Kuna watu wengi wanaanzia chini kabisa, wanakuwa na hamasa kubwa, wanaweka juhudi kubwa, na juhudi hizo zinazaa matunda, wanaanza kufanikiwa. Lakini haichukui muda wanaanguka. Watu hawa wanakuwa wamefanya kosa moja kubwa, wanakuwa wameshiba, wanakuwa wamezoa kile ambacho wamekuwa nacho kiasi cha kusahau walipotoka na kilichowafikisha pale walipo.

Dunia Inajiendesha

Watu pia, wanapoanzia chini wanakuwa wanyenyekevu sana, wanathamini na kuheshimu kila mtu. Hata mtu anapoonesha dharau kwao hilo haliwasumbui, wanaachana naye na kusonga mbele. Hali hiyo inawaepusha na matatizo mengi na hivyo kutumia muda na nguvu zao kufanikiwa zaidi. Lakini wanapokuwa wamefanikiwa, wanapokuwa wamepiga hatua kubwa, wanaanza kupoteza heshima na unyenyekevu, wanaanza kujiona wao ndiyo wao na hakuna wa kuwababaisha. Hata mtu anapoonesha dharau kwao, basi huhakikisha wanamfundisha mtu huyo somo.

Kuna vitu viwili ambavyo unapaswa kufa navyo, na ninachomaanisha ni kwamba, hakikisha vitu hivi unaishi navyo kila siku mpaka siku ambayo unaondoka hapa duniani.

SOMA; UKURASA WA 424; Kulinganisha, Unyenyekevu Na Udadisi.

Kwa kuishi vitu hivi kila siku, utakuwa na hamasa ya kupiga hatua zaidi hata kama umefika hatua ya juu kiasi gani. Na pia utajiepusha na changamoto nyingi na kuepusha kuvuruga mahusiano yako na wengine.

Vitu viwili ninavyopenda kukushirikisha leo ni NJAA NA UNYENYEKEVU.

Kila siku kuwa na njaa ya kupiga hatua zaidi, kuwa na njaa ya kuwa bora zaidi. Isitokee hata siku moja ukasema sasa nimefika mwisho, sasa nimeshapata kila ninachotaka, sasa najua kila ninachopaswa kujua. Ikifika siku ya aina hiyo, jua ndiyo mwanzo wa anguko lako.

Kila siku na kila wakati kuwa mnyenyekevu, mheshimu kila mtu na epuka migogoro isiyo na msingi na wengine. Msikilize kila mtu na usimdharau yeyote, hata kama anaonekana hana maana, usioneshe hilo kwa yeyote. Msikilize kila mtu, japo siyo lazima ufanyie kazi kila kitu. Usije kujiona upo bora kuliko wengine, au hakuna wa kukuambia chochote.

Safari ya mafanikio haina kituo cha mwisho, kila siku ambayo upo hai ni siku ya safari, ni siku ya kujifunza na ni siku ya kupiga hatua zaidi. NJAA NA UNYENYEKEVU vitakusaidia sana kwenye safari hii.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog