Rafiki yangu mpendwa,

Ushauri ni moja ya vitu ambavyo watu hawajawahi kukosa. Hata usipoomba ushauri, wapo ambao watajitolea kukushauri ni namna gani bora ya kufanya kile ambacho unafanya. Wengine watakaokushauri hawajawahi hata kufanya chochote kikubwa, ila wamekuwa wanasikia wengine wanashauri hivyo na wao wanakushauri pia.

Hivyo ili kupata ushauri mzuri, lazima wewe unayetafuta ushauri uweke kazi kubwa kwenye kutafuta ushauri mzuri kwako kuliko kazi wanayoweka wale wanaokushauri. Ushauri mzuri kwako utaupata kwa kufanya kazi ya ziada, kuwatafuta watu sahihi, ambao wamefanya, ambao wamepitia changamoto kubwa na kuzishinda. Na pia unaweza kupata ushauri mzuri wa vitu gani usifanye kwa kuangalia wale walioshindwa kabisa.

vitabu softcopy

Tukiwa hapa kwenye ushauri, kuna kundi moja la watu wanaokushauri unapaswa kuwa nalo makini sana. Hili ni kundi hatari sana kwako kiushauri. Kwa sababu japo wanaweza kuwa wanakutakia mema kupitia ushauri wao, wanakuwa wanakupoteza zaidi. Yaani mtu anakushauri akijua anakusaidia, kumbe dhana yake ya kukusaidia wewe inakupoteza zaidi.

Kundi hili ni wale watu ambao wamewekeza hisia zao kwako, wale watu ambao una mahusiano nao kwa namna moja au nyingine. Hapa nawazungumzia ndugu, jamaa na marafiki. Wale watu ambao wanakupenda wewe kwanza kabla ya kile unachofanya.

Kuba baadhi ya taaluma ambazo maadili yanazuia watu wa karibu kama hao wasihudumiane. Kwa mfano, kama wewe ni daktari, basi kimaadili hupaswi kumtibu ndugu yako wa karibu. Kadhalika kwenye sheria, kama ni wakili maadili hayaruhusu umwakilishe ndugu yako wa karibu kwenye kesi zake.

SOMA; Sababu Moja Kwa Nini Kanuni Ya Mafanikio Haifanyi Kazi Kwako, Na Jinsi Ya Kuitumia Vizuri.

Sababu inayopelekea taaluma hizi kuzuia kuwahudumia ndugu wa karibu, ndiyo hiyo pia tunaitumia kuchunguza kwa makini ushauri wa watu hawa. Na sababu kubwa ni kwamba, watu wenye mahusiano ya aina hiyo, wanakuwa wanaunganishwa zaidi kihisia. Hivyo maamuzi yoyote yanayofanywa baina ya watu hao yanakuwa yanaongozwa na hisia.

Sasa katika kufanya maamuzi, maamuzi mabovu kabisa ni yale yanayotokana na hisia na siyo kufikiri. Kwa sababu hisia zinapokuwa juu, fikra zinakuwa chini.

Kwenye ushauri, pale watu wako wa karibu wanapojaribu kukushauri, kwanza wanaangalia kitu kimoja, hawataki kukuumiza. Hivyo ushauri wowote wanaokupa, unaanza na hali ya kuepuka kukuumiza. Kuna vitu vitakuwa wazi kabisa, lakini wataogopa kukuambia wakigundua kwamba wakikuambia ukweli utaumia.

Kwa mfano kama unaanzisha biashara, ushauri wowote wa watu wako wa karibu hautakuwa ushauri mzuri. Kwa sababu kama una mipango mikubwa, watajaribu kukushauri uipunguze, ili usiumie pale unaposhindwa. Pili kama wazo lako la biashara siyo zuri na kama wanafikiri halitafanya kazi, wengi wataishia kukuambia kazana tu, utafanikiwa tu. Hawatathubutu kukueleza ukweli kwamba wazo lako lina mapungufu gani na wapi pa kuweka juhudi zaidi.

Hivyo rafiki yangu, kuwa makini sana na ushauri unaopokea kutoka kwa watu ambao mna mahusiano yanayoongozwa zaidi na hisia kuliko kufikiri. Wengi watakudanganya, kwa sababu hawataki uumie. Na sababu hiyo ndiyo itakuumiza zaidi kuliko wanavyofikiri wao.

Na kama unachotaka ni ushauri kwenye biashara yako, ni bora kuchukua ushauri wa mteja ambaye ana uhitaji lakini hakujui wewe, hivyo hajali kama utafanikiwa au utashindwa, yeye atakuambia ukweli kama ulivyo.

Kila ushauri una gharama zake, kuwa tayari kwa gharama za ushauri unaopokea kwa watu wa karibu. Japo wanaweza kuwa wanakupa ushauri huo bure, utakuumiza zaidi kwa sababu ya kuogopa kukuumiza.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/koch

Usomaji