Rafiki, huwa kuna matatizo ya aina mbili ya fedha;

Aina ya kwanza ni matatizo ya kutokuwa na fedha, hapa unashindwa kupata vile vitu unavyotaka na unahangaika sana kupata fedha, huku ukiwa na mipango mizuri ya matumizi yake utakapoipata.

Aina ya pili ni matatizo ya kuwa na fedha, hapa unakuwa na fedha lakini zinakuja na matatizo yake, unajikuta una matumizi makubwa kuliko ulivyotarajia, unashangaa changamoto ambazo hazikuwepo awali zinajitokeza na hela inapata matumizi ambayo hayakuwepo awali. Kinachotokea fedha zinaisha na unajiona hakuna ulichokamilisha kufanya katika vile ulivyopangilia.

Leo kwenye makala yetu ya ushauri wa changamoto, tutaangalia aina ya pili ya changamoto za fedha, changamoto unazokutana nazo unapokuwa na fedha.

Wapo watu wengi ambao wakipata fedha wanajikuta kama akili zao zinahama. Kabla ya kuwa na fedha wanakuwa na mipango mizuri sana, lakini wanapozipata fedha mipango mizuri yote inayeyuka, na wanajikuta wana mambo mengi yanayohitaji fedha hizo. Mwisho wa siku, fedha inaisha na mipango yao hawajaitekeleza.

Kwenye makala ya leo, nakwenda kukushauri jinsi ya kuituliza fedha unayopata ili uweze kutimiza malengo uliyojiwekea kwenye maisha yako.

Hapa kuna maoni ya wasomaji mbalimbali waliotuandikia kuhusiana na changamoto hii, ni watu tofauti tofauti lakini msingi wa tatizo ni moja; WAKIPATA FEDHA HAITULII.

Changamoto nikipata fedha nakosa awazo nifanye nini nikishatumia ikiisha ndio napata mawazo. – Eunice F.K.

Mimi ni mfanyabiashara kila nikipata pesa malengo yangu huhalibika najikuta nafanya jambo ambalo sikulipanga naomba ushauri wenu NAWATAKIA KAZI NJEMA. – Said J. L.

Nilichukua mkopo 30m. Ndani ya miezi 4 iliyopita hakuna nilichofanya na ninadaiwa mtaani 15m. Hela za riba mpaka Sasa nahangaika tu. Naomba ushauri. – Melk M.

Changamoto ya kutunza fedha. – Vincent P. Z.

Mimi kuna kitu kinanisumbua katika maisha yangu nikipata hela akili inanituma kwenye starehe na pombe naomba ushauri ? – Mamno J. M.

88c15-4326597376_a74a527ef3_z

Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia ili kuweza kuituliza kile fedha unayopata na iweze kufanya makubwa kwako.

ACHA UTOTO KWENYE FEDHA.

Upo usemi wa Kiswahili unaosema mtoto halali na hela. Umewahi kuuelewa vizuri? Kama bado, basi hiyo ndiyo inasababisha changamoto zako kifedha.

Mtoto halali na hela kwa sababu mtoto akipata hela hana siri, atamwambia kila mtu, atamringishia kila mtu, na wakati wote, atashika hela yake kwenye mkono wake. Sasa ukitaka kuipata fedha ya mtoto huyo, subiri alale, utaichukua kirahisi tu, na akiamka wala hatakuwa na kumbukumbu fedha hiyo imeenda wapi.

Hivi ndivyo watu wazima wengi wenye changamoto za fedha wanavyoishi. Wakipata fedha, iwe wamepokea mshahara, au wamepata faida, basi kila mtu atajua huyu ana fedha. Wataanza kutoa zawadi zisizo za msingi, wataanza kutoa ofa za vinywaji kwa watu, mtu atakutana na muuza nguo, hakuwa na mpango wa kununua nguo ila kwa kuwa amemuona na fedha anayo, basi ananunua.

Sasa jamii inapojua mtu ana fedha, na anazitoa kirahisi, kila mtu anatafuta mbinu ya kupata fedha hizo. Hapo sasa ndiyo utaona kila mtu anakuja na shida yake, shida ambayo kwa namna inaelezewa, utaona ni kubwa sana na wanahitaji msaada wako wa fedha, na kwa kuwa kila mtu anajua una fedha, basi huna budi bali kuchangia.

Hata matapeli wa fedha pia, wanafuata wale ambao wanaonekana wazi kwamba wana fedha, na wanakwenda na mitego ambayo ni vigumu kwa mtu kuing’amua.

Hivyo rafiki, hatua ya kwanza ya kutuliza fedha zako, acha utoto kwenye fedha, acha kuionesha dunia kwamba umepata fedha. Yaani kama kwa matendo yako tu mtu wa nje anaweza kujua una fedha au huna, wewe bado una tabia za kitoto kwenye fedha.

Jijengee ukomavu kwenye fedha, ukomavu ambao ukiwa na fedha au ukiwa huna hakuna mabadiliko kwenye tabia. Hiyo itakuwezesha kutulia na fedha ambazo unazipata na kujiepusha na wanyonyaji wa fedha wanaokuzunguka.

SOMA; Kila Kitu Unachopaswa Kujua Kuhusu Cryptocurrency Na Bitcoin (Fedha Za Kidijitali) Na Kwa Nini Siyo Uwekezaji Mzuri Kwako Kwa Sasa.

PANGILIA FEDHA KABLA HUJAIPATA.

Usikubali hata mara moja ukutane na fedha kwa mshangao, yaani upate fedha halafu ndiyo ukae chini na kupanga unafanya nini na fedha hiyo, chochote utakachopanga ukiwa na fedha, kitaishia kuwa hovyo.

Kuwa na mipango ya kila kiasi cha fedha unachoweza kupata na utakifanyia nini.

Kwa mfano weka madaraja mbalimbali na vitu utakavyofanya. Kwamba labda ukipata milioni moja, utafanya hivi, ukipata milioni 5 utafanya kile, ukipata kumi, kingine na kuendelea.

Sasa unapopata fedha, kataa mawazo yoyote mapya yanayokujia ukiwa na fedha, hayo siyo mawazo sahihi. Rudi kwenye ile mipango uliyoweka kabla hujawa na fedha na tekeleza hiyo. Kwa sehemu kubwa utapata mafanikio kuliko kujaribu mambo mapya unapokuwa na fedha.

USINUNUE KITU AMBACHO HUJAPANGA KUNUNUA.

Kamwe, kamwe, kamwe, usinunue kitu ambacho hukupanga kununua, hata kama utakuta kinauzwa kwa bei sawa na bure. Tena epuka sana kununua vitu vya bei rahisi pale unapokuwa na fedha.

Ukipata fedha, usikimbilie kununua vitu ambavyo ulikuwa hununui wakati hukuwa na fedha. Badala yake nunua vile ulivyokuwa unanunua hata wakati hukuwa na fedha, na kile kiasi cha ziada cha fedha kiende kwenye mipango yako mingine.

Iwapo umekutana na kitu kizuri ukatamani kununua, usikinunue mara moja, bali jipe muda usiopungua masaa 24 wa kufikiria kama kweli kitu hicho ni muhimu. Kama kweli maisha yatashindikana kwenda kwa sababu huna kitu hicho basi nunua, kama maisha yataendelea bila ya shida, achana nacho.

USIKOPE KAMA HUNA NJIA YA KUINGIZA FAIDA.

Usikope fedha kwa ajili ya matumizi, kufa njaa lakini usikope, nielewe vizuri kwenye hilo. Kamwe usikope kwa ajili ya chakula, au mavazi, kama huwezi kutesa mwili wako kwa kazi yoyote ile mpaka ukapata fedha ya kula, wewe na familia yako, basi maisha yako bado yana matatizo makubwa.

Inapotokea unataka kukopa, basi uwe na kitu ambacho tayari kinaingiza faida, na hivyo mkopo unaochukua unaenda kuongeza faida zaidi. Na unapokopa, fedha yote iende kwenye mradi unaoingiza fedha, na siyo kutumia kwa kitu kingine chochote.

Usikope ili kwenda kuanza biashara, usikope. Nisisitize tena, usikope kwenda kuanza biashara, utajiumiza sana na mikopo ya aina hiyo.

SOMA; Tofauti Ya Fedha Kwenye Uwekezaji, Matumizi Na Kukopa.

TENGENEZA GEREZA LA FEDHA ZAKO.

Tabia ya fedha ni moja, huwa haikosi matumizi. Hivyo fedha yoyote ambayo ipo wazi, haikosi matumizi. Utajikuta inapata sababu ya kutumika.

Hivyo ili kuepukana na ushawishi huo wa kutumia fedha, tengeneza gereza la fedha zako. Kuwa na mfumo ambao unakuruhusu kuweka fedha lakini siyo kutoa. Kuna aina za uwekezaji na pia akaunti za benki zinakuwezesha kuweka fedha lakini zinakuwekea ukomo kwenye kutoa.

Cha kufanya, tenga asilimia fulani ya kipato chako ambayo utakuwa unaiweka kwenye gereza la fedha, kisha fungua akaunti yenye ukomo wa kutoa na weka fedha zako kwenye akaunti hiyo. Hii itakuwezesha kukuza akiba yako bila ya kuitumia na baadaye ukaweza kufanya makubwa.

BADILI KANUNI NA MTAZAMO WAKO KUHUSU FEDHA.

Unatumia fedha kila unapozipata kwa sababu ndani ya akili yako umeweka kanuni hii; FEDHA = MATUMIZI. Hivyo kila unapopata fedha unaanza kuangalia nini unaweza kununua, na kwa kuwa fedha huwa haikosi matumizi, unajikuta unanunua vitu vingi ambavyo hata havina maana.

Unahitaji kubadili kanuni yako ya fedha na mtazamo ulionao kuhusu fedha. Tengeneza kanuni ya FEDHA = UWEKEZAJI, hivyo kila fedha unayoipata, jiulize unaweza kuiwekeza vipi ili izalishe zaidi.

KWA NINI SIYO TAJIRI

ELIMU YA MSINGI YA FEDHA.

Kitu ambacho tumenyimwa kwenye maisha yetu, ni elimu ya msingi ya fedha. Hakuna mtu ambaye amewahi kukaa na wewe chini na kukueleza kwa msingi kabisa kuhusu fedha, inapatikanaje na inatumikaje. Huenda unaposikia uwekezaji basi unafikiria mamilioni kwa mabilioni ya fedha.

Lakini je unajua kwamba unaweza kuanza kuwa mwekezaji hata kwa shilingi elfu 5? Je unajua kwa kipato chochote kidogo ulichonacho unaweza kutengeneza utajiri mkubwa kwa kutumia muda na nguvu ya uwekezaji?

Hayo yote unaweza kuyapata kwenye ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, somo ambalo linapatikana kwenye KISIMA CHA MAARIFA pekee. Hili ni somo ambalo lina vipengele kumi, ambavyo ukivisoma na kuvifanyia kazi, hutabaki hapo ulipo sasa kifedha.

Kama bado hujapata elimu hii ya msingi ya fedha, jiunge sasa na KISIMA CHA MAARIFA, kwa ada ya shilingi elfu 50 kwa mwaka, utajifunza mengi sana kuhusu fedha, uwekezaji, biashara, falsafa na afya.

Karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA, tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717396253.

Jukumu kubwa unalopaswa kuchukua kwenye fedha, ni kuhakikisha wewe unaitawala fedha na siyo fedha kukutawala wewe. Kuwa na mipango kabla ya kuwa na fedha, na unapokuwa na fedha, kutulia na kutekeleza mipango hiyo.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog