Ndugu mmoja alikuwa ni rubani ambaye kazi zake alikuwa anazifanyia umoja wa mataifa. Alitamani sana na kijana wake awe rubani kama yeye na ikiwezekana afanye kazi pale pale ambapo yeye anafanya hata akistaafu mwanaye ataendelea kufanya kazi pale.

Baba huyo alijitahidi kuwekeza kwa mtoto kweli huku akiwa na matarajio au mategemo makubwa sana juu ya mwanaye huyo wa kiume. Miaka ya kustaafu ya shule ndugu ilifika hivyo akalipwa mafao yake, yule mzee aliamua kutumia fedha yake kwenda kumsomesha kijana wake huko marekani katika chuo cha urubani.

Rafiki, yule kijana alipofika marekani alijifunza vizuri na ikabakia muda kama wa mwaka mmoja kuwa rubani na alishaanza hata kurusha ndege hewani. Yule kijana akajiingiza katika makundi ya madawa ya kulevya ikafikia kipindi yule kijana akashindwa kuendelea na chuo na akajikuta anaacha baada ya kuathirika na madawa ya kulevya.

malezi bora
silhouette of parents and their children on the beach

Huku nyumbani baba akiwa anajua kuwa mwanaye anaendelea vizuri na masomo na amebakiza muda mfupi kumaliza. Kijana madawa yalimteka na hivyo akawa teja akapelekwa katika kliniki za wagonjwa walioathirika na madawa ya kulevya.

Hivyo basi, baadaye alirudishwa nchini Tanzania na baba yake alivyoweka mategemeo makubwa na akiwekeza kwa kijana wake na kumlipia fedha nyingi ambazo aliteseka katika kipindi chake chote cha kufanya kazi hatimaye kijana anarudi nyumbani akiwa ameathirika na madawa.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Craving Mind (Jinsi Tunavyonasa Kwenye Uraibu Na Jinsi Ya Kuvunja Tabia Mbaya.)

Ooh! Mpendwa msomaji, mzee alipomwona kijana yake na akijiangalia na yeye, mzee anaonekana ndiyo kijana na mtoto ndiyo mzee. Kijana madawa yalimchakaza, yule baba alipalalaizi pale pale alimwona mwanaye mpaka leo hii hawezi tena kuongea na watu wakienda kumwona anakuwa na karatasi anamwandikia mtu aliyekwenda kumwona hivi please pray for Innocent akimaanisha tafadhali mwombee Innocent.

Tunajifunza nini katika hadithi hii ya kweli iliyomkuta mzazi ambaye ni mzazi kama leo hii wewe ulivyo au unatarajia kuwa mzazi?

  1. Usiweke matarajio makubwa kwenye kitu chochote hata katika mtoto kwani mambo huwa hayawi kama unavyodhania.
  2. Tegemea kupata chochote, jenga taswira hasi kutarajia kupata chochote hata mambo yakienda hovyo huwezi kuumia kama ndugu yaliyomkuta ya kupalalaizi na kushindwa kuongea.
  3. Mlee mtoto katika misingi bora, misingi itamwongoza popote pale duniani, nyumba ni msingi na mtoto ni malezi na malezi ni msingi.
  4. Futa nadharia kuwa usomeshe mtoto halafu aje akusaidie. Kila mtu na maisha yake kama umeshindwa kujiwekezea sasa hivi ukiweka matarajio kwa mtoto wako ni kujidanganya. Huna mkataba na mtoto wako kwamba utaishi naye milele na watu wanabadilika muda wowote.
  5. Usimchagulie mtoto kusudi la maisha yake, kila mtu ana kitu chake anachokipenda, kila mtu ana sauti yake ya ndani hivyo mwache mtu asikilize sauti yake ya ndani inataka nini. Kumchagulia mtu kitu cha kufanya ni kama kulazimisha maji kupanda juu mlimani.

Hatua ya kuchukua leo, usiweke matarajio makubwa kwa mtoto wako juu ya kitu fulani, wewe jiwekee hamsini kwa hamsini ili mambo yakienda ndivyo sivyo ile hali haitakusumbua sana na kukuumiza kwa sababu ulijiandaa kiakili kupokea matokeo tofauti.

SOMA; Hii Ndio Faida Ya Kutumia Falsafa Ya Imani Ya Kidini Kwenye Malezi Bora Ya Watoto

Kwahiyo, kubali kulipa gharama mapema kwenye kitu chochote, ukikwepa kulipa sasa, utakuja kulipa kwa riba kubwa. Maisha hayana huruma na mtu pale unaposhindwa kuendana na sheria ya asili.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku  ambayo ni www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana !