“There are two things a person should never be angry at, what they can help, and what they cannot.” -Plato

Hongera mwanamafanikio kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo, fursa ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari VITU HIVI VIWILI VISIKUSUMBUE…
Tumekuwa tunaruhusu baadhi ya vitu kutusumbua kwenye maisha yetu kwa namna ambavyo vinatokea.
Vinatuangusha, kutukatisha tamaa, kutukasirisha na hata kutufanya tujione hatifai.
Lakini ukichunguza vitu vyote kwa undani, utagundua kwamba hakuna kinachopaswa kukusumbua.
Na hii ni kwa sababu vitu vyote vinavyotokea kwenye maisha yako vimegewanyika kwenye makundi mawili;

MOJA; Vitu unavyoweza kuviathiri, vilivyopo ndani ya uwezo wako.
Hivi ni vitu ambavyo unaweza kufanya kitu kuvibadili, vipo ndani ya uwezo wako wa kuviathiri, kivifanya kuwa bora zaidi.
Kwa vitu vya aina hii, hupaswi kuviruhusu vikuathiri kwa sababu kuna kitu unachoweza kufanya, hivyo fanya kitu hicho.

MBILI; Vitu usivyoweza kuviathiri, vilivyopo nje ya uwezo wako.
Hivi ni vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wako, vitu ambavyo huna cha kufanya kuvibadili.
Kwa vitu vya aina hii, huhitaji kuviruhusu vikusumbue, kwa sababu huna cha kufanya, hivyo achana navyo.

Kila unapojikuta kwenye kitu ajbacho kinataka kukusumbua, subiri kwa kuda kidogo na jiulize je kitu hichi kipo ndani ya uwezo wangu au nje ya uwezo wangu?
Kama kipo ndani ya uwezo wako, chukua hatua na usikubali kiendelee kukusumbua.
Kama kipo nje ya uwezo wako, achana nacho na kisiendelee kukusumbua.
Kama utaruhusu tena vitu viendelee kukusumbua, hapo sasa unapenda usumbufu wewe mwenyewe.

Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha