Papa Alexander aliwahi kunukuliwa akisema kujifunza kidogo ni kitu hatari sana, ni heri mtu anywe kuliko kuonja chemchem ya hamasa.
Kauli hii ina ukweli mzito sana ndani yake.
Angalia kwenye maisha ya kawaida, watu hatari sana ni wale waliojifunza kidogo, wameonja tu elimu fulani lakini wanaamini tayari wanajua kila kitu.

Kwa kuamini kwao kwamba tayari wanajua kila kitu, wanajiamini kupitiliza na kufanya maamuzi makubwa, ambayo yapo nje ya uwezo wao. Kinachotokea ni wanapata matokeo mabovu sana kwa sababu hawakuwa wanajua kile wanachofanya kama wanavyofikiri.
Chochote unachofanya kwenye maisha, kufanya kidogo au kuonja ni hatari sana. Ni bora mtu uchague kufanya kwa undani, kujua kwa undani wa hali ya juu, na kama huwezi hivyo basi bora usiguse kabisa.
SOMA; UKURASA WA 850; Chanzo Cha Kujiona Hufai…
Usijifunze kitu juu juu kisha kujiita mtaalamu ambaye unaweza kufanya maamuzi makubwa kwenye hicho ulichojua kwa juu juu.
Hili limekuwa hatari sana kwenye zama hizi za taarifa, ambapo taarifa zinapatikana kwa wingi, lakini ni vigumu kujua usahihi wake. Kwa mfano ukiingia kwenye mtandao wa google na kutafuta chochote, utaletewa majibu mengi mno ndani ya sekunde chache. Machaguo hayo hayamaanishi ni sahihi, bali google imekukusanyia kila kilichopo mtandaoni kuhusu unachotafuta.
Majibu mengi kati ya yale unayopata siyo sahihi, na hata kama ni sahihi, yameelezewa kwa juu juu sana kiasi kwamba hayakupi uelewa wa kutosha kufanya maamuzi.
Lakini kila siku utakutana na watu ambao baada ya kusoma makala chache za biashara mtandaoni tayari wameshakuwa washauri wa biashara. Au kwa sababu wapo kwenye mitandao ya kijamii na wameona watu wanazungumzia kitu fulani, tayari nao wanaweza kuzungumzia, na kutoa maoni yao, ambayo wanataka yaheshimiwe, hata kama hayana uzito wowote.
Hakuna hatari kubwa kama kuonja chemchem ya hamasa, maana utapata hamasa mbovu halafu itakupoteza kabisa. Ni bora uzame kabisa kwenye chemchem hiyo, unywe kwa undani kabla hujajaribu kufanya maamuzi yoyote.
Jua kitu kwa undani kabla hujajipa nguvu ya kufanya maamuzi, jua kitu kwa undani kabla hujajipa nafasi ya kutoa maoni ya wengine.
Na kumbuka huhitaji kujua kila kitu, bali yale muhimu kwako, mengine waachie wengine wahangaike nayo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog