Katika safari ya mafanikio, sehemu kubwa ya hatua utakazochukua ni zile ambazo huna uhakika nazo kwa asilimia mia moja. Unajua kabisa kuna kitu unapaswa kufanya, lakini huna uhakika matokeo yatakuwaje.

Hapo ndipo wale wanaoishia kuwa kawaida wanakwama, wakati wale wanaofanikiwa wanafanya licha ya kutokuwa na uhakika.

Kinachowasukuma ni kauli kwamba hebu tuone nini kitatokea. Unaamua kufanya kitu hata kama huna uhakika na matokeo, lakini unakuwa tayari kujifunza kupitia matokeo yoyote utakayoyapata.

Haki Yako

Hii ni dhana nzuri sana ya kutumia kwenye safari yako ya mafanikio, pale unapokuwa huna uhakika na kitu, badala ya kuahirisha ukisubiri uhakika ambao huwezi kuupata, fanya kama njia ya kujifunza. Fanya ukitaka kuona nini kitakachotokea na hapo utajifunza.

Watu hufikiria kwamba ukishafanikiwa basi unaondoka kwenye hali hiyo ya kutokuwa na uhakika, ni kama ghafla unapata nguvu za ajabu za kuwa na uhakika wa kila kitu. Hilo siyo sahihi.

SOMA; UKURASA WA 1089; Tamaa Ikishawaka, Jua Unapoteza…

Na ndiyo maana wale wanaofanikiwa, wengine huishia kuanguka, kwa sababu wanapofikia njia panda ya kufanya ambacho hawana uhakika nacho, wanaogopa kufanya kwa sababu wanaona mafanikio ambayo wameshapata watayapoteza. Hili linawafanya wafanye kwa mazoea na hivyo kutokupiga hatua na hilo kupelekea kushindwa.

Kadiri unavyofanikiwa, ndivyo hatari ya kuchukua hatua inavyozidi kuwa kubwa. Hata kwenye uhalisia tu, kadiri unakwenda ngazi kwenda juu, ndivyo hatari ya kuanguka inakuwa kubwa. Lakini katika yote, usipoteze ile dhana ya tuone nini kitakachotokea.

Na kadiri unavyofanikiwa, fanya hili kuwa zoezi maalumu, mara kwa mara, jaribu mambo mapya, jaribu mambo ambayo ni hatari, lakini kwa lengo la kujifunza ili ujue hatua sahihi za kuchukua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog