Huwa tunawalalamikia wale wanaotuzunguka, tukiona kama wao ndiyo kikwazo cha sisi kushindwa kufanikiwa kwenye yale tunayotaka. Labda ni watu wanaopaswa kutupa vitu fulani na hawatupi, au ni watu ambao wanatutegemea zaidi kuliko uwezo wetu.

Wakati mwingine tunaona mazingira tuliyopo ni kikwazo cha sisi kupiga hatua, pale mazingira yanaoonekana kukosa yale ambayo tungetaka yawepo, au mazingira yanapoonekana magumu kuliko kwa wengine.

wp-image--1427239600

Yote haya yanaweza kuonekana kama sababu nzuri, lakini ukweli ni kwamba hivyo siyo vikwazo vikubwa.

Kikwazo kikubwa kabisa cha wengi kupiga hatua na kufanikiwa kinaanzia ndani yao wenyewe. Kikwazo kikubwa kabisa ni pale mtu anapojiona ameshafika hatua ya juu kabisa. Pale mtu anapoona hakuna tena hatua ya juu ya kwenda, kwamba amefikia kilele.

SOMA; UKURASA WA 748; Kuridhika Na Pale Ulipo Sasa…

Cha kushangaza, wapo wengi ambao wanajiwekea kilele kwenye hatua ndogo kabisa za maisha yao, wanakuwa hata hawajafika mbali lakini wanaona inatosha.

Chukua mfano wa mtu ambaye maisha ni magumu na hana kazi, anapata kazi ambayo inamlipa mshahara kidogo, ambao haumtoshelezi kwa namna angependa, lakini hana jinsi inabidi aikubali. Baada ya muda unamkuta ameshazoea kazi ile na kuona hana tena namna nyingine zaidi ya kazi hiyo. Anakuwa ameyajenga maisha yake kuzunguka kazi hiyo na hapo ndipo unakuwa mwisho wa ukuaji wake.

Popote ulipo sasa, jua zipo hatua nyingi zaidi za kupiga kuelekea mafanikio makubwa. Jua kwamba mafanikio siyo mwisho wa safari, bali safari yenyewe. Unafanikiwa pale unapopiga hatua, na siyo unapoona umeshafanikiwa.

Usiwe kikwazo chako mwenyewe cha kufanikiwa, kazana kuwa bora zaidi kila siku, kazana kupiga hatua zaidi kila siku.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog