Watu ambao hawajafanikiwa, huwa wana sababu nyingi sana kwa nini hawajafanikiwa, nyingi mno kiasi kwamba ukianza kuzisikiliza, utajikuta unawaonea huruma na kusema wamewezaje kuendelea kuwa hai mpaka sasa.

Labda walitelekezwa wakiwa watoto, hawakupewa elimu, walibakwa, wazazi walifariki wakiwa wadogo, walifeli shule, wakadhulumiwa mali, wamepata kazi ambayo wananyanyaswa, na hapo bado hujaweka malalamiko ambayo huwa yanaenda kwa serikali na mamlaka nyingine.

Kwa upande wa pili, watu waliofanikiwa wana sababu moja tu kwa nini wamefanikiwa. Siyo kwamba wao hawana hizo sababu za kushindwa kufanikiwa ambazo wengi wanazo, ila wao wanaachana nazo, na kutafuta sababu moja tu kwa nini wanapaswa kufanikiwa na wanaishi sababu hiyo, kila siku bila ya kuchoka.

Watu ambao hawajafanikiwa ni wa kwanza kusema kwamba hakuna kanuni ya mafanikio, kwamba wale waliofanikiwa, ni kwa sababu wana bahati au walipata upendeleo, au mambo tu yalitokea ambayo yaliwapa nafasi ya kufanikiwa.

vitabu softcopy

Lakini waliofanikiwa wanajua kwamba ipo kanuni ya mafanikio, wameshajifunza na wanajua kabisa kuna vitu wakifanya wanapata mafanikio, na kuna vitu wasipofanya mafanikio yanakosekana. Wameshajifunza na kujua kwa hakika kwamba kuna hatua fulani wakichukua zinawaangusha na hivyo wanaziepuka.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuituliza Fedha Unayoipata Ili Uweze Kutimiza Malengo Ya Maisha Yako.

Tatizo ni kwamba, kanuni za wengi waliofanikiwa huwa hazionekani kwa nje, na kwa kuwa watu hao huwa wapo ‘bize’ sana na mafanikio yao, hawajui hata kile wanachofanya na kuishi ni kanuni, wao wanaona ni sehemu ya maisha yao.

Kwa mfano, utakuta mtu tayari ana tabia kwamba kila fedha anayopata, ataweka kwanza kiasi fulani pembeni kabla hajafanya matumizi, na hivyo anakuwa na akiba ambayo baadaye ataitumia kuzalisha zaidi. Yeye anaona ni sehemu ya maisha yake, lakini kwa nje ni kanuni muhimu sana kwa mafanikio yake. Kwa upande wa pili, utakuta wengi wakipata fedha, wanatumia kwanza, wakiamini kama itabaki ndiyo wataweka akiba, na kwa kuwa fedha huwa hazitoshi, wanajikuta hawajabaki na kitu.

Hivyo wale ambao hawajafanikiwa, wanakataa uwepo wa kanuni ya mafanikio, kwa sababu hawajui kama ipo. Na pale anapoambiwa kitu fulani ni kanuni ya mafanikio, huwa wanakijaribu, lakini hawapati matokeo mazuri, na hivyo kuona kwamba huenda wamedanganywa au hakuna kanuni.

Leo napenda nikukumbushe hili rafiki yangu, kanuni ya mafanikio ipo, tena siyo moja bali ni nyingi. Na ni kweli kwamba kanuni za mafanikio huwa hazifanyi kazi kwa wengi.

Na hii ni kwa sababu, hakuna kanuni ya mafanikio inayofanya kazi kwa yeyote, mpaka pale mtu atakapoifanyia kazi kanuni hiyo ya mafanikio.

Kwa maneno mengine haijalishi unazijua kanuni ngapi za mafanikio, kama hutaziishi kanuni hizo kweli, hutaweza kufanikiwa.

SOMA; Mambo Muhimu Ya Kujifunza Kuhusu Nidhamu Binafsi Na Mafanikio.

Mafanikio siyo kujua, mafanikio ni kufanya, mafanikio ni kuishi. Tulidanganywa sana tulipoambiwa elimu ni nguvu, elimu siyo nguvu, bali elimu inayofanyiwa kazi ndiyo nguvu.

Unaweza kujua kila kitu kuhusu mafanikio, lakini kama hutachukua hatua, unachojua ni bure na hakina msaada wowote kwenye maisha yako.

Hivyo rafiki, kanuni ya mafanikio itafanya kazi kwako, kama na wewe utafanya kazi kwenye kanuni hiyo. Mafanikio ni nipe nikupe.

Kingine muhimu sana ni kwamba kuishi kanuni ya mafanikio kunachukua muda, siyo kwamba ukijua kanuni leo na kuanza kuiishi basi kesho unapata mafanikio. Inachukua muda mrefu, wakati mwingine miaka.

Pia haitakuwa rahisi, kwamba kwa sababu unajua kanuni basi 2 + 2 = 4, japokuwa jibu unalotaka ni 4, kanuni inaweza kwenda hivi, 1 + 1 – 6 + 2 + 3 + 4 – 2 + 3 = 4. Unaona hapo, jibu kwenye hesabu zote mbili ni 4, lakini moja imechukua njia ndefu kufika kwenye 4.

Nakukumbusha hilo leo kwenye mafanikio yako, ili usikate tamaa hata kama unapitia magumu kiasi gani. Usilalamike kwamba kanuni hazifanyi kazi kwako, bali fanyia kazi kanuni unazojua na utapata matokeo bora kabisa kwenye maisha yako.

Hakuna atakayekupa mafanikio, bali utayafanyia kazi mafanikio. Hakuna mafanikio ambayo yamewahi kuwa rahisi lakini mafanikio yanawezekana. Achana na kila sababu kwa nini huwezi kufanikiwa na chagua sababu moja tu kwa nini ufanikiwe, jikumbushe sababu hiyo kila siku na jisukume kuchukua hatua ili kuweza kufanikiwa kweli.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog