Rafiki yangu, muda unayoyoma na mwaka unakatika, ni imani yangu jinsi muda unavyokwenda kazi, ndivyo hatua unazochukua zinavyozidi kuwa kubwa na kupata matokeo bora zaidi. Hongera kwa hilo rafiki.

Juma namba 16 la mwaka 2018 linamalizika, hatutakuwa na juma hili tena. Ni muda sasa wa kushirikishana yale muhimu niliyojifunza na kukutana nayo kwenye juma zima ambalo linakwisha.

Na juma hili yapo mazuri sana ya kujifunza, ambayo nakwenda kukushirikisha, imani yangu ikiwa kwamba tutajifunza na kuchukua hatua ili maisha yetu kuwa bora zaidi.

Uongozi

#1 KITABU NILICHOSOMA; HUIJUI DUNIA KAMA UNAVYOFIKIRI UNAIJUA.

Huwa tunaamini kwa kufuata habari basi tunaijua dunia, tunajiambia tusipofuata habari basi tutaachwa nyuma, lakini hili limekuwa siyo sahihi. Kwa kadiri mtu anavyofuata habari na mambo yanavyojadiliwa sana, basi ndivyo anavyokuwa na uelewa mdogo sana kuhusu dunia.

Mambo mengi yanayopewa nafasi kwenye habari na mijadala ya watu ni yale ambayo ni hasi, yenye kusisimua na kuibua hisia za hofu. Ukifuatilia habari kwa muda mrefu, utajishawishi kwamba dunia ni mbaya na inazidi kuwa mbaya. Lakini kama utachukua hatua ya kutaka kuijua dunia vizuri, ukazisoma takwimu za dunia jinsi zilivyo, basi utaona picha tofauti ya dunia.

Aliyekuwa mwandishi na mshauri wa afya Dr Hans Rosling kwenye kitabu chake cha mwisho, FACTFULLNESS ametuonesha kwa mifano maeneo kumi ambayo tunakosea kuhusu dunia, tukifikiri tunaijua dunia kumbe hatuijui kabisa.

Maeneo hayo kumi ni kama ifuatavyo;

  1. Tunaamini dunia imegawanyika kwenye makundi mawili makuu, matajiri na masikini. Ukweli ni kwamba hakuna makundi mawili makuu, kuna ngazi na watu wengi wapo katikati, huku wachache wakiwa kwenye umasikini na wachache kwenye utajiri.
  2. Habari hasi zimekuwa zinapewa nafasi kubwa kuliko habari chanya, na tunaamini dunia inazidi kuwa mbaya. Ukweli ni kwamba habari hasi ni sehemu ndogo ya habari zote, lakini vyombo vya habari vinapenda habari hasi.
  3. Huwa tunafikiri mambo yanaenda kwa mstari nyoofu, kama watu wanaongezeka basi wataendelea kuongezeka bila ukomo. Ukweli ni kwamba kila kitu kina ukomo, na watu hawataongezeka bila ya ukomo.
  4. Hisia za hofu zimekuwa kikwazo kwa wengi kuchukua hatua, lakini hofu inapaswa kuwa kitu cha kutuongezea umakini na siyo kutuzuia.
  5. Tunapenda kuviona vitu kwa ukubwa usio sahihi, tunavifanya vitu vionekane ni vikubwa kuliko uhalisia wake. Tunapaswa kuona vitu kwa ukubwa wake kiuhalisia, kwa kuvilinganisha na vitu vingine pia.
  6. Tunapenda kujumuisha watu na vitu kwenye kundi moja, lakini watu na vitu vinatofautiana, hivyo kabla ya kujumuisha angalia utofauti na ufanano ndani ya kundi na nje ya kundi pia.
  7. Tunapenda kuona hatima zimeshaamuliwa, kwamba masikini wataendelea kuwa masikini hata wafanye nini. Ukweli ni kwamba mabadiliko yanatokea, hata kama ni madogo, lakini yanatokea.
  8. Tunapenda kuona vitu vinasababishwa na kitu kimoja, au suluhisho ni moja. Ukweli ni kwamba, chochote kinachotokea, kinasababishwa na vitu vingi, na hakuna suluhisho moja linalomaliza kila kitu.
  9. Ni rahisi kulaumu mtu mmoja au kitu fulani kwa yanayotokea. Epuka kutoa lawama kwa yeyote au chochote, inaeleza zaidi kuhusu wewe kuliko unayemlaumu.
  10. Tunapenda kuchukua hatua za haraka pale tunapokuwa kwenye hali ya hatari, hili linatupelekea kujiingiza kwenye matatizo zaidi, ni vyema kutafakari kabla ya kuchukua hatua.

Haya ndiyo maeneo kumi tunayokosea kuhusu dunia na maisha kwa ujumla, tukifanyia kazi hayo, tutaiona dunia kwa uhalisia wake.

#2 MAKALA YA WIKI; KWA NINI KANUNI YA MAFANIKIO HAIFANYI KAZI KWAKO.

Umewahi kuona kwamba wale wanaofanikiwa wanaendelea kufanikiwa, na wakati wasiofanikiwa wanazidi kuwa na matatizo zaidi? Halafu ukaambiwa zipo kanuni za mafanikio, ukazijaribu halafu hupati matokeo wanayopata wale unaoona wamefanikiwa?

Kama umewahi kujaribu kanuni fulani ya mafanikio lakini haikufanya kazi kwako, tatizo siyo kanuni, tatizo ni wewe. Na kwenye makala ya wiki hii nimeeleza kwa nini kanuni ya mafanikio haifanyi kazi kwako, na jinsi ya kuitumia vizuri. Soma makala hiyo hapa; Sababu Moja Kwa Nini Kanuni Ya Mafanikio Haifanyi Kazi Kwako, Na Jinsi Ya Kuitumia Vizuri. (https://amkamtanzania.com/2018/04/20/sababu-moja-kwa-nini-kanuni-ya-mafanikio-haifanyi-kazi-kwako-na-jinsi-ya-kuitumia-vizuri/)

#3 NILICHOJIFUNZA JUMA HILI; TATIZO NI PESA.

Rafiki, nimekuwa nakuambia hili mara zote, UMASIKINI NI MBAYA. Kila tatizo ambalo mtu au jamii inapitia, ukiichimba kwa undani, basi unakuta tatizo ni fedha.

Kwa mfano, watu wana afya mbovu kwa sababu hawana fedha za kuweza kumudu afya nzuri, hawawezi kula vizuri na mazingira wanayoishi ni mabaya na yanachochea maradhi zaidi. Wakipata fedha kidogo, inarudi kwenye tatizo la afya, na umasikini unaendelea zaidi.

Watu ni wajinga kwa sababu hawakuwa na fedha za kupata elimu, na kwa ujinga wao unasababisha kipato chao kuwa kidogo, hivyo hawawezi kuwapeleka watoto wao shule, na wao wanaishia kuwa masikini.

Tatizo la kila kitu linaanzia kwenye fedha, na fedha isipokuwepo basi matatizo yanakuwa makubwa.

Hivyo kitu kimoja unachopaswa kujikumbusha kila siku ni hichi, UMASIKINI NI MBAYA, FEDHA NI MUHIMU, NAHITAJI FEDHA ZAIDI.

Pia kaa mbali na wale wanaokuambua fedha hainunui furaha, fedha siyo kila kitu na ujinga mwingine wa aina hiyo, kama huna uhakika wa kuishi mwaka mmoja ujao iwe una kipato au la, fedha ni kila kitu kwako, na fedha ni muhimu kuliko kitu kingine kwako.

Naomba  nisisitize hili vizuri ili tuwe upande mmoja, kama ikitokea leo huwezi tena kufanya kazi ua bishara, lakini maisha yako yote yaliyobaki hayataathirika, utaweza kuendelea kula na kuendesha maisha yako, basi una haki ya kusema fedha siyo muhimu na siyo kila kitu. Lakini kama usiku hulali ukiwaza mwezi unaishaje, kama huna uhakika kesho unakula nini, na kama upo kwenye madeni, basi FEDHA NI MUHIMU SANA KWAKO, FEDHA NI KILA KITU KWAKO, la sivyo maisha yako yatakuwa magumu zaidi.

Kila wakati weka juhudi kuhakikisha unaongeza kipato chako zaidi, tenga sehemu ya kipato chako kama akiba, na wekeza kwa ajili ya kipato cha baadaye. Fedha ni muhimu, ukiondoa hewa tunayopumua, ambayo ndiyo kitu pekee tunapata bure hapa duniani, na hapo ni kama hujaumwa, basi kitu cha pili kwa umuhimu ni fedha, hakikisha unapata za kutosha na usiwasikilize wasiokuwa na fedha wanapokupa ushauri wao wa hovyo kuhusu fedha.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; PERSONAL COACHING.

Kila mwezi huwa natoa nafasi ya kufanya kazi moja kwa moja na watu wasiozidi watano. Hii ni huduma ya mimi kukukochi moja kwa moja kwenye kitu unachotaka kufanyia kazi lakini kila siku unakwama.

Kupitia programu hii, tunaweka mipango ya mwezi mzima, ya wapi unataka kufika, kisha tunagawa kwenye mipango ya wiki, na hatua za kuchukua. Kila mwisho wa wiki tunawasiliana ukinieleza hatua zipi umepiga na changamoto zipi umekutana nazo, ambapo tunajadili hatua bora zaidi za kuchukua.

Ni mwezi ambao unajisukuma kuchukua hatua zaidi ya ulivyozoea, na hilo linakuletea matokeo ambayo hujawahi kupata.

Huduma hii inalipiwa gharama ya tsh laki moja na huwa inaanza tarehe moja ya kila mwezi. Kama unapenda kuwahi nafasi za COACHING kwa mwezi wa tano basi muda ndiyo huu. Tuma ujumbe kwenye wasap namba 0717396253 wenye maneno PERSONAL COACHING kisha tutajadili eneo lipi unahitaji kukochiwa na hatua zipi tunachukua.

Karibu tufanye kazi pamoja kwa maendeleo yako.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; TABIA MOJA YA USHINDI.

“The habit of persistence is the habit of victory.” – Herbert Kaufman

Tabia ya ushindi ni moja, UNG’ANG’ANIZI. Chagua kipi unataka kwenye maisha yako, kisha amua kuyatoa maisha yako kukipata, halafu sasa, NG’ANG’ANA mpaka utakapopata kile unachotaka.

Wapo watakaokuambua unachotaka hakiwezekani, wapo watakaokuambia usijitese, wapo watakaokuambia unapotea, wapo watakaokuambia haijawahi kufanyika, lakini wote hao wana kitu kimoja kinachofanana kwao. Ni watu walioshindwa na hawawezi kuvumilia wanapoona mtu anashinda kwenye kile ambacho wao wameshindwa.

Wapuuze na NG’ANG’ANA mpaka upate kile unachotaka. Bora ufe ukipigania unachotaka, kuliko kuishi maisha ya matamanio huku huchukui hatua, kwa sababu unakuwa ni sawa na umekufa ila tu unasubiri kuzikwa.

Nenda kaweke mipango ya juma namba 17, na lianze juma hilo kwa hamasa kubwa, usikubali kupoteza muda wako, wala kuwasikiliza walioshindwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji