“Each problem that I solved became a rule, which served afterwards to solve other problems.” -Rene Descartes

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu wa mafanikio kwa mwaka huu 2018.

Asubuhi ya leo tutafakari KILA TATIZO UNALOTATUA NI SHERIA.
Kwenye maisha yetu, tumekuwa tunakutana na matatizo au changamoto mbalimbali.
Wapo ambao wanaweza kutatua changamoto hizi na kusonga mbele.
Pia wapo ambao wanajaribu kuzitoroka na kukimbia, wasizitatue.

Matatizo na changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha ni sehemu ya maisha yetu.
Hazitaondoka wala kukoma, na ukitatua matatizo uliyonayo sasa, yatakuja mengine makubwa zaidi.
Na usipotatua matatizo uliyonayo sasa, utaendelea kuwa nayo, hayataondoka yenyewe.

Kila tatizo au changamoto unayotatua kwenye maisha yako, inakuwa sheria ya kutatua matatizo mengine zaidi.
Unakuwa umejipandisha kiwango, kwamba tatizo au changamoto ya aina hiyo haiwezi kukusumbua tena, maana unajua jinsi ya kuitatua.
Kila tatizo au changamoto unayokutana nayo ni kubwa kabla hujaitatua, lakini ukishatatua, inakuwa ya kawaida na haiwezi kukusumbua tena.

Kazana kutatua matatizo na changamoto unazokutana nazo kwenye maisha, hata kama zinaonekana ni kubwa kiasi gani.
Kwa sababu kwa kutatua changamoto, unakuwa umeifanya isiwe tena changamoto kwako, wakati mwingine ikitokea unakuwa tayari una uzoefu wa nini cha kufanya.

Ukawe na siku bora leo, siku ya kutengeneza sheria za kutatua matatizo na changamoto.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha