makubwa sana kama ukiweza kulifanya.
Kwenye jambo lolote unalokutana nalo kwenye maisha yako, jua kuna pande tatu, kuna upande wako wewe, huu unatokana na mapenzi au chuki uliyonayo, kuna upande wa wengine, na huu unatokana na mapenzi au chuki walizonazo pia, halafu kuna upande wa ukweli.
Hakikisha unajua upande wako ni upi kwenye kila jambo, kisha weka upande huo pembeni na angalia upande wa ukweli. Epuka upendeleo wako usikuzuie kuuona na kuutumia ukweli.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog