Rafiki, watu wengi wamekuwa wanatafuta njia ya mkato, ya uhakika na isiyotumia nguvu ya kupata mafanikio kwenye maisha. Iwe ni kupata fedha, kufaulu mitihani, kutatua changamoto, kila mtu anatafuta wapi rahisi pa kupita ili aweze kupata.

Mara zote nimekuwa nasema hakuna njia rahisi, ya mkato na isiyo ya kutumia nguvu ya kupata kitu chochote chenye thamani. Lakini kama ipo njia inayokaribiana na hiyo, basi ni kujiongeza maarifa. Kama mtu atakuwa na maarifa sahihi ya kufanya kitu, basi itakuwa rahisi zaidi kwake kukifanya kuliko mtu asiyekuwa na maarifa hayo.

Hivyo kama unachotaka ni fedha, kuongeza kipato chako, kama una maarifa sahihi kuhusu fedha itakuwa rahisi zaidi kwako kupata na kutunza fedha zako kuliko yule ambaye hana maarifa sahihi kuhusu fedha.

Kadhalika kwenye maeneo yote ya maisha, kama unataka kuwa na mahusiano mazuri, ukiwa na maarifa sahihi yanayohusu mahusiano, itakuwa rahisi kwako kuboresha mahusiano yako kuliko ukiwa huna maarifa ya aina hiyo.

Abraham Lincolin, aliyekuwa raisi wa Marekani, amewahi kunukuliwa akisema, akipewa masaa 6 ya kukata mti, atatumia masaa manne ya kwanza kunoa shoka lake. Na hilo halina siri, kwa sababu ukiwa na shoka kali, kazi ya kukata mti inakuwa rahisi kuliko ukiwa na shoka ambalo ni butu.

Hivi pia ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu, kama una maarifa sahihi, akili yako inakuwa makini, unaweza kufanya maamuzi bora na kupiga hatua. Lakini kama huna maarifa sahihi, akili yako inakuwa butu na unashindwa kufanya maamuzi bora ya kukuwezesha.

Maarifa sahihi tunayapata kwa kujifunza, kupitia kusoma, kuangalia, kusikiliza na kutafakari. Lakini njia kuu kabisa, ambayo kila mmoja wetu anaweza kuitumia kwa ubora kabisa kujifunza ni kusoma. Na ninaposema kusoma simaanishi tu kusoma magazeti au makala, bali namaanisha kusoma vitabu.

vitabu likizo 2017

Leo nakwenda kukupa sababu kumi kwa nini ni lazima popote unapokuwa basi uwe na kitabu. Ninaposema popote, namaanisha popote kweli, kuanzia pembeni ya kitanda chako na hata kwenye kazi yako. Na pia ninazungumzia kitabu halisi, kitabu unachoweza kushika na siyo cha kukaa kwenye simu au kompyuta.

Sababu ya kwanza; vitabu vinakupa maarifa.

Unahitaji maarifa sahihi ili kuweza kufanya maamuzi sahihi. Hakuna njia bora ya kupata maarifa kama vitabu. Licha ya teknolojia kubadilika na kuwa bora zaidi, bado vitabu vina thamani kubwa kuliko kitu kingine chochote. Unaposoma kitabu, unapata maarifa ambayo kama ukiyatumia, maisha yako hayawezi kubaki pale yalipo sasa.

Sababu ya pili; vitabu vinabadili mtazamo wako bila hata ya wewe kujua.

Watu huwa wanawaambia wenzao badili mtazamo wako kama unataka kufanikiwa. Kama vile ni kitu rahisi kusema basi kuanzia sasa nabadili mtazamo wangu! Siyo rahisi hivyo, mtazamo ambao unao, ambao umeujenga kwa miaka mingi, hautavunjika kirahisi kwa kujiambia mara moja. Badala yake unabadilika kidogo kidogo kutokana na ushahidi unaoupata kila siku kwenye maisha yako.

Unaposoma vitabu mara kwa mara, unalisha mawazo yako kitu fulani, sasa vitabu vinapokuwa vya aina moja, basi unaanza kujenga mtazamo unaoendana na vitabu unavyosoma. Hivyo kama unataka kutengeneza mtazamo mzuri kuhusu fedha, hebu soma vitabu kadhaa kuhusu fedha.

Ukitaka kujaribu usahihi wa hili, mwambie mtu anayecheza kamari au bahati nasibu kwamba njia anayotumia kutafuta fedha siyo sahihi, atakupa kila sababu kwa nini ni sahihi, au kwa nini kila kitu ni kamari. Lakini ukimfuata mtu anayesoma vitabu vya fedha na akavielewa, atakuambia kwa nini kucheza kamari na bahati nasibu ni njia ya hovyo kabisa ya kutafuta fedha.

Sababu ya tatu; vitabu vinakupa hoja za kutetea msimamo wako.

Ukiwa mtu wa kusikiliza vitu ambavyo watu wanavisema na wewe ukavibeba kama vilivyo na kuviamini, ni rahisi sana kubadilishwa na mtu yeyote. Kwa sababu mtu akija na hoja hata kama ni za uongo lakini anajiamini, atakufanya uone unachoamini wewe siyo sahihi.

Lakini ukiwa msomaji wa vitabu, unakuwa na hoja nyingi za kutetea kile unachoamini, kile unachosimamia. Na yeyote atakayekuja kwako kutaka kukuaminisha vinginevyo, utaweza kumjibu kwa hoja ambazo zitamfanya naye afikiri zaidi.

SOMA; Vitabu Saba Siku Saba Za Mafanikio Makubwa Kwa Mwaka 2018 (Zawadi Ya Vitabu Kwako Rafiki Yangu).

Sababu ya nne; vitabu vinakusaidia kutumia muda ambao ungepotea wenyewe.

Umewahi kuwa na mkutano na mtu, halafu ukafika muda wa mkutano ule na mtu huyo akachelewa na inabidi umsubiri? Huwa unafanya nini kwenye muda huo? Umewahi kufika eneo la huduma fulani, labda ofisi au hospitali na unapaswa kusubiri kwenye foleni ndefu? Umewahi kwenda benki kuweka au kutoa fedha na ukasimama kwenye foleni kwa zaidi ya nusu saa? Karibu kila ninayemfahamu amewahi kuwa kwenye nyakati kama hizo, ambapo muda unapotea lakini huna namna ya kuuokoa, kwa sababu lazima usubiri.

Hizo sasa ndizo nyakati unazoweza kuziokoa kwa kutoa kitabu chako na kuanza kukisoma. Ukiwa unasubiria kitu chochote, kama itakuchukua zaidi ya dakika tano, basi toa kitabu na usome. Kwa dakika tano, utasoma siyo chini ya kurasa 2 ambazo zitakupa kitu kipya. Sasa ukikaa dakika 30 au saa moja, utasoma siyo chini ya kurasa 10.

Sababu ya tano; kitabu kitakufanya uonekane mjanja.

Siku hizi, kila eneo ambalo lina mkusanyiko wa watu ambao wanafanya au kusubiri kitu fulani, kila mtu utamkuta ameinama kwenye simu yake. Kila mtu anakazana na kile ambacho kinaweza kushika akili yake kwa wakati huo. Iwe ni mawasiliano au kuzurura kwenye mitandao ya kijamii.

Sasa kwenye maeneo kama hayo wewe ukawa na kitabu, ukawa ‘bize’ na kitabu chako, kila mtu atakuwa anaona wewe ni wa tofauti, kila mtu atakuwa anakushangaa wewe.

Nimekuwa naona hili mara nyingi, nikiwa eneo lenye watu wengi, halafu nikatoa kitabu na kusoma, lazima kuna mtu baadaye huja kuuliza ni kitabu gani na anawezaje kukipata.

Sababu ya sita; kitabu kitakuunganisha na wasomaji wengine.

Ukitembea na kitabu, na kila nafasi unayoipata ukatoa kitabu chako na kusoma, unajiweka kwenye nafasi ya kujuana na wasomaji wengine. Mara nyingi nimekuwa najuana na watu wapya kupitia vitabu. Mtu anakuja na kuuliza kitabu gani na hapo mazungumzo kuhusu vitabu yanaanza.

Watu huwa wanalalamika kwamba hakuna wasomaji wa vitabu, anza kusoma vitabu na utaona jinsi wasomaji walivyo wengi.

Sababu ya saba; vitabu vinakuwezesha kuishi maisha ya wengine.

Unaposoma kitabu ambacho kimeandikwa na mtu aliyeishi miaka 2000 iliyopita, unakuwa umepata nafasi ya kuishi maisha yake, katika kipindi hicho kilichopita. Unajifunza yale ambayo yalifanyika kipindi hicho na kwa namna gani waliweza kupiga hatua.

Unaposoma kitabu cha kurasa 300 ambacho mwandishi ametumia miaka na miaka kukitafiti, unakuwa umekusanya yote anayoyajua mwandishi kwa wakati mmoja na urahisi zaidi.

Kama husomi vitabu, unakosa nafasi ya kuishi maisha ya wengine, na ni kitu kinachofanya maisha yako yakose hamasa ya kuishi.

Sababu ya nane; kitabu kitakuepusha na majungu.

Majungu na umbeya huwa vinaanza pale watu wanapokuwa hawana kitu cha kufanya. Hivi umewahi kukuta watu walioko kwenye kazi ya dharura, inayohitajika haraka wakianza kujadili watu wengine? Huwa haitokei. Sasa kama kazi unayofanya inakupa nafasi ya kuwa na muda mwingi wa kutokuwa na kazi, basi kuwa na kitabu kunakuepusha na majungu.

Maana muda ambao huna kazi, basi unafungua kitabu chako na kusoma. Hapo hata wale wanaokuja na habari za wengine, hawatakuwa na nafasi ya kukupa habari hizo.

SOMA; Huu Ndiyo Uwekezaji Bora Kabisa Unaokufanya Wewe Kuwa Tajiri Kwenye Maisha Yako.

Sababu ya tisa; kitabu kitawafanya watu waheshimu muda wako.

Watu wakiona mtu anatumia simu, huwa wanasema anachezea simu, hasa kama huonekani unaongea na simu, basi kushika kwako simu tu, watu wanajua labda upo kwenye mitandao ya kijamii au unafanya mambo yasiyo muhimu. Hata kama umeshika simu na unasoma kitabu, ni vigumu kuwashawishi watu unasoka kitabu.

Lakini unaposhika kitabu na ukawa unasoma, mara moja watu wanaanza kuthamini muda wako. Huwezi kusikia mtu anasema aliyeshika kitabu anachezea kitabu. Hivyo watu wanaheshimu muda wako, na siyo rahisi kuja kwako kwa jambo ambalo siyo muhimu.

Sababu ya kumi; kitabu kitakupa njia mbadala.

Ukiwa unafanya kitu, halafu ukakwama na kila ukifikiria hupati njia, pumzika kitu hicho kwa muda na chukua kitabu usome. Hata kama kitabu hicho hakihusiani na kile unachofanya, wewe ondoa mawazo yako kwenye kile unachofanya na yaweke kwenye kitabu unachosoma. Siyo muda mrefu utapata njia ya kufanya kile ambacho umekwama.

Hii ni njia ambayo huwa inafanya kazi mara zote, sijui kwa nini inafanya kazi, ila kwa hakika inafanya kazi, itumie.

Wito wangu kwako rafiki yangu, nunua na tembea na kitabu popote unapokuwa, hata kama kitakuwa ni kitabu kimoja, fanya hivyo. Kitakupa manufaa mengi, zaidi ya haya kumi niliyokutajia hapa.

Nasisitiza tena, nilichokushauri hapa ni kuwa na kitabu halisi, najua kuna vitabu vya nakala tete, mimi binafsi navisoma hivyo kwa wingi sana, na pia naandika vitabu hivyo, lakini bado huwa natembea na vitabu halisi, siyo kimoja, bali vitabu kadhaa, na kila ninapopata nafasi kwenye siku yangu, natoa kitabu na kusoma.

Kama umekuwa unapenda kusoma vitabu lakini unakwama, hujui upate wapi vitabu au hujui utapataje muda wa kusoma kwa sababu umebanwa sana, ninayo programu maalumu kwako, programu hii inaitwa KURASA KUMI ZA KITABU. Kupata maelezo kuhusu programu hii na jinsi ya kujiunga, tuma ujumbe kwa njia ya wasap namba 0717396253 wenye maneno KURASA KUMI na utapata maelekezo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji