“Care about what other people think and you will always be their prisoner.”—Lao Tzu
Hongera rafiki kwa asubuhi nyingine nzuri ya leo,
Siku mpya ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU , UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JINSI UNAVYOKUWA MTUMWA WA WENGINE…
Umekuwa unachagua kuwa mtumwa wa wengine wewe mwenyewe,
Na umekuwa unafanya hivyo pale unapoanza kujali watu wanakufikiriaje au kukuchukuliaje.
Iko hivi, huwezi kuwapangia watu wakufikirieje au wakuchukulieje, bali unachoweza ni kuishi maisha yakonya uhalisia.
Ukishaanza kutaka watu wakufikirie au kukuchukulia kwa namna fulani, hapo ndiyo unaanza kuishi maisha ya maigizo, na bado watu hawatakuchukulia kama unavyotaka wakuchukulie.
Watu hawatumii muda mwingi kukufikiria kama unavyodhani, kwa sababu wanatumia muda mwingi kifikiria maisha yao na matatizo yao.
Hivyo kukazana kuishi maisha ya maigizo ili watu wakufikirie vizuri, ni kujiweka kama mtumwa wao.
Ishi yale maisha ya uhalisia kwako,
Fanya kile ambacho unajua ni sahihi kufanya,
Na wale wanaojali watachukulia kwa njia bora,
Wasiojali hata hawatajua unafanya nini.
Usiwe mtumwa wa kutaka kuwaridhisha wengine, hakuna unayeweza kumridhisha isipokuwa wewe mwenyewe.
Uwe na siku bora leo, siku ya uhuru wa kufanya unachotaka.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha