Rafiki, kufumba na kufumbua juma namba 11 la mwaka huu 2018 linakwisha. Kitu pekee ambacho unaweza kueleza kuhusu kila juma linalopita ni jinsi ulivyoishi, mambo uliyofanya na jinsi ulivyogusa maisha ya wengine.

Kama kila siku unaishi kwa mazoea, kufanya kile ulichofanya jana huku ukiwa hujui kwa hakika ni wapi unakwenda, huwezi kufika mbali. Juma litaanza na juma litaisha, mwaka utaanza na mwaka utaisha, halafu siku moja utastuka na kusema hivi muda umeenda wapi.

Ndiyo maana kila wiki nimekuwa nakuletea mkusanyiko wa mambo matano muhimu, huku nikikukumbusha kuipitia wiki yako inayoisha na kuipangilia wiki inayoanza.

Karibu kwenye TANO ZA JUMA LA 11 tunalomaliza, nikushirikishe mambo matano muhimu ambayo nimejifunza na kukutana nayo, ambayo kuna kitu unaweza kujifunza na kuchukua hatua ili maisha yako kuwa bora zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; TWO AWESOME HOURS.

Kila mtu ambaye amekuwa anashindwa kupiga hatua kwenye maisha yake, huwa ana sababu nyingi za kusema, na moja ya sababu zinazotajwa na kila mtu ni muda. Hivi ni nani asiyejua kwamba muda wa sasa hautoshi, ukizingatia kila tunachotaka kufanya, kuanzia maisha ya kawaida, kazi na biashara zetu, halafu ukaja kwenye maisha ya kijamii, tunatamani tungepeta angalau muda zaidi.

Vimeandikwa vitabu vingi sana kuhusu muda, lakini bado muda ni changamoto kwa wengi. Hivyo mwandishi na mwanasayansi wa ubongo na mishipa ya fahamu, Josh Davis, anatuambia tunahangaika na muda kwa namba ambayo siyo sahihi. Anatuambia mambo mengi tunayofanya kujaribu kuokoa, kudhibiti au kutunza muda, siyo sahihi, ndiyo maana kadiri tunavyokazana tupate muda zaidi, ndivyo muda unazidi kuwa adimu.

Kwa mfano tabia ya watu kupenda kuanza kufanya vitu ambavyo ni rahisi na vya haraka kwa siku, ili wakimalizana navyo wawe na muda wa kufanya yale ambayo ni makubwa, ina matokeo mabovu kabisa. Kwa sababu sisi binadamu siyo kama kompyuta kwamba muda wote ukiwasha inafanya kazi kwa viwango vya juu. Akili zetu huwa zinachoka kadiri zinavyofanya maamuzi, hivyo kuanza kufanya mambo madogo madogo, kama kujibu email, hata kama hayachoshi mwili, yanachosha akili, hivyo baadaye unapotaka kufanya makubwa, akili haiwezi na hivyo unaishia kuahirisha.

Katika kitabu chake cha TWO AWESOME HOURS, Josh anatuambia kwamba kila mtu anaweza kupata masaa mawili na zaidi kwenye siku yake, iwapo atajua njia bora za kutumia akili na mwili wake.

Na katika kitabu hichi anatushirikisha mbinu tano za kupata muda zaidi kwenye siku zetu.

Mbinu ya kwanza; tambua hatua zako za kufanya maamuzi.

Mwandishi anasema kwamba, hakuna wakati tunaoupoteza kwenye maisha yetu kama wakati ambao tunapata fursa ya kufanya maamuzi. Na anachosema mwandishi ni kwamba, unapokuwa unafanya kitu kimoja, halafu ukakimaliza, ule wakati umemaliza, hupaswi kukimbilia kufanya kitu kingine. Badala yake tumia muda huo kufikiria na kupanga kipi muhimu kinachofuata. Anachotuambia mwandishi ni kwamba, huwa tuna tabia ya kufanya vitu kwa mazoea, hatufikirii umuhimu wa kitu, tunafanya tu, mwisho wa siku tunajikuta tumechoka huku hatuoni kipi kikubwa tumefanya.

Panga kufanya kitu kimoja, ukikimaliza kabla hujaenda kwenye kitu kingine, tumia muda huo kufanya maamuzi sahihi ya kipi kifuate.

Mbinu ya pili; dhibiti nguvu yako ya kiakili.

Hapa ndipo watu wengi hupotea, wanaianza siku wakiwa na akili yenye nguvu ya kufanya maamuzi na hata kazi zinazohitaji watu wafikiri. Lakini wanachezea nguvu hiyo kwa maamuzi ya hovyo halafu inapofika wakati wanahitaji akili zao kwa mambo muhimu, zinakuwa hazina nguvu. Hii ni sawa na kuiweka simu kwenye chaji usiku kucha, asubuhi ukaamka na kuikuta imejaa asilimia 100, halafu ukaanza kucheza game mpaka ikafika asilimia 10, kisha ukataka kuanza kupiga simu, hapo hapo inakuletea ujumbe kwamba BATTERY LOW. Sasa mara nyingi umekuwa unatumia akili yako wakati ipo kwenye BATTERY LOW, unatumia nguvu yako ya kiakili vibaya, kwa kuzurura kwenye mitandao ya kijamii, kufuatilia habari na mengine yasiyo muhimu.

Tenga muda wako wa asubuhi kwa zile kazi ambazo ni muhimu, zinahitaji akili yako kwa umakini na zinakutaka ufanye maamuzi magumu. Angalau saa moja au mawili ya mwanzo ya siku yako, usiangalie simu yako, wala kuangalia habari zozote, wewe ni kufanya yale muhimu. Jaribu hili na litakusaidia sana.

Mbinu ya tatu; acha kupigana na kelele.

Tunaishi kwenye dunia yenye kelele za kila aina, simu ya mkononi tuliyonayo, ina kelele za kila aina, mitandao ya kijamii, habari mbalimbali na mawasiliano ya watu mbalimbali. Huwa tunajidanganya kwamba tunaweza kudhibiti kelele hizo, kwa kupigana nazo na kuzishinda. Mwandishi anatuambia hilo ni jambo la hovyo sana, kwa sababu hata kama utapigana nazo na kuzishinda, mwisho akili yako itakuwa imechoka kiasi kwamba haiwezi kufanya yale muhimu.

Hivyo dawa ni kuondokana kabisa na kelele, siyo kupigana nazo, bali kuziepuka. Hivyo kaa kwenye mazingira ambayo hayana kelele zinazokuondoa kwenye yale muhimu unayofanya. Mfano kuwa mbali na simu yako wakati unafanya kazi zilizo muhimu. Au kuepuka kabisa kuwa na programu za mitandao ya kijamii kwenye simu yako, ili uepuke tamaa ya kutaka kuangalia kujua nini kinaendelea.

Mbinu mbili za mwisho ni kutumia vizuri uhusiano wako wa akili na mwili na kufanya eneo lako la kazi kuendana na wewe. Hizi nitakuja kuzielezea vizuri wakati mwingine.

Muhimu ni kuhakikisha unatumia vizuri akili yako, mwili wako na mazingira yako kuhakikisha unafanya yale muhimu kwanza kwenye siku yako kabla hujaingia kwenye yale ambayo siyo muhimu. Na nidhamu inahitajika sana kwenye hili.

#2 MAKALA YA WIKI; SABABU KUMI KWA NINI NI LAZIMA UWE NA KITABU POPOTE UNAPOKUWA.

Linapokuja swala la kusoma vitabu, kwa kweli, kutoka ndani ya moyo wangu nikuambie tu huwa sielewi watu ambao hawasomi vitabu. Huwa naona kama ni watu ambao wanaruhusu akili zao zenye uwezo mkubwa zioze, wasizitengeneze vizuri ili ziweze kuwasaidia. Na kwa dunia ya sasa tunayoishi, ambayo habari hasi zinaufuata mpaka ukiwa kitandani kwako, kusoma vitabu vizuri kumekuwa muhimu kuliko kipindi kingine chochote.

Ndiyo maana nimekuwa nasisitiza sana usomaji wa vitabu. Na kwa kila sababu ambazo watu wanazo kwa nini hawasomi vitabu, nimeshazipatia suluhisho kupitia programu ya KURASA KUMI ZA KITABU. Hivyo yeyote asiyesoma vitabu, hana sababu yoyote, bali tu ni mtu mzembe aliyeamua kuozesha akili yake na kushindwa kuitumia kwa ufanisi wa hali ya juu.

Makala ya wiki hii nimekupa sababu kumi kwa nini unapaswa kuwa na kitabu halisi popote pale unapokuwa. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, isome sasa hapa na kisha chukua hatua. Makala; Sababu Kumi(10) Kwa Nini Ni Lazima Uwe Na Kitabu Popote Unapokuwa. (https://amkamtanzania.com/2018/03/15/sababu-kumi10-kwa-nini-ni-lazima-uwe-na-kitabu-popote-unapokuwa/)

#3 HABARI KUBWA YA WIKI HII; TUMEMPOTEZA MWANASAYANSI NGULI WA ZAMA ZETU.

Kila zama hapa duniani, pamekuwepo na wanasayansi ambao wamekuwa wanabadili kabisa jinsi watu wanavyoelewa mambo. Yaani wanakuja na nadharia ambazo zinabadili kabisa uelewa wa watu juu ya vitu fulani. Kwa mfano zamani watu walijua na kuamini kwamba jua linaizunguka dunia na dunia siyo duara bali ni kama meza, na yeyote atakayeenda mbali zaidi ya alipo, atafika ukingo wa dunia na kuanguka. Wanasayansi Copernicus na Galileo walikuja na nadharia zilizoonesha kwamba hili siyo sahihi, na sasa tuna uelewa sahihi kwamba dunia inazunguka jua, na dunia ni duara. Mwanasayansi Newton alikuja na nadharia zilizobadili kila kitu kuhusu mwendo na nguvu ya mvutano wa dunia. Mwanasayansi Einstein alikuja na nadharia kuhusu nishati na mwanga, na nadharia zake zimeweza kutumika kutengeneza silaha hatari sana duniani.

Wanasayansi hao wengi wameishi miaka mingi iliyopita, hivyo wengi tumekuwa tunasoma habari zao tu. Lakini kwenye zama zetu hizi tumepata nafasi ya kushuhudia mwanasayansi aliyebadili kabisa uelewa wa watu kuhusu dunia ilipotoka, ilipo sasa na inapokwenda. Huyu ni mwanasayansi aliyeweza kuzielezea dhana mbili kuu za sayansi ya sasa, BLACK HOLES na GUANTUM MECHANICS kwa njia ambayo kila mtu anaweza kuielewa na kuona namna gani inafanya kazi.

Mwanasayansi huyu ni Stephen Hawking ambaye alifariki juma hili, tarehe 14/03/2018 akiwa na miaka 76. Ni mwanasayansi aliyewashangaza wengi kwa maisha yake, ambayo hakuwa akiweza kutumia kabisa mwili wake, baada ya kupata ugonjwa wa kupooza. Hivyo kwa miaka zaidi ya 50, amekuwa akitumia akili yake tu, na msaada wa vifaa vya kumwezesha kutoa sauti na hata kusogeza mwili wake.

Yapo mengi ya kujifunza kuhusu maisha na sayansi kupitia maisha na nadharia za kisayansi za Stephen Hawking ambaye ametuacha kwenye dunia hii, ambayo alitumia maisha yake yote katika kuielewa, na kutupa maarifa yanayotufanya tuielewe dunia zaidi.

stephen hawking

#4 HUDUMA NINAZOTOA; KITABU; PATA MASAA MAWILI YA ZIADA KILA SIKU.

Kama umekuwa unapata changamoto ya muda, na kutamani ungeweza kupata muda zaidi kila siku, nina habari njema kwako, kwamba muda zaidi unapatikana, ni wewe tu kuchagua jinsi unavyoweza kuiishi siku yako.

Ukichagua vyema jinsi unavyoiishi siku yako unaweza kupata mpaka masaa mawili ya ziada kila siku.

Nimekuandalia maarifa ya jinsi unavyoweza kuipangilia na kuiishi siku yako kwenye kitabu nilichoandika kinachoitwa PATA MASAA MAWILI YA ZIADA KILA SIKU. Kitabu hichi ni softcopy na kinatumwa kwa njia ya email. Unaweza kukisomea kwenye simu yako, kwenye kompyuta yako au kwenye tablet yako.

Gharama ya kitabu hichi ni tsh elfu tano (5,000/=) na kukipata unatuma fedha hiyo kwenda namba 0755 953 887 au 0717 396 253 kisha tuma email yako na jina la kitabu kwenda kwenye moja ya namba hizo na utatumiwa kitabu.

Usikubali tena muda uwe kikwazo kwako kufanikisha ndoto za maisha yako. Muda ni mwingi kama utaweza kuutumia vizuri. Soma kitabu PATA MASAA MAWILI YA ZIADA KILA SIKU na utaweza kutumia muda wako vizuri.

MASAA MAWILI YA ZIADA

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; UNAVYOFUPISHA MAISHA YAKO.

“Life is very short and anxious for those who forget the past, neglect the present, and fear the future.” – Seneca

Mwanafalsafa Mstoa Seneca anatuambia sisi wenyewe tunachagua maisha yetu kuwa mafupi na yaliyojaa wasiwasi pale tunaposahau tulipotoka, tunapopuuzia tulipo sasa na kuhofia tunakokwenda. Kila wakati tunakuwa hatuishi kwa wakati tuliopo, na hivyo wakati huo unapotea, huku tukiwa tumesahau wakati uliopita na kuhofia unaokuja.

Njia bora ya kuishi maisha yetu ni kujifunza kupitia tulikotoka, kuishi kwa wakati ulipo, na kujiandaa vyema kwa wakati ujao, bila ya kuwa na hofu wala mashaka. Ukiishi vizuri leo, sasa hivi kwa wakati ulionao, huna haja ya kuhofia kesho itakuwaje, kwa sababu kesho itakuja na utaishi vizuri kesho pia.

Tunakwenda kuanza juma namba 12 la mwaka huu 2018, kitu kimoja unapaswa kuona ni kwamba majuma yanayoyoma na mwaka unaisha, hivyo usikubali kufanya chochote kwa mazoea, fanya tathmini ya kila juma lako, na pangilia juma kabla hujalianza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog