Mtu akikuambia anataka umlipe hela ili akufundishe jinsi ya kusikiliza utamcheka, au siyo? Kwa sababu utaona ni kitu cha ajabu mno. Yaani ufundishwe jinsi ya kusikiliza, kwamba huna masikio au una matatizo gani?

Lakini ukweli ni kwamba, kila mmoja wetu ana mengi ya kujifunza kuhusu kusikiliza. Na kwenye zama hizi tunazoishi sasa, ambazo kila mtu anapiga kelele na hakuna mwenye muda wa kusikiliza tena, jinsi ya kusikiliza umekuwa ujuzi adimu sana.

Furaha

Hivyo unahitaji kujifunza jinsi ya kusikiliza, na akijitokeza mtu wa kukufundisha hilo, uwe tayari kumlipa chochote anachostahili kulipwa.

Leo tunakwenda kukumbushana yale muhimu kuhusu kusikiliza, kwa sababu, kama kipo kitu muhimu sana, ni kusikiliza.

Kama kila mtu angeweza kusikiliza kwa umakini, sehemu kubwa ya matatizo yanayotokea kwenye jamii wala yasingekuwepo.

Kama watu wangeweza kusikilizana kwa makini kwenye mahusiano, sehemu kubwa ya matatizo ya mahusiano yasingetokea kabisa.

Kama watu wangesikiliza kwa makini maelekezo wanayopewa kwenye kazi, afya na mengineyo, mambo yangekuwa rahisi na changamoto chache.

Lakini tatizo watu hawasikilizi, na hawajui kama hawasikilizi.

SOMA; UKURASA WA 939; Sikiliza Zaidi Ya Unavyoongea…

Hivyo mambo muhimu kuhusu kusikiliza;

Anapoongea mtu kaa kimya na sikiliza, sikia kila neno analosema.

Anapoongea mtu sikia kile anachosema, usitumie muda huo kufikiria utamjibu nini, kazana kumsikiliza kwanza.

Anapoongea mtu msikilize huku unamwangalia, mwangalie uone jinsi sura yake ilivyo wakati anaongea, uone vitendo anavyoonesha wakati anaongea.

Anapoongea mtu elewa kile ambacho hakisemi lakini anamaanisha, kupitia ukali au upole wa sauti, uharaka au utaratibu wa uongeaji wake, yote hayo yana kitu cha kukufanya uelewe zaidi.

Anapoongea mtu na ukawa kuna kitu hujaelewa au kusikia vizuri, muulize anamaanisha nini au arudie kwa sauti ili uelewe.

Anapoongea mtu na akamaliza, subiri sekunde chache, utafakari aliyosema kabla hujaanza na wewe kuongea.

Hayo yanatosha kwa leo, jifunze kusikiliza na sikiliza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog