Kila mtu ana dakika kumi na tano anazopoteza kwenye siku yake, ndiyo, kila mtu na hasa wale utakaowasikia wakisema wapo bize na hawana muda kabisa.
Yawezekana ni dakika kumi na tano moja unapoteza kwenye siku yako, au dakika kumi na tano nyingi unazipoteza kwenye nyakati tofauti tofauti za siku yako.
Haijalishi ni dakika kumi na tano ngapi unapoteza, cha kwanza kukubali kwamba kuna dakika kumi na tano unazozipoteza.

Iwe ni zile dakika tano ambazo umejiambia unaingia kwenye mitandao ya kijamii, na kuja kustuka dakika 15 mpaka nusu saa imeisha na bado upo kwenye mitandao ya kijamii.
Au zile dakika tano ambazo mtu amekuambia umsubiri, kwa sababu mna kikao maalumu, lakini zinaenda mpaka dakika 20.
Au ni dakika tano ambazo unasubiria mteja aje, au kazi ianze, lakini zinakuwa dakika 20 za kusubiri.
Dakika kumi na tano ni uhakika unazo na unazipoteza kila siku, na mara nyingi dakika kumi na tano nyingi, lakini kwa kukubaliana tuchukue kwamba unapoteza dakika 15 moja tu.
SOMA; UKURASA WA 178; Lakini Nitapitwa…. (Sababu Ya Kijinga Inayokufanya Upoteze Muda)
Sasa tuangalie vitu ambavyo unaweza kuvifanya ndani ya dakika kumi na tano;
Unaweza kusoma kurasa 5 za kitabu, ambapo ukisoma kurasa hizi kila siku, ndani ya miezi miwili unamaliza kitabu kimoja.
Unaweza kufanya tahajudi kwenye dakika hizo 15, ukatuliza akili yako na kudhibiti hisia zako.
Unaweza kuwasiliana na mtu muhimu, ambaye kila siku umekuwa unasema huna muda wa kuwasiliana naye.
Unaweza kupangilia siku yako, unaweza kupitia mipango na malengo yako na kujikumbusha yapi muhimu kwako kuzingatia.
Unaweza kuandika ukurasa mmoja wa makala au kitabu, na ndani ya miezi mitatu ukawa umekamilisha kuandika kitabu unachowaza kuandika.
Unaweza usifanye chochote, ukajipa muda wa kujipumzisha, kwa dakika kumi na tano na ukaanza upya ukiwa na fikra mpya na safi.
Yapo mengi ya muhimu sana unayoweza kufanya ndani ya dakika kumi na tano, ambazo kila mmoja wetu anapoteza.
Muhimu ni hili, kubali kwamba utakuwa na dakika 15 za kupoteza kwenye siku yako, kisha panga unapopata dakika hizo utafanya nini.
Sasa uwe mjanja pia, dakika kumi na tano hazitakuja wazi wazi, zikakuambia kwamba hizi ndiyo zile dakika 15 za kupoteza, badala yake kila kitu ambacho unakadiria kitasubiri dakika tano, basi jua hizo ndiyo dakika 15 ambazo unakwenda kupoteza.
Na mara nyingi, zitakuwa zaidi ya dakika 15, hivyo utanufaika zaidi na zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog