Mafanikio yako kwenye maisha yanaendana na kiwango chako cha kuchukua hatua, kwenye kila eneo la maisha yako.

Na inapokuja kuhusu kuchukua hatua, kuna viwango vitatu;

Cha kwanza ni kutokuchukua hatua kabisa, yaani mtu yupo yupo tu, hafanyi chochote mpaka pale inapombidi kweli afanye. Kama ni kazi basi ana kila sababu ya kutokufanya kazi hiyo, ataahirisha kila kitu mpaka pale ambapo haifai tena kuahirisha. Watu wa aina hii huwa hawafiki popote kimafanikio, wanaishia kushindwa kabisa.

Kila Mtu

Cha pili ni kuchukua hatua za kawaida, hapa mtu anafanya kile ambacho kila mtu anafanya. Anachukua hatua sawasawa na wengine na hivyo kupata matokeo ambayo ni sawa na wengine wanafanya. Kama ni kazi basi atafanya kama wengine wanavyofanya, siyo pungufu na siyo zaidi. Watu wa aina hii huishia kuwa na maisha ya kawaida, hawafanikiwi na wala hawashindwi, wapo tu wakisukuma siku.

SOMA; UKURASA WA 1043; Kufanya Kazi Kwa Nguvu, Akili, Kujitoa Na Kuamini Unachofanya.

Cha tatu ni kuchukua hatua kubwa kabisa, hapa mtu anafanya zaidi ya ilivyozoeleka, anafanya kwa viwango vikubwa sana. Kama ni kazi basi anafanya zaidi ya wengine wote, kama watu wanafanya kazi masaa 8 mpaka 10 kwa siku, yeye anafanya masaa 16 mpaka 18 kwa siku. Anachukua hatua ambazo wengine hawathubutu hata kuzifikiria. Hawa ndiyo watu ambao wanafanikiwa sana, ndiyo ambao kila mtu akiwaangalia anasema nataka kuwa kama yeye.

Je ni kiwango kipi cha hatua ambacho wewe unachukua? Je ni mtu wa kuahirisha na kukwepa kufanya au mtu wa kufanya kawaida au unafanya zaidi ya kawaida?

Kama kwenye akili yako kuna kitu kama mafanikio kimewahi kukatiza, hata tu kwa kufikiri, basi unapaswa kuchukua hatua zisizo za kawaida.

Na wala huhitaji mtaala wa kukuonesha kisicho cha kawaida ni nini. Wewe angalia tu wengine wanafanya nini, kisha wewe fanya mara mbili yao. Ndiyo fanya mara mbili, utapewa maneno mengi lakini wewe usiyasikilize, fanya, fanya zaidi ya kawaida.

Huwezi kufanikiwa kwa kufanya kawaida, hivyo yeyote atakayekusema kwamba unafanya sana, kwa hakika hajafanikiwa na siyo mtu sahihi kwako kumsikiliza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog