Watu wengi huwa wanapenda kubadili vitu mbalimbali kwenye maisha yao, lakini wanashindwa.
Wanataka kuibadili dunia, lakini kila wanachojaribu kinawashinda.
Wanataka kuwabadili wengine, lakini kila juhudi wanazotumia zinashindwa.
Wanataka kuibadili dunia lakini hawajui hata waanzie wapi.
Lipo sharti la kwanza muhimu sana unalopaswa kuzingatia kwenye chochote unachotaka kubadili.

Sharti hilo ni kujua kwanza jinsi kitu hicho kilivyo na kinavyofanya kazi.
Kama unataka kuibadili dunia, jua kwanza dunia ilivyo na jinsi inavyofanya kazi.
Kama unataka kuwabadili wengine, wajue kwanza jinsi walivyo na namna wanavyofanya maamuzi na kufanya mambo yao.
Na hata kujibadili wewe mwenyewe, jijue kwanza kiundani, jijue kinachokusukuma, jua jinsi unavyofanya maamuzi na unavyofanya kazi.
SOMA; UKURASA WA 1109; Kuchukua Hatua Ni Bora Kuliko Kuwa Sahihi…
Hili ni sharti muhimu na hitaji la msingi kabisa kwenye mabadiliko yoyote unayotaka kufanya.
Kwa sababu usipokijua kitu kwa undani, hatua zozote ambazo utachukua, hazitakuwa hatua halisi za kuweza kuleta mabadiliko.
Utabadili vitu vya juu, ambavyo haviathiri kiini muhimu cha mabadiliko.
Na hii ndiyo sababu kwa nini ni vigumu sana kuwabadili wengine, kwa sababu ni vigumu sana kuwajua wengine kiundani.
Ndiyo maana mabadiliko muhimu unayoweza kufanya kwenye maisha yako ni kuanza na wewe mwenyewe, kwa sababu unaweza kujijua vizuri zaidi kuliko wengine.
Inapokuja swala la mabadiliko, sahau kuhusu haraka, sahau kuhusu njia za mkato, unachohitaji cha msingi kabisa ni kujua kitu kwa undani, kujua jinsi kinavyofanya kazi ili unapobadili, ujue wapi pa kubadili.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog