Watu wengi huwa wanakwama kwenye safari ya mafanikio,
Wanakuwa wanajua kabisa nini wanataka kwenye maisha yao, lakini wanashindwa kuchukua hatua ili kuweza kufika au kupata kile wanachotaka.
Wengi huwa hawajui ni wapi wanakwama, na hivyo inakuwa vigumu kwao kuchukua hatua.

Lakini ukipata nafasi ya kuchunguza kwa undani, utakuta watu wengi wanakwama kwenye moja ya maeneo haya matatu.
Eneo la kwanza; KUPANGA.
Kujua tu unachotaka au unakotaka kufika haitoshi kukufikisha, lazima ukae chini na kupanga, unafikaje pale. Kuna hatua nyingi za kupita mpaka ufike, hivyo lazima uzipangilie hatua hizo vizuri. Lazima ujue unaanzia wapi na kipi kinafuata. Lazima ujue hatua unazopaswa kuchukua kila siku, kila wiki, na kila mwezi. Lazima uweze kupima kila hatua unayochukua. Bila mipango, huwezi kupiga hatua.
Eneo la pili; MAANDALIZI.
Wengi wakishajua wanachotaka, wanakurupuka na kuanza kufanya, hivyo wanajikuta wanafanya mengi na hakuna matokeo wanayopata. Wanachokosa wengi ni maandalizi, hivyo hata wanapojua wanachopaswa kufanya, wanakuwa hawana maandalizi ya kuwawezesha kufanya wanachopanga kufanya.
Wanajikuta kwenye hali ambayo haiwapi nafasi nzuri ya kuchukua hatua, na hivyo kila hatua wanazochukua zinawapelekea kushindwa. Chochote unachofanya, maandalizi ni muhimu. Maandalizi kabla ya kuanza, na maandalizi wakati unaendelea kufanya ni muhimu. Kila hatua kubwa unayopiga, lazima uwe umejiandaa.
Na kujiandaa ni pande zote mbili, kujiandaa pale unaposhindwa ujue utachukua hatua gani, maana hapo ndipo wengi wanakwama. Pia ujiandae pale unapofanikiwa nini kinaendelea, maana mafanikio nayo yanawakwamisha wengi.
SOMA; UKURASA WA 1083; Saa Moja Takatifu Ya Maisha Yako…
Eneo la tatu; MATEGEMEO.
Haijalishi unachukua hatua kiasi gani, unapata kile unachotegemea kupata. Ni hivyo tu, hivyo kama umeweka mipango yako vizuri, umejiandaa na unachukua hatua sahihi, lakini matokeo unayopata ni ya tofauti, hebu anza kujichunguza ndani yako ulitegemea upate nini. Kama unakuwa na wasi wasi kwamba huwezi kufika unakotaka kufika, basi hutafika. Kama unajiona utashindwa, ni kweli utashindwa. Mategemeo yako yana nguvu kubwa sana kwenye matokeo unayopata.
Hivyo rafiki, unapokwama, angalia maeneo haya matatu, je umeweka MIPANGO yako vizuri, je UMEJIANDAA kabla na hata baada ya kupata matokeo? Na je UNATEGEMEA kupata matokeo gani, maana hicho ndiyo unapata mara zote.
Tatua pale unapokwama ili uweze kufanikiwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog