Sisi binadamu ni majaji wazuri sana wa kuhukumu wengine kabla hata hatujapata taarifa kamili.
Ni mara ngapi umekutana na mtu kwa mara ya kwanza, akawa labda siyo mtu wa kuongea sana na ukajiambia huyu mtu anaringa.
Au umemsalimia mtu hakuitika japo wewe unaona amekusikia kabisa, na ukasema mtu huyo ana dharau? Mpaka baadaye unakuja kugundua kwamba alikuwa kwenye mawazo mengine, au ana matatizo yanayomvuruga kiasi cha kutokuwa pale alipo?
Mara ngapi umesikia tu habari ya mtu na kusema niliua tu, halafu unakuja kupata taarifa kamili na kugundua ulichokua unajiambia ulijua hata hakikuwa sahihi?

Tunahukumu sana, na asilimia 99 ya hukumu tunazotoa siyo sahihi, kwa sababu hatujui ukweli wenyewe, hatupo ndani ya yule mtu ambaye tunamhukumu, hatujavaa viatu vyake.
Hivyo kwa hukumu yoyote tunayotoa, tunakosea sana, kwa maana hiyo tunahitaji kuacha kuhukumu mara moja.
Lakini swali gumu ni unaachaje kuhukumu, kitu ambacho umeshazoea kufanya na kila mtu anafanya?
Na njia ni rahisi, ni kuacha kuhukumu. Kila wakati ambapo unapata msukumo wa kuhukumu wengine, jiambie huna taarifa au uelewa wa kutosha kuwa na hitimisho la hukumu yako.
Kila unachoona au kusikia kwa nje kuhusu mwingine, jiambie ndani kuna mengi yanaendelea, ambayo huyajui na wala huwezi kuyajua.
SOMA; UKURASA WA 461; Mara Zote…
Na mwisho kabisa, kumbuka jukumu lako la kwanza ni kujali mambo yako, unapoanza kuhukumu wengine, unaanza kujali mambo ya wengine wakati ya kwako mwenyewe hayajakaa vizuri. Hivyo weka nguvu kwenye kujali mambo yako na acha wengine wajali mambo yao.
Hii haimaanishi uache kukemea ubaya na uovu kwa sababu hutaki kuhukumu. Kama kuna kusa, ubaya au uovu umefanyika, eleza kwa wazi lile kosa au ubaya uliofanyika, elezea tukio na kwa nini siyo sahihi, usianze kuelezea sababu za mtu kufanya na mengine ambayo huyajui vizuri. Hii itakusaidia kuwa sahihi, kusimamia kile ambacho ni sahihi, ambacho ni kukemea ubaya au uovu na kuachana na hukumu za wale waliofanya au ambao hawakufanya nini katika ubaya huo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog