Watu wa kawaida, wanapowaangalia watu waliofanikiwa huwa wanaona kama watu hao wanajitesa. Huwa wanaona watu hao licha ya kuwa na fedha nyingi, maisha yao ni ya kawaida sana na wanaendelea kuweka juhudi kubwa kwenye kazi zao kama vile ndiyo wanaanza.

Watu wa kawaida hujiambia kama wakiwa na fedha kama walizonazo watu waliofanikiwa basi wangeishi maisha ya raha mustarehe, kupata kila wanachotaka, kutokuumia tena na kazi na kadhalika.

Jua

Ukiwaangalia hata wale watu ambao tayari wameshafikia uhuru wa kifedha, kwamba hata kama wasipofanya kazi maisha yao yote, wana fedha za kuwatosha kuendesha maisha yao, ndiyo wafanyaji wakubwa wa kazi. Hii ni kwa sababu wanachofanyia kazi siyo fedha, bali maono na ndoto kubwa walizonazo.

Sasa, kinachowafanya watu hawa waliofanikiwa kuwa na maisha ya kawaida licha ya kuwa na fedha nyingi ni kwa sababu wanachokazana nacho ni ndoto zao kubwa na siyo kingine. Hivyo kama wataruhusu maisha yawe mteremko, wapate kila wanachotaka, inakuwa rahisi kusahau ndoto zao kubwa.

SOMA; UKURASA WA 719; Njia Ya Kuwa Bora Ni Ngumu, Lakini Nzuri Kusafiri…

Ukishaanza kuwa na vitu vingi ambavyo siyo muhimu, unakuta akili yako inapotelea kwenye vitu hivyo badala ya kuitumia kufikia ndoto kubwa ulizonazo.

Kadiri unavyofanikiwa, kazana kuwa na kiasi, hasa kwenye vitu unavyokuwa na maisha. Ukishaanza kuwa na chumba kizima kimejaa nguo tu, ukawa na magari mengi ya kifahari ya kutembelea, ukawa unakula kila aina ya chakula na kila aina ya vinywaji, ukawa unapata kila aina ya mapumziko na starehe, utakuwa na muda gani wa kuendelea kupigania ndoto kubwa za maisha yako?

Labda kama huna ndoto kubwa, na kama huna jua kabisa hutatoka kwenye hayo maisha uliyopo sasa, kwa sababu utaishia kuwa mtumwa wa wengine na kuwa mtumwa wa vitu. Utumwa huo utadumaza akili yako na hutaweza kupiga hatua kubwa.

Mara zote kwenye maisha yako, ongozwa na ndoto kubwa ulizonao. Hata kwa sekunde moja usitoe macho yako kwenye ndoto yako. Kitu pekee kinachopaswa kutawala akili na mawazo yako kinapaswa kuwa ndoto kubwa ya maisha yako.

Mtu mmoja amewahi kusema hofu ni kile unachoona unapotoa macho kwenye ndoto yako kubwa. Na ninakubaliana naye bila ya shaka yoyote.

Usikubali mteremko wa maisha uwe kikwazo cha wewe kushindwa kufikia mafanikio makubwa. Kadiri unavyofanikiwa, kadiri fedha zinavyokuwa nyingi, ndivyo unavyopaswa kujidhibiti, kuhakikisha matumizi yako hayawi makubwa na yakakutoa kwenye ndoto yako. Siyo kwamba unajitesa, bali unaweka kipaumbele kwenye yale muhimu zaidi.

Punguza utumwa wako kwa wengine na kwa vitu unavyokuwa navyo, na hilo litakupa uhuru wa kufanyia kazi ndoto zako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog