Umewahi kusikia watu wanasema mtu fulani ana jina kubwa?

Umewahi kuona biashara ambazo zina majina makubwa? Na biashara hizo unakuta zinauza siyo kwa sababu zina bidhaa au huduma bora kuliko biashara nyingine, bali kwa sababu ni jina linaloaminika.

Kwenye dunia ambayo ina kelele za kila aina, watu hawawezi kufanya maamuzi sahihi mara zote. Kuna vitu vingi mno vya kuchagua na hawana muda wa kuchambua kila kimoja.

wp-image--1138462510

Hivyo wanachofanya ni kuamua kupitia jina au umaarufu wa kitu. Watu wanafikiria kama jina ni kubwa hivi, na wengi wanaliamini, basi itakuwa sahihi na wao kuamini.

Hii ina maana kwamba, moja ya vitu muhimu ambavyo kila mtu anapaswa kufanya kwenye maisha yake, ni kutengeneza jina lake.

Na hapa hatumaanishi lile jina ambalo umepewa na wazazi wako, bali kuongeza maana kwenye jina hilo, kiasi kwamba mtu akisikia limetajwa basi kuna taswira anaipata kwenye akili yake.

SOMA; UKURASA WA 923; Anayekutawala Anakunyima Vitu Hivi Vitatu…

Ili kujenga jina lako, chagua kitu kimoja au vichache ambavyo unataka kujulikana kupitia vitu hivyo. Kisha fanya vitu hivyo kwa ubora wa hali ya juu sana, vijue nje ndani na hakikisha yeyote anayekwama kwenye vitu hivyo basi anakuja kwako, hii itakutofautisha na wengine na jina lako litakuwa kubwa.

Njia nyingine ni kuwa na ujumbe ambao unaotoa kila mara na kwa kila mtu kiasi kwamba mtu akisikia jina lako, ule ujumbe unamjia kwenye mawazo yake mara moja. Unahitaji kurudia ujumbe huo kila mara mpaka watu washindwe kukutofautisha wewe na ujumbe wako.

Hii ni kwa maeneo yote, iwe unatengeneza jina binafsi au unatengeneza jina la biashara yako, kujitofautisha kwa ubora na kwa ujumbe wa kipekee ni njia bora ya kutengeneza jina lako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog