Moja ya njia ambazo tumekuwa tunatumia kupata mawazo ya biashara au huduma gani tutoe ni kujiuliza dunia inataka nini kisha kuipatia. Kuangalia thamani gani unayoweza kuitoa kwa dunia na watu wakawa tayari kuilipia.
Swali hili ni dhahiri na linaleta majibu mazuri sana, lakini majibu yake ni mengi na wakati mwingine unaweza usiweze kuchukua hatua. Kwa mfano kama ukigundua dunia inahitaji magari yanayojiendesha yenyewe na wewe haupo kwenye sekta ya magari, unaweza kuona huna hatua ya kuchukua.

Kipo kitu ambacho dunia inakihitaji zaidi na mtu yeyote anaweza kutoa kitu hicho. Kwa kujua kitu hichi, inakuwa rahisi kwa mtu kutoa thamani kubwa kwa dunia na kulipwa kadiri ya thamani anayoitoa.
Kitu ambacho dunia inahitaji zaidi ni watu wanaoishi maisha yao, watu ambao wanaishi maisha halisi, wakifanya mambo halisi na yenye manufaa kwa wengine. Haijalishi mambo hayo ni makubwa au madogo kiasi gani, kiasi cha mtu kuwa halisi, anaaminika na kutegemewa zaidi.
SOMA; UKURASA WA 1099; Tofauti Ya Wabobezi Na Wachanga Kwenye Fani Mbalimbali…
Mtu anapokuwa halisi anakuwa na uadilifu wa hali ya juu, anakuwa mwaminifu, anakuwa wa kujituma na anafurahia chochote anachofanya. Hafanyi tu kitu kwa sababu anategemea alipwe, bali anafanya kwa sababu ndicho anachoweza kufanya, ndiyo sehemu ya maisha yake.
Mwalimu anapofundisha kwa sababu ana kitu cha kutoa ka wengine, mwandishi anapoandika kwa sababu ana ujumbe wa kuwasaidia wengine, mwimbaji anapoimba kwa sababu ana burudani ya kutoa kwa wengine, na kiongozi anaoongoza kwa sababu ana maono makubwa yenye manufaa kwa wengine, dunia haiwezi kuwaacha watu hao bila ya kuwalipa kwa kile wanachofanya.
Jiangalie wewe mwenyewe, kipi kinakufanya uwe hai, kipi ambacho kipo ndani yako na kinakusukuma kutoa kwa wengine zaidi. Anza kuishi maisha yako, anza kuipa dunia thamani na hutabaki pale ulipo sasa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog