Kama unazama kwenye maji, uking’ang’ania kushikilia maji ukidhani ndiyo utaacha kuzama, ndiyo utazidi kuzama zaidi na zaidi. Kama unataka kuepuka kuzama, unachopaswa kufanya siyo kushikilia maji, badala yake kuachilia maji, kujiachia kwenye maji na hili litasaidia maji kukufanya uelee.
Kadhalika kama unaanguka kutoka juu ya kitu, kung’ang’ana kushika hewa hakutakusaidia usianguke, badala yake kutakufanya uanguke vibaya zaidi. Lakini kama utajiachilia kwenye hewa wakati unaanguka, angalau utaweza kutua vizuri na usiumie vibaya.

Hivi ndivyo maisha yalivyo, vitu vingi tunavyong’ang’ania kwenye maisha ndivyo vinavyotuangusha zaidi. Angalia kila mtu anayekufa, kuna kitu anang’ang’ana nacho mpaka kinamuua.
Iwe ni mtu anayesumbuliwa na msongo wa mawazo, au anayesumbuliwa na magonjwa mengine yoyote, kuna kitu ambacho watu hao wanang’ang’ania ambacho hakiwasaidii na ndiyo kinazidi kuwakandamiza zaidi.
SOMA; UKURASA WA 89; Sheria Tatu Muhimu Za Kufanikiwa Kwenye Maisha.
Kila wakati unapojikuta kwenye ugumu wowote ule kwenye maisha yako, jaribu kuangalia nini unang’ang’ania kwenye eneo hilo la maisha yako. Labda ni chuki au kinyongo ulichonacho kwa watu fulani. Au ni mazoea fulani ambayo umekuwa nayo kwenye maisha yako kwa muda mrefu ambayo kwa sasa siyo msaada tena.
Kwenye kila eneo la maisha yako, jifunze kuachilia, jifunze kuacha kung’ang’ana na mazoea na kuangalia kipi bora unaweza kufanya kwenye hali hiyo uliyojikuta.
Maendeleo na mafanikio ni matokeo ya kuwa tayari kubadilika na kujaribu vitu vipya. Japo inaweza kuwa hatari, lakini hatari ndiyo inaleta mafanikio.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog