Embe likiiva kwenye mti, huwa linaanguka chini.
Lakini je ni nini kinasababisha embe hilo kuanguka kutoka kwenye mti?
Je ni kwa sababu dunia ina nguvu ya mvutano ambayo inafanya embe kuanguka chini? Kama ndivyo kwa nini halikuanguka wakati likiwa halijaiva?
Je ni kwa sababu kikonyo kinachoshikilia embe hilo kinakuwa kimechoka?
Au ni kwa sababu embe hilo linakuwa zito kiasi cha kushindwa kukaa kwenye mti?
Au ni kwa sababu upepo umepita na kutikisa embe hilo kisha kupelekea kuanguka?

Hakuna jibu moja pekee ambalo tunaweza kupata kwenye mfano huo wa embe kuanguka. Na hii inatuonesha kwamba, kuanguka kwa embe hakusababishwi na kitu kimoja pekee. Zipo sababu nyingi ambazo zote zikikutana kwa pamoja, zinapelekea kitu kutokea.
Sasa kwenye maisha yetu, mambo pia huwa yapo hivyo, hakuna kitu chochote kwenye maisha yako, ambacho kinasababishwa na kitu kimoja pekee. Kila kinachotokea kwenye maisha yetu kinasababishwa na mambo mengi ambayo yamekutana kwa pamoja na kuleta matokeo.
SOMA; DARASA LA JUMAPILI; JINSI YA KUFIKIRI KWA KINA NA KUFANYA MAAMUZI SAHIHI.
Kwa mfano kama kipato chako ni kidogo, ni rahisi kuamini ni kwa sababu unalipwa kidogo. Lakini hiyo siyo sababu pekee. Kipato kidogo kinachangiwa na mambo mengi, ikiwepo ufanisi wako wa kazi, njia ulizonazo za kuingiza kipato, mambo unayovumilia na hata kuridhika au kukataa tamaa kwenye kipato hicho.
Kadhalika kwenye biashara na hata maisha kwa ujumla, biashara inapokufa, hakuna kitu kimoja pekee kinachosababisha, bali vitu vingi vinakutana. Hata mahusiano yanapovunjika, watu hupenda kusingizia sababu moja, lakini kwa uhalisia kunakuwa na sababu nyingi ambazo zinawafanya watu wachokane na kuona hakuna haja ya kuendelea kuwa pamoja.
Kwa kujua hili, inatusaidia kutatua matatizo mbalimbali tunayopitia, kwamba tusihangaike na kitu kimoja, bali tuhangaike na vitu vingi. Tuangalie kila kinachohusika na kukifanyia kazi ili kuweza kutatua au kuzuia tatizo lisitokee.
Kila kitu unachopitia kwenye maisha yako, kimesababishwa na mambo mengi, yajue na uyafanyie kazi ili kuleta mabadiliko.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog