Kusema ni rahisi, kufanya ni kugumu, ndiyo maana kuna wasemaji wengi, washauri wengi na wakosoaji wengi kuliko wafanyaji.

Kuahidi ni rahisi, kutekeleza ni kugumu, ndiyo maana ahadi ambazo hazijatekelezwa ni nyingi sana.

Kila Mtu

Wapo watu ambao wanaanzisha biashara au huduma, wanaahidi makubwa, wanavutia wengi mwanzoni, lakini wanashindwa kutekeleza yale waliyoahidi, kinachotokea ni wateja kuwakimbia.

UKURASA WA 1067; Tatizo Siyo Wazo Bora, Tatizo Ni Kufanya Mambo Yatokee…

Unachohitaji kwenye zama hizi, zama ambazo kila mtu ana kipaza sauti cha kusema, kila mtu anaweza kusema chochote anachojisikia kusema, kwa wakati wowote anaojisikia, siyo na wewe kusema, bali kufanya.

Ukiwa mfanyaji, hata kwa hatua ndogo sana, unajitofautisha na wasemaji wote. Hatua ndogo unayochukua, inazidi maneno mengi ambayo yamezungumzwa.

Hivyo chagua kipi unachofanya, thamani gani unataka kuongeza kwenye maisha ya wengine, kisha weka juhudi katika kufanya.

Usiwe mtu wa kwenda kwenye mitandao ya kijamii na kusema nitafanya hivi au nitafanya vile, bali fanya. Muda unaotumia kuahidi na kusema yapi unafanya, ukiutumia kufanya, utapiga hatua zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog