Rafiki,

Kazi yangu kubwa ni moja, kuhakikisha wewe unapata maarifa sahihi yatakayokuwezesha ufanye maamuzi sahihi na maisha yako yawe bora kabisa. Hii siyo kazi rahisi hasa kwa zama hizi za taarifa, ambapo kuna kelele nyingi mno na zote zinakusubiri wewe.

Wakati unasoma hapa huenda unafikiria kuangalia wasap na kusoma jumbe mbalimbali, unafikiria kuingia instagram ujue nini kinaendelea, na huenda unafikiria kile ulichoandika facebook au picha uliyoweka, kuna ‘likes’ ngapi?

Kwenye zama hizi za changamoto, kama mtu hutatuliza akili yako chini, na kuchagua vitu vichache ambavyo utaruhusu viingie kwenye akili yako, utashangaa siku zinaisha na huoni kipi umefanya. Kelele zinachosha, zinatafuna muda halafu hazina manufaa yoyote.

Kila mwanzo wa mwezi nimekuwa nakushirikisha kitabu cha kusoma kwa mwezi husika, na kwa kuwa najua utasema huna muda wa kusoma, japo una muda wa mengine, nimekuwa pia nakupa njia bora ya kusoma.

Kwa njia ninayokupa, kama utaitumia, basi ndani ya mwezi lazima umalize angalau kitabu kimoja. Nitakukumbusha tena njia hiyo muda siyo mrefu. Lakini kwanza nikushirikishe kitabu cha mwezi April 2018.

Mwezi huu wa April 2018 tunakwenda kusoma kitabu cha ushindi, mimi nataka wewe rafiki yangu ushinde, ufanikiwe, kwa sababu kwa kushinda wewe, basi kila mtu anayekuzunguka anakuwa ameshinda.

Lakini ushindi hauji kama ajali, na wala hauji kama bahati, zile unazopigiwa kelele kila siku kwamba ushiriki michezo ya bahati nasibu au kamari ili ushinde. Ushindi ni kitu ambacho kinapangwa na kufanyiwa kazi, ipo misingi ya ushindi, ambayo ukiifuata, lazima na wewe utashinda. Elewa hapo, LAZIMA utashinda, siyo kama ukiwa na bahati, bali ni uhakika.

winners do

Nicki Joy mwandishi wa kitabu WHAT WINNERS DO TO WIN anatupa misingi ya ushindi, hatua ambazo washindi wamekuwa wanachukua ili kushinda, ambazo hata sisi tukizichukua tutashinda pia.

Msingi wa kwanza kabisa ambao Nicki anatushirikisha ni kwamba washindi wana hali ya ukomavu. Unaweza kufikiria wewe kama mtu mzima unakosaje ukomavu?

Nicki anatupa mambo 9 ambayo yanapima ukomavu wa mtu, ambayo kama mtu huna hayo, basi jua huwezi kushinda. Moja katika mambo 9 yanayopima ukomavu ni uwezo wa kuwa na fedha mfukoni halafu usiitumie, hata kama unatamani au unasukumwa kiasi gani kuitumia.

Nicki pia anatuambia unahitaji dakika 7 tu kwa siku kubadili kabisa maisha yako. Kwa sababu kama ambavyo nimekuwa nakuambia mara kwa mara, mabadiliko ya kweli yanaanzia kwenye fikra zetu. Kitabu hichi kimepangwa kwenye sura fupi fupi ambazo unaweza kusoma sura moja kwa dakika 7 tu, na ukaondoka na vitu vya kufanyia kazi.

Sasa rafiki yangu, kama huna dakika saba kwa siku za kujifunza na kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi, sina cha kukuambia zaidi ya kukupa pole na kukutakia kila la kheri kwa maisha magumu uliyoamua kung’ang’ania.

Kwa wale ambao wanaweza kutenga dakika saba, au hata nusu saa (ndiyo unastahili angalau nusu saa ya kujifunza kila siku) basi karibuni kwenye kujisomea kitabu cha mwezi huu.

NJIA BORA YA KUSOMA KITABU CHA MWEZI.

Nilikuahidi kukupa njia bora ya kusoma na kumaliza kitabu kila mwezi. Njia hiyo ni kwa kusoma KURASA 10 ZA KITABU KILA SIKU. Kurasa kumi tu kila siku, zinakuwezesha kumaliza kitabu kimoja kila mwezi.

Na huhitaji kujikumbusha wewe mwenyewe kusoma kurasa hizi kumi, bali ipo programu maalumu ya kusoma kurasa hizi kumi. Program hiyo ni kundi maalumu la wasap ambapo unakutana na wasomaji wengine, unasoma na kuwashirikisha wengine na wao pia wanashirikisha hivyo unajifunza kupitia usomaji wa wengine.

Kuipata program hii unapaswa kulipa ada ya shilingi elfu 10 tu, ni ada ya mara moja na hapo kinachobaki ni wewe kusoma vitabu na kujifunza kupitia usomaji wa wengine.

Kujiunga na program hii, tuma ujumbe wenye maneno KURASA KUMI kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 na utatumiwa maelekezo.

Usikubali siku yako iishe hujajifunza kwa kusoma kitabu, na elewa namaanisha kusoma kitabu. Hata kama umesoma makala nzuri, umeangalia video nzuri, tenga muda wa kusoma kitabu kila siku na akili yako itakomaa kwa ajili ya mafanikio.

Kitabu cha mwezi huu cha WHAT WINNER S DO TO WIN kinapatikana kwenye kundi la KURASA KUMI ZA KITABU hivyo kama hujajiunga jiunge upate kitabu hichi na vingine vingi kwa ajili ya kujisomea na kuongeza maarifa.

Usomaji

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog