Habari rafiki?

Nianze kwa kukukumbusha kile ambacho nimekuwa nakuambia mara kwa mara, ya kwamba changamoto ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Na dunia haikosi changamoto za kutupatia mpaka ile siku ambayo tunaondoka hapa duniani.

Hivyo kama bado unapumua, jua kitu kimoja, changamoto zipo na zitaendelea kukuandama. Hivyo kukimbia changamoto yoyote unayokutana nayo ni kujidanganya, kwa sababu hazitakuacha.

Wakati mwingine ni vigumu kutatua changamoto mwenyewe, kama ilivyo kwa mchezaji ndani ya uwanja kushindwa kuona hatua sahihi za kuchukua wakati mtu anayeangalia kwa nje anaona wazi kwamba pale angepaswa kufanya hivi.

Katika makala hizi za ushauri wa changamoto, nimekuwa nakushirikisha hatua za kuchukua katika changamoto unazopitia, kwa kuangalia kwa nje na kuona kipi kinafaa kufanya.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kuangalia changamoto mbili zinazomsumbua msomaji mwenzetu. Moja ni jinsi ya kusimamia miradi wakati umeajiriwa na nyingine jinsi ya kumshawishi mwenza wako kuelewa ndoto na maono yako ya mafanikio.

Kabla hatujaangalia ni hatua zipi za kuchukua, tusome kile alichotuandikia msomaji mwenzetu;

Kukosa usimamizi wa kuendesha mradi, mie ni mtumishi nafanyaje? Pili kuna pingamizi katika ngazi ya familia, juu ya wazo langu kuwekeza muda mrefu katika kilimo cha miti, lakini upande wa pili hautaki, nafanyaje? Ni mwaka wa sita sasa hakuna kinachoendelea, nifanyeje? Niachane na familia ili kusimamia ndoto yangu au la! naomba msaada. Nilishindwa kuacha kazi kwenye international organization kwaajili ya mwenzi wangu kukataa, na sasa hili lanipa shida sana. tafadhali msaada wako ni muhimu. – K. W. Matiko.

  1. Jinsi ya kusimamia miradi ukiwa umeajiriwa.

Kila mtu anaijua changamoto ha hatari kubwa ya kuajiriwa ni ukomo wa kipato. Kwamba utafanya kazi sana lakini maamuzi ya kiasi gani cha fedha upate yapo kwa mtu mwingine. Hivyo mara nyingi utalipwa kiasi ambacho hakikutoshi na hakiendani na juhudi unazoweka. Na wote tunajua fedha ni muhimu, hata kama kazi yako unaipenda kiasi gani, kama huna fedha za kutosha kuendesha maisha yako, kila siku utakuwa na msongo.

Hivyo kila mtu ambaye ameajiriwa, anapaswa kuwa na njia mbadala za kumwingizia kipato, kama ambavyo tumekuwa tunasema, kuwa na mifereji mingi ya kipato.

Kamwe usiishi kwa kutegemea mshahara pekee, usijiridhishe na mshahara na wakati mwingine kupunguza maisha yako yaendane na mshahara. Ongeza vyanzo vya kipato, hili litakusaidia kununua uhuru wa maisha yako.

Swala linakuja kwamba umeajiriwa, unabanwa sana, huna muda wa kusimamia miradi utakayoanza.

Na hapo ndipo huwa ninakataa kabisa, kwa sababu muda ambao mtu unao, ni muda mwingi kama utautumia vizuri. Tatizo la wengi tumekuwa tunaangalia muda kwa siku na kuona hakuna nafasi ya kufanya mengine.

Nakuasa uanze kuangalia muda kwa wiki, na usiangalie siku, bali angalia masaa. Kwa mfano wiki ina masaa 168, kwa ufanyaji kazi wa kawaida, kwa wiki utafanya kazi masaa 40 labda mpaka 60 kama unafanya kazi sana. Sasa hapo unabaki na masaa zaidi ya 100 ambayo huwa unayapoteza tu kwa mambo yasiyo ya msingi.

Na hata tukiondoa masaa 50 ya kulala kwa wiki, bado unabaki na masaa mengine 50 ambayo umekuwa unayapoteza kwenye mitandao ya kijamii, kufuatilia maisha ya wengine, kuangalia tv, kusoma magazeti, vitu ambavyo havina faida yoyote kwako.

Hivyo hatua ya kwanza, weka muda wako sawa, hakikisha muda wowote ambao haupo kazini, basi upo kwenye miradi yako. Kila siku yako moja igawe upate siku mbili. Kama unaingia kazini saa mbili asubuhi na kutoka saa kumi jioni, saa kumi na moja jioni mpaka saa nne usiku kuwa kwenye miradi yako, fuatilia na simamia nini kinaendelea.

SOMA; KITABU; PATA MASAA MAWILI YA ZIADA KILA SIKU.

Hatua ya pili, miradi yako ifanye kuwa karibu na unapoishi na/au kufanya kazi. Hii itakusaidia kuisimamia vizuri kwa muda mfupi unaopata kila siku. Miradi ikiwa mbali, ambapo kufika lazima ufunge safari, itakuwa changamoto kwako.

Tatu, tengeneza watu watakaosimamia miradi yako vizuri. Waweke watu ambao unawaelekeza kila wanachopaswa kufanya na kila siku fika au wasiliana nao na wakupe taarifa sahihi ya nini kinachoendelea kila siku. Usikubali siku ipite hujajua nini kinaendelea kwenye mradi wako, hata kama ni kwa njia ya simu na kuoneshwa maendeleo kwa mitandao mbalimbali tunayo. Pia kila unapokwenda kutembelea, fuatilia kuhakikisha kila taarifa unayopata ni sahihi. Ukiendea miradi yako kwa njia hii, hata wale unaowaweka wanakuwa makini kwa sababu wanajua na wewe upo makini pia.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

  1. Jinsi ya kumshawishi mwenza wako aelewe na kukubaliana na ndoto yako kubwa ya mafanikio.

Moja ya vikwazo ambavyo wanandoa wengi wamekuwa wanakutana navyo ni ndoto au maono ambayo mmoja anayo, kutokueleweka na mwingine, na hivyo hakubaliani nayo. Hili linakuwa tatizo kwa sababu kufanya kitu ambacho hamjakubaliana, inaleta msuguano ambao unaweza usiache ndoa salama.

Kitu kikubwa kinachokosekana katika hali kama hizi ni uelewa sahihi wa kipi ambacho mtu anafanya na kipi kinategemewa kupatikana.

Kwa mfano, hakuna mwanamke mwenye akili zake timamu, anayeweza kukubaliana na mume wake pale anapomwambia naacha kazi na kuingia kwenye biashara. Hii ni kwa sababu familia inakuwa imeshazoea kwamba baba anafanya kazi fulani na kipato ni uhakika. Hata kama ni kidogo, lakini kila mwezi kipo. Biashara hata kama italeta kipato kikubwa, haitabiriki na hivyo kuwa hali ya hatari kwa maisha ya familia.

SOMA; USHAURI; Hatua Za Kuchukua Pale Unapogundua Umeoa Au Kuolewa Na Mtu Ambaye Tabia Zake Na Zako Haziendani.

Hivyo kama umekutana na hali hiyo ya mwenza kuwa kipingamizi kwenye ndoto unazotaka kufanyia kazi, fanya mambo haya mawili.

Moja, mweleze kwa kina na aelewe vizuri ni nini hasa unakwenda kufanya. Mweleze kwa nini hatua unazokwenda kuchukua ni muhimu. Mshirikishe picha ya namna maisha yatakavyobadilika kwa kufanikiwa kwenye kile unachokwenda kufanyia kazi, ambacho unahitaji sana ushirikiano wake. Pia mweleze hatari unazoweza kukutana nazo na jinsi gani umepanga kukabiliana nazo.

Jambo la pili ambalo ni muhimu kabisa, mpe mwenza wako uhakika wa maisha. Kitu ambacho familia yako inafurahia wewe ukiwa kwenye ajira ni uhakika wa kipato kila mwezi, sasa wape hali hiyo. Hakikisha una mishahara ya miezi sita kama akiba kwa ajili ya kuyafanya maisha yaweze kwenda katika kipindi ambacho hutakuwa kwenye kazi. Au pia unaweza kupiga zile gharama za msingi za maisha ya familia kisha kuwa na kiasi hicho kwa miezi sita inayokuja na kikawa kwenye akaunti maalumu ya benki. Hili litakuwezesha wewe kutuliza akili kwenye kile unachofanya na familia kuwa na uhakika kwamba maisha yataenda.

Kama utachukua muda wa kuliuza wazo lako vizuri kwa mwenza wako, ukamsikiliza hatari anazoziona yeye ni zipi na kumweleza namna ya kukabiliana nazo, na ukawa na akiba angalau ya kuweza kusukuma maisha miezi sita inayokuja hata kama hutakuwa  na kipato kabisa, mwenza wako atakuelewa.

Na kama kwa juhudi zote hizo hatakuelewa, basi jua huyo ni mtu ambaye yeye binafsi hana hamasa ya kufanikiwa na hatakuacha wewe ufanikiwe pia. Katika hali kama hiyo, unahitaji kuona ni njia zipi mbadala unaweza kutumia kuhakikisha zile ndoto kubwa za maisha ulizonazo unaweza kuzifikia.

Kufanyia kazi ndoto kubwa ya maisha yako haijawahi kuwa kitu rahisi, upinzani huanzia ndani yako na nje yako pia. Kuwa tayari kuvuka kila aina ya pingamizi unalokutana nalo kuanzia ndani yako na kwa wale wanaokuzunguka pia.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog