Kuzaliwa, kuishi na hata kufa imekuwa ni fumbo kubwa kwa uelewa wetu sisi binadamu. Kuna watu wanazaliwa na kufa hapo hapo au muda mfupi baada ya kuzaliwa, kuna watu wanazaliwa na kuishi maisha ya taabu na wengine kuishi maisha marefu. Lakini mwisho wetu sote ni kifo. Japokuwa hatujui ni wakati gani hasa tutakufa, wote tunajua tutakufa.

Siri ya maisha na kifo lilikuwa swali ambalo Paul Kalanithi alikuwa akijiuliza kwa maisha yake yote.

Paul alikuwa mwandishi na daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, moja ya kazi ngumu na inayohitaji muda kwenye kujifunza na hata kuifanya. Katika maisha yake ya utoto na hata ujana, Paul hakuwahi kufikiri angekuja kuwa Daktari, na hivyo alisoma sanaa na lugha katika elimu yake ya chuo.

Lakini swali la kuelewa maisha na kifo, lilimsukuma kusoma baiolojia na hatimaye kusoma udaktari na baadaye kusomea udaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu. Lakini kwa bahati mbaya sana, Paul hakuweza kuhitimu masomo yake ya udaktari bingwa, wakati anafikia kileleni kabisa mwa mafunzo hayo, aligundulika kuwa na saratani ya mapafu ambayo ilikatisha maisha yake akiwa bado mdogo.

Kwenye kitabu cha kumbukumbu yake cha WHEN BREATH BECOMES AIR, Paul anatushirikisha safari ya maisha yake, tangu utoto, kusoma, udaktari na hata safari ya miaka saba ya kusomea udaktari bingwa ambayo hakufanikiwa kuikamilisha.

when breath becomes air

Kitabu hichi kina nguvu kubwa sana kwetu kuyaangalia maisha kwa mtazamo mwingine. Tumekuwa tunachukulia vitu kwa urahisi sana, wakati ndiyo vitu muhimu sana kwenye maisha yetu. Pia kitabu hichi kinatufundisha kuchagua kile hasa unachojali kwenye maisha, bila ya kujali watu wanasema nini.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hichi cha WHEN BREATH BECOMES AIR, tujifunze siri kubwa iliyojificha nyuma ya maisha na kifo.

 1. Tangu akiwa mtoto, Paul hakuwahi kufikiria kama atakuwa daktari. Licha ya baba yake na ndugu zake wengine kuwa madaktari, hakuwa na kitu kinachomsukuma kuwa daktari. Wakati anafika wakati wa kuchagua akasome nini chuoni, alichokuwa anafikiria ni uandishi. Alipenda sana lugha, alipenda falsafa na kupenda kuandika. Lakini haya aliyaweka pembeni alipochagua kurudi kusoma udaktari, na alipofika mwisho wa maisha yake, alirudi kwenye uandishi. Hili linatufundisha kwamba, ndoto unazokuwa nazo ukiwa mtoto au kijana unaweza kuziacha kwa sababu mbalimbali, lakini ndiyo ndoto unazohitaji zaidi kwenye maisha yako.
 2. Moja ya vitu vilivyomfanya asivutiwe na udaktari akiwa mtoto ni kumkosa baba yake. Baba yake alikuwa daktari na alifanya kazi kwa muda mrefu wa siku, aliondoka asubuhi kabla watoto hawajaamka na kurudi usiku wakiwa wameshalala. Paul aliona hayo siyo maisha anayotaka kuenda nayo. Hii inatuonesha namna gani kazi na mambo mengine tunayofanya kwenye maisha yanaweza kuwa mfano mzuri au mfano mbaya kwa wale wanaotuangalia.
 3. Katika kutafuta maisha, baba yake Paul alihamisha familia yake jini la New York kwenda maeneo ya vijijini Arizona, eneo walilohamia lilionekana kuwa chini kielimu. Mama yake aliumizwa na hilo na kuhakikisha pamoja na eneo kuwa chini kielimu, watoto wake watapata elimu bora. Na hivyo alikuwa akiwapa vitabu na kutaka wavisome tangu wakiwa wadogo. Hili liliwajengea watoto wake mapenzi kwenye kusoma na elimu kwa ujumla.
 4. Usomaji wa vitabu ulimfanya Paul kuanza kujiuliza maswali magumu kuhusu maisha na kifo. Alisoma kazi za wanafalsafa mbalimbali na kushangazwa namna akili za binadamu zinavyofanya kazi, asili ya vitu na kutaka kujua zaidi kuhusu maisha na kifo. Hili lilimfanya kuchagua kusoma udaktari ili kuyajua zaidi maisha na pia kusomea udaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo kujua zaidi namba ubongo na akili zetu zinavyofanya kazi.
 5. Kupitia udaktari, Paul aliamini ndiyo angeweza kuyaelewa zaidi maisha, kuelewa siri ya maisha na kifo, na kuelewa jinsi ambavyo akili zetu zinafanya kazi.
 6. Mwaka wa kwanza wa udaktari haukuwa rahisi kwa Paul. Kuanza kupasua maiti ili kujifunza mwili wa binadamu ulivyo halikuwa zoezi rahisi kwake. Zoezi la kupasua maiti liliondoa utu kwa zile maiti na kuishia kuwa vitu vya kujifunza. Hili lilikuwa funzo kubwa sana kwenye maisha yake, kwamba kazi yake inayofuata ya udaktari, itafikia hatua wagonjwa wanaacha kuwa watu na kuwa kazi.
 7. Kwenye shule ya udaktari ndipo Paul alipoona kwa ukaribu uhusiano baina ya maana, maisha na hata kifo. Aliona mateso ya watu na kifo kinavyowakuta. Aliona jinsi binadamu, kama viumbe na vitu vingine duniani, vinavyotawaliwa na sheria za asili na mwisho wa kila kitu ni kifo.
 8. Siku ya kwanza kujifunza kupitia wagonjwa, ilikuwa siku ya kwanza kwa Paul kushuhudia uzazi na kifo kwa wakati mmoja. Katika siku hiyo ya kwanza, mama mjamzito aliyekuwa na ujauzito wa mapacha wawili, alikuwa kwenye hali mbaya, kitu kilichopelekea maamuzi ya upasuaji yafanyike haraka. Lakini mimba ilikuwa na miezi mitano na wiki tatu, na hivyo watoto hao walikuwa wadogo sana kuweza kuishi, walikufa muda mfupi baada ya kuzaliwa. Hili lilifanya Paul azidi kuona namna ambavyo maisha yana siri kubwa.
 9. Kusudi kubwa la Paul ilikuwa kukielewa kifo, kukutana na kifo uso kwa uso na kukichunguza kwa undani, kwa nini watu wanakufa na kwa nini watu hawawezi kujua wanakufa lini na wanakufaje. Udaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu ulionekana kuwa sehemu yenye majibu sahihi kwake, kwa sababu kupitia ubingwa huo, ataelewa ubongo, akili na ufahamu.
 10. Safari ya udaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu haikuwa fupi wala rahisi, ni safari ya miaka saba ambayo ilikuwa na vitu vingi vya kujifunza. Kufanya kazi kwa masaa mpaka 100 kwa wiki, kuhudumia majeruhi waliopata ajali na hata kufanya upasuaji wa ubongo kwa watu waliokuwa na uvimbe na kansa kwenye ubongo.
 11. Kazi kubwa kwake kama daktari bingwa mafunzoni haikuwa kuokoa maisha, kila maisha yana mwisho, bali kazi kubwa ya Paul ilikuwa kuwafanya wagonjwa na familia kuelewa ugonjwa na kifo pia. Aliona kwa kuwasaidia watu kuelewa hili, wangeacha kujilaumu wenyewe au kulaumu madaktari pale wagonjwa wao wanapokufa. Kwa kuona labda kama kuna kitu wangeweza kufanya kuokoa maisha, au kama madaktari wangechukua hatua fulani basi asingekufa.
 12. Safari ya kujifunza udaktari bingwa pia haikukosa majuto, yapo makosa mengi ambayo Paul aliyafanya katika kujifunza, hasa kufanya upasuaji ambao una hatari kubwa na baadaye mtu kupata kilema cha maisha yake yote. Hili lilimfundisha kwamba hata uwe na uelewa kiasi gani, kama daktari kukosea kupo na kuna mambo mengine huwezi kuyaingilia au kuyafanya kuwa bora zaidi.
 13. Wakati anaelekea kwenye mwaka wa mwisho wa masomo yake ya udaktari bingwa, huku akiwa ameshajizolea kila sifa na zawadi kwa ufanisi wake mzuri, Paul alianza kupata dalili za magonjwa ambazo hazikueleweka. Alipoteza uzito kwa kiasi kikubwa, kuchoka sana na hata maumivu ya kifua. Mwanzo alifikiri ni kazi kuwa nyingi na kujipa moyo kwamba ndani ya mwaka mmoja yote yatapita. Japo alijua kuna jambo kubwa linaendelea kwenye mwili wake, kwa kuwa yeye ni daktari, hakutaka kukubali kwa haraka.
 14. Kwa kuona hali inazidi kuwa mbaya, Paul aliamua kufanya vipimo na ndipo alipogundulika kwamba ana kansa ya mapafu ambayo imeshaanza kukua kwa kasi kubwa. Haikuwa rahisi kwake kukubali matokeo yale, hivyo alirudia vipimo na vyote vilionesha kwamba ana kansa. Kwa kugundulika huku kwamba ana kansa, kulibadili maisha yake yote, kutoka kuwa daktari anayewapa habari wagonjwa kuhusu ugonjwa wao na matokeo yake, mpaka kuwa mgonjwa akipewa taarifa kuhusu ugonjwa wake na matokeo yake.
 15. Hali mpya ya kuwa daktari na wakati huo huo kuwa mgonjwa ilimweka Paul njia panda, hakujua ajiweke upande upi. Akijiweka kama daktari hawezi kujitibu tatizo lake, na akijiweka kama mgonjwa aliona kuna vitu atavikosa, kwa kuwa madaktari huwa hawasemi kila kitu kwa wagonjwa wao. Hili lilimtesa na kumsumbua sana, hakuamini sasa yupo upande wa pili, kama mgonjwa na siyo kama daktari.
 16. Baada ya mvutano wa ndani wa muda, Paul alikubali kuwa mgonjwa na kuchagua daktari wa kumhudumia kwa hali yake. Lakini alitaka daktari yule awe muwazi kwake, mfano alitaka amwambia ana miaka mingapi ya kuishi tangu kipindi hicho, kitu ambacho daktari wake hakutaka kumwambia. Hilo lilimfanya ajisikie vibaya lakini hakuwa na namna. Alichomwambia daktari wake ni kama akijua ana miaka zaidi ya kumi ya kuishi basi atarudi kwenye upasuaji, na kama ana chini ya miaka mitano basi atarudi kwenye uandishi.
 17. Baada ya vipimo, Paul aligundulika aina ya kansa aliyonayo ingeweza kutibiwa na dawa moja badala ya dawa kali za kutuliza kansa. Hii ilikuwa habari njema kwake na alianza matibabu. Baada ya kuanza matibabu afya yake iliimarika, aliamua kuanza kurudi kwenye upasuaji na kumalizia shule yake, kitu ambacho aliweza taratibu. Wakati anaendelea na matibabu aliendelea kufanya vipimo na alikuwa anaendelea vizuri.
 18. Katika vipimo alivyokuwa anaendelea navyo, alikuja kugundua kuna kansa mpya imeanza kukua, kiashiria kwamba daa aliyokuwa akitumia imeshindwa. Hili lilipelekea kubadilishiwa matibabu na kuanzishiwa dawa kali za kuua seli za kansa, kitu ambacho kilimfanya asiweze tena kuendelea na kazi za upasuaji. Licha ya kuwa amebakisha miezi tu kuhitimu udaktari bingwa.
 19. Wakati akiendelea na matibabu ya dawa kali za kansa, ambazo zilifanya mwili wake kudhoofu sana, alipewa taarifa kwamba bodi ya maprofesa imeridhia atunukiwe udaktari bingwa kwa kuwa alikuwa ameshakamilisha karibu kila anachopaswa kukamilisha. Lakini siku ya kutunukiwa, alianza kuumwa sana, akitapika na kuharisha na mwili kukosa nguvu. Hakuweza kuhudhuriwa kutunukiwa kwake na aliishia kulazwa hospitali, safari ambayo ilikuwa ndiyo ya mwisho kwa maisha yake.
 20. Baada ya dawa kali za kansa nazo kushindwa, hali ya Paul ilidhoofu sana, na alianza kukubali ndani yake kwamba ule ndiyo ulikuwa mwisho wa maisha yake, hakuona haja ya kuendelea kukataa na kuona kwa nini yale yametokea kwa maisha yake, katika kipindi ambacho ndiyo kama alikuwa anayaanza maisha yake ya kikazi kama daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu. Alikuwa ameahidiwa kazi zenye malipo mazuri na kila aina ya maisha aliyotaka, lakini yote hayo hayakuwezekana.
 21. Ndani ya miaka miwili tangu kuambiwa ana kansa, Paul alifariki dunia, akiwa katika maumivu makali na kushindwa kupumua. Alikuwa na nafasi ya kuwekwa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua, lakini hilo lisingesaidia kwa sababu mapafu yake yalikuwa yameharibiwa vibaya na kansa. Hivyo alikubali kuruhusu kifo kimfike, akiwa amezungukwa na familia yake, kuanzia wazazi mpaka mke na mtoto.
 22. Yapo mengi sana tunaweza kujifunza kuhusu maisha na kipo kupitia kitabu hichi kinachoelezea maisha ya Paul, ni safari ya kusikitisha, lakini kikubwa cha kuondoka nacho ni kwamba, tuishi kwa wakati ambao tupo, hatujui nini kitakachotokea kesho, hivyo kila nafasi tunayoipata, tuiishi kwa ukamilifu, tufanye yale ambayo ni muhimu kwetu na tunayojali. Na pale mambo yanapotutokea kwenye maisha yetu, tusikatae na kuona labda hatustahili, mambo mabaya yanatokea kwa kila mtu.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji