Yapo mambo mengi sana ambayo nimekuwa najifunza kupitia huduma ninayofanya, ya kutoa maarifa na hamasa ya watu kuchukua hatua na kuyafanya maisha yao kuwa bora zaidi.
Katika watu wengi ambao wamekuwa wanaomba ushauri kwenye mambo mbalimbali, nimejifunza kwamba wengi huwa hawatafuti ushauri, badala yake wanatafuta mtu wa kukubaliana nao.
Unakuta mtu tayari ameshaamua kufanya kitu, na hata aambiwe nini hataacha kufanya, lakini kwa kuwa hataki kuona amefanya maamuzi hayo mwenyewe, basi anaomba ushauri.

Sasa kama ushauri utakuwa unaendana na kile alichopanga, anafurahi na kuendelea na mipango yake. Lakini kama ushauri utaenda kinyume na kile ambacho yeye anapanga kufanya, anaanza kukosoa ushauri, anaona ushauri siyo mzuri, au unakatisha tamaa.
Leo nataka nikukumbushe rafiki yangu, ili uokoe muda wako na wa wengine ambao unawaomba ushauri.
Kama kitu umeshaamua kwamba utakifanya kweli, hakuna kitakachokuzuia, iwe ni kitu kibaya au kuzuri, acha kupoteza muda kwenye kukusanya ushauri wa ufanye au usifanye, maana mwisho wa siku utafanya, sasa ya nini uwachoshe watu? Fanya na utajifunza kupitia yale unayofanya.
SOMA; UKURASA WA 941; Juhudi Hizo Weka Kwenye Kila Eneo La Maisha Yako…
Kama kitu huna uhakika ufanye au usifanye, na hujui ni hatua ipi uchukue, chagua mtu unayemuamini, ambaye unaona anastahili kukushauri, mwombe akushauri kisha mhoji sana kulingana na hali yako, na hakikisha unaondoka na jibu la unakwenda kufanya au hutakwenda kufanya.
Watu wengi wamekuwa wanapoteza muda kwenye kutafuta ushauri kwenye mambo ambayo hata washauriwe vipi bado watayafanya au hawatayafanya. Okoa muda wako na wa wengine, kwa kujua yapi utafanya hata uambiwe nini, yapi hutafanya hata iweje na yapi ukipata maoni ya wengine utaweza kufanya maamuzi sahihi.
Usitafute ushauri wa kukubaliana na wewe kwamba ufanye au usifanye, bali tafuta ushauri wa kukufanya ufikiri, wa kukuwezesha kuona kile ambacho ulikuwa huoni ili uweze kufanya maamuzi sahihi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
Kweli nakubaliana na ww kuhusu ushauri na kushauriwa.
LikeLike
Karibu.
LikeLike