Hakuna kitu kinawapa watu msongo wa mawazo kwa sasa kama kupata muda wa kufanya kila kitu. Kila mtu ana mambo mengi ya kufanya kuliko muda alionao. Na hivyo kwa kuwa ya kufanya ni mengi kuliko muda, kinachofuata ni msongo.
Kama hiyo haitoshi, bado mambo ya kufanya yanaongezeka, wakati muda haujawahi kuongezeka. Kadiri tunavyokwenda na maisha yetu, majukumu yetu yanaongezeka lakini muda ni ule ule.

Hivyo imekuwa ni kiu ya wengi kutaka kujua wanawezaje kupata muda wa kufanya kila kitu wanachotaka kufanya.
Na hili halina muujiza, ukweli ni kwamba una muda wa kufanya chochote unachotaka kufanya, lakini huna muda wa kufanya kila kitu.
Hii ni kwa sababu hakuna hata anayejua maana ya kila kitu, kwa sababu kila kitu haina mpaka. Kama unataka ufanye kazi ya kuajiriwa, ufanye biashara yako, utembelee mitandao yote ya kijamii, uangalie habari, upige soga na wengine, ukae na familia yako, upokee simu na kujibu jumbe yote hayo ndani ya siku moja, ni kwamba haiwezekani.
SOMA; UKURASA WA 942; Kinachokupoteza Ni Vipaumbele…
Hivyo rafiki, acha kwanza kutaka kufanya kila kitu na anza na kile unachotaka kufanya kweli.
Kwenye kila kitu unachojiambia unataka kufanya, orodhesha kwenye karatasi, orodhesha kila kitu. Kisha mbele ya kila kitu weka alama ya kuonesha umuhimu na uharaka wa vitu hivyo.
Weka alama A kwa vitu ambavyo ni muhimu sana na vinahitajika kwa haraka. Hapa kuna vitu kama ripoti muhimu ambazo tarehe ya kuziwasilisha imefika.
Weka alama B kwa vitu ambavyo ni muhimu sana lakini havihitajiki kwa haraka. Hapa kuna vitu vya kufanyia kazi ambavyo bado tarehe yake haijafika.
Weka alama C kwa vitu ambavyo siyo muhimu lakini vinahitajika kwa haraka. Hivi ni vitu kama simu inayoita ukiwa katikati ya kazi, au mtu anayetaka muongee mambo yasiyohusu kazi unayofanya.
Weka alama D kwa vitu ambavyo siyo muhimu na wala havina haraka. Vitu kama kusoma habari, mitandao ya kijamii.
Na weka alama E kwa vitu ambavyo ni usumbufu kwako, yaani hata hutaki kuviona au kuvisikia. Vitu kama kufuatilia maisha ya wengine, na kujilaumu kwa mambo yaliyopita.
Anza kufanya vitu vyenye alama A, na anza na kimoja mpaka kiishe ndiyo uende kwenye kingine. Ukimaliza A nenda B, kisha fanya kimoja kwa wakati mpaka viishe.
Usifanye vitu vya alama C kama alama A na B havijaisha.
Vitu vyenye alama D usivifanye, achana navyo, ni bora upumzike kuliko kufanya hivyo.
Vitu vyenye alama E vikate kabisa kwenye orodha yako, na hata usivifikirie kabisa.
Fanya zoezi hili kila mwanzo wako wa siku, na utaona jinsi muda wako ulivyo wa kutosha kufanya yale muhimu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog