The heart is great which shows moderation in the midst of prosperity. – Lucius Annaeus Seneca

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA na mwongozo wetu ni TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KIASI KWENYE WINGI….
Upo usemi kwamba ukitaka kujua tabia halisi ya mtu, mpe fedha nyingi au madaraka makubwa. Hapo ndipo utamjua mtu ni wa aina gani hasa.

Ni rahisi kuwa mnafiki na kuficha makucha pale ambapo unakuwa huna nguvu na uwezo wa kufanya chochote ambacho unafikiria kufanya.
Mtu akiwa hana kitu, ni rahisi kuona ni mtu mzuri, ni mtu mwenye kujali.
Lakini pale mtu anapopata nguvu na uwezo wa kufanya chochote anachotaka kufanya, ndipo ukweli wa mtu unakuwa hadharani. Hapo sasa ndiyo utaijua rangi halisi ya mtu.

Mkuu ni yule anayeweza kuonesha kiasi kwenye wingi, mwenye kuweza kuendelea na maisha yake ya kawaida hata kama ana uwezo wa kufanya chochote anachotaka kufanya.
Hili siyo rahisi, hasa kwa dunia ya sasa, dunia ya maonesho na likes za kitandao ya kijamii.

Kazana kuwa na kiasi hata kama una nguvu na uwezo kiasi gani wa kufanya chochote unachotaka kufanya.
Usinunue kila kitu kwa sababu tu una fedha ya kufanya hivyo.
Usile kila kitu kwa sababu una uwezo wa kununua chochote unachotaka.
Usiwashurutishe watu kwa sababu una mamlaka ya kuwasimamia.
Kila kitu fanya kwa kiasi, kwa kadiri inavyotosha, hata kama una uwezo mkubwa kiasi gani, hii itayanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Ukawe na siku bora ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha