Kitu rahisi kabisa kufanya duniani, ni kutoa ushauri, kila mtu anaweza kufanya, hata mtoto wa miaka mitano anaweza kushauri.
Na ndiyo maana, kila mtu huwa ana ushauri wa kutoa kwenye jambo lolote lile, hata kama siyo mtaalamu na hana uzoefu. Watu watatoa hata ushauri waliosikia wengine wanatoa.

Sasa katika ushauri, upo ushauri mbovu sana ambao kila mtu anapaswa kuwa nao makini.
Kuna ule ushauri ambao unaenda kumwomba mtu, ambapo unakuwa umemweleza tatizo lako, amelielewa kwa undani, amekuhoji maswali, kisha baada ya kutafakari, akakuambia kama angekuwa yeye angefanya nini. Lakini pamoja na hayo, hakulazimishi ufanyie kazi ushauri huo, badala yake anakutaka utafakari na ukiona unafaa uutumie, lakini ukijua unaweza kuwa na madhara pia.
Kuna ule ushauri ambao ni wa kujitolea, ushauri ambao hujaomba mtu akupe, lakini yeye anakupa. Amekuja kwenye biashara yako na kuanza kukuambia hapa ungefanya hivi, ungeweka kile, ungefanya kama fulani na kadhalika. Hawa ni washauri ambao kwa kuona, au kusikia watakuja na njia ambazo unapaswa kufuata, hapo hata hawajaelewa kwa undani unachofanya au unachopitia. Halafu sasa, wanataka usikilize ushauri wao, uufanyie kazi, la sivyo utakuja kujuta.
SOMA; UKURASA WA 76; Jinsi Ushauri Unavyoweza Kufanya Kazi Kwako
Huu wa pili ndiyo ushauri hatari kabisa kwenye maisha yako, ni ushauri unaopaswa kuuogopa mno, yaani ufute haraka sana unapoanza kuusikia, na mtu anapoanza kukushauri kabla hujamwomba, mwombe aishie hapo hapo.
Iwapo unaona mtu anaweza kukushauri vizuri, na ameanza kujitolea kukushauri, usipokee ushauri wake haraka, badala yake mwombe mpate muda, umweleze kila unachopitia, umwambie kila hatua ambayo umeshachukua kisha mwambie wapi anataka kufika. Halafu muulize kama angekuwa yeye angefanya nini.
Utagundua baada ya watu kujua kwa undani, ushauri unabadilika, utaona wanaanza kufikiria kwa kina na kuacha kushauri mambo ya kawaida, ambayo kila mtu anaongea.
Kuwa makini na ushauri wa kujitolea, kamwe usifanye maamuzi kwenye maisha yako kwa sababu ya ushauri ambao mtu amejitolea kukupa, ambao hata hujamwomba akupe. Kama unaona mtu anaweza kukushauri, hakikisha unamwelezea hali yako ili akushauri kwa usahihi zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog