Habari za leo rafiki yangu?

Tarehe 13 Machi 2018 serikali kupitia waziri wa sanaa na michezo ilitangaza kanuni mpya za udhibiti wa maudhui yanayotolewa kwa njia ya mtandao wa intaneti.

Kanuni hizi zimeeleza wajibu wa waendeshaji wa mitandao inayotoa habari yaani blogu na kutoa maelekezo ya blogu zote kusajiliwa na mamlaka ya mawasiliano kabla ya kuruhusiwa kuendesha shughuli zake nchini.

Baada ya tangazo hili wengi wamekuwa wananiuliza nini hatima ya AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA, kutokana na ukali wa sheria je mitandao hii ambayo wengi wamekuwa wanatumia kujifunza na kuhamasika kwa miaka mitano sasa itaendelea kuwepo?

Nimekuwa nawajibu wale wanaouliza lakini kwa kuwa wengi wanaendelea kuuliza, nimeona ni vyema kuandaa makala hii fupi ambayo itaelezea nini hatima ya mitandao hii kwenye sheria hii mpya.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Kwanza kabisa sitazungumzia iwapo sheria ni mbaya au ni nzuri, kama ni sahihi au siyo sahihi, kama umekuwa mfuatiliaji wa kazi zangu kwa muda, unajua falsafa ninayoishi, huwa silalamiki wala kumlaumu yeyote, kama kitu sikipendi nakibadili, kama siwezi kukibadili naachana nacho. Kulaumu hakujawahi kuwa na msaada kwenye maisha yetu.

Sasa tukirudi kwenye sheria na kanuni hii mpya kwa ufupi, ina mahitaji makubwa kidogo ili kuweza kuendesha blog. Mahitaji makuu ni blog iwe inaendeshwa kama kampuni iliyosajiliwa, yenye wakurugenzi na wafanyakazi. Pia hitaji jingine ni kulipa ada, ambapo kuna ada ya maombo shilingi laki moja, ada ya leseni shilingi milioni moja, ambayo leseni inakaa kwa miaka mitatu, na ada ya kila mwaka ambayo ni laki moja. Hivyo ukijumlisha na kugawa hizo ada vizuri unapata wastani wa shilingi laki tano kila mwaka unayopaswa kulipa ili kuendesha blogu.

Sasa nini hatima ya AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA?

Tangu nimeanza blog hizi, AMKA MTANZANIA imekuwa blog ya bure kabisa na watu hawahitaji kulipa chochote kuitembelea. Japo kuiendesha kunagharimu, lakini nimekuwa naitumia kama sehemu ya kusambaza elimu muhimu bure kabisa kwa wale inaoweza kuwasaidia. Na kulingana na mrejesho ninaopata kwa wengi, imekuwa msaada.

KISIMA CHA MAARIFA imekuwa blogu ya kulipia, ambapo ili uweze kusoma makala, unahitaji kulipa ada ya shilingi elfu 50 kwa mwaka. Ni ada hizi ndiyo zinawezesha mitandao yote hata ule wa AMKA MTANZANIA ambao watu hawalipii kuweza kuwa hewani.

Ili mitandao ninayoendesha iwe hewani, kwa mwezi huwa nalipa gharama za dola mia moja, ambapo ni kama laki mbili na nusu za Kitanzania, kwa mwaka ni kama milioni tatu, ambazo hizi ni kuhakikisha mitandao inakuwa hewani, watu wanapokea email na vingine vingi.

Gharama zote hizi zimekuwa inalipwa kutokana na wale wachache wanaojiunga na KISIMA CHA MAARIFA, ndiyo wanawawezesha wengi zaidi kusoma makala nyingi bure bila ya kukipa chochote.

Hivyo ukilinganisha gharama za uendeshaji za sasa, na ile ya usajili wa serikali ambayo itaongeza shilingi laki tano kwa mwaka, ni kiasi ambacho tutaweza kukilipa na huduma zetu zinaendelea kama kawaida.

Hivyo napenda kuwaambia wote kwamba, tutafuata mchakato wa kusajili blog hizi, lakini siyo katika kipindi cha ukomo kilichowekwa na serikali. Kwa sababu nimekuwa naendesha shughuli hizi chini ya jina la biashara AMKA CONSULTANTS, sasa sheria mpya inahitaji blog iwe chini ya kampuni. Hivyo tutaanza na mchakato wa usajili wa kampuni kwanza, kisha baadaye kusajili blog kwa mujibu wa sheria.

Hivyo basi kwa kipindi hichi kilichotolewa, mpaka mwisho wa tarehe 05 May hatutakuwa tumekamilisha hilo, hivyo mitandao itaendelea kuwa hewani, na iwapo itafungwa kwa kuchelewa kuandikisha, basi tutaona njia ipi bora ya kuendelea kutoa mafunzo haya.

Nipo tayari kulipia gharama yoyote kuhakikisha mafunzo haya yanaendelea kuwafikia wengi, kwa sababu kwa miaka mitano sasa nimekuwa natoa mafunzo haya na wengi wamenufaika. Pia wengi walionufaika wapo tayari kulipia huduma mbalimbali ili mitandao hii iendelee kuwa hewani.

Pia kutokana na mabadiliko haya, huenda gharama za huduma ambazo tumekuwa tunatoa zikaongezeka, hasa ada ya KISIMA CHA MAARIFA na hata vitabu mbalimbali tunavyouza. Hivyo litakaokuja hilo, lisiwe geni kwako rafiki yangu.

Mwisho kabisa napenda nikuahidi kitu hichi kimoja, hata itokee nini, nitaendelea kuandika kila siku, hii ni ahadi ambayo nimejiwekea na nafsi yangu, hivyo hata kama nitasoma mwenyewe kile ninachoandika, nitaendelea kuandika.

Hivyo basi, kwa kuwa kuna viashiria vingi vya mitandao ambayo tumezoea kuitumia bure kushirikishana maarifa haya kuendelea kubanwa zaidi, nahitaji kukusanya mawasiliano ya wale marafiki ambao ni wa kweli kabisa, ambapo wapo tayari kuingia gharama yoyote kuhakikisha wanaendelea kupata mafunzo haya, bila ya kujali nini kinatokea.

Hivyo rafiki, nimeandaa fomu maalumu, ya kukusanya majina na mawasiliano ya simu na email kwa wale ambao ni MARAFIKI WA KWELI WA KOCHA DR MAKIRITA AMANI.

Siyo lazima ujaze fomu hii, na usipojaza haimaanishi kwamba wewe siyo rafiki yangu. Bali ukiijaza umeniambia kwamba wewe upo tayari kuendelea kupata mafunzo ninayotoa kwa gharama yoyote ile. Hivyo kama itatokea leo mitandao yote ikafungwa, upo tayari kutumia njia nyingine zitakazofaa kupata mafunzo ninayotoa, hata kama nitaandika kama barua na kukutumia kwa njia ya posta.

Hivyo rafiki, kama kweli umejiridhisha kwamba upo tayari kuendelea kupata mafunzo ninayotoa kwa gharama yoyote, bonyeza hapa na ujaze fomu inayofunguka.  (fungua; https://docs.google.com/forms/d/e/1FAIpQLSesUf4O_TCeWGh9dhgiwORb5NCVpaAZGRzO-VjThbnxOcG_oQ/viewform?usp=sf_link )

Nikushukuru sana rafiki yangu kwa namba ambavyo tumeendelea kuwa pamoja. Napenda sana kujifunza, napenda sana kufundisha na mtandao wa intaneti umeweza kulirahisisha sana hili kwangu. Lakini hata kama mtandao huu utaondoka au kuondolewa, huo hautakuwa mwisho wa mimi kufanya kile ninachopenda kufanya. Nitaendelea kukifanya kwa njia itakayofaa kwa wakati huo. Kwa sababu watu wamekuwa wakijifunza kwa zaidi ya miaka elfu 3 iliyopita, na mtandao wa intaneti umekuwepo kwa miaka kama 30 tu. Hivyo huduma hii haitakufa kwa namna yoyote ile kama mimi nitakuwa hai, na kama hutaki kukosa huduma hii, usisahau kujaza fomu hii hapa. (fungua link hii; https://docs.google.com/forms/d/e/1FAIpQLSesUf4O_TCeWGh9dhgiwORb5NCVpaAZGRzO-VjThbnxOcG_oQ/viewform?usp=sf_link )

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji