“Never let the future disturb you. You will meet it, if you have to, with the same weapons of reason which today arm you against the present” – Marcus Aurelius

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Tumepata nafasi nyingine nzuri sana kwenye maisha yetu, ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UTAIKUTA KESHO…
Tunapofikiria wakati ujao, huwa tunakuwa na hofu na mashaka iwapo tutaweza kweli kukabili wakati huo.
Hali hiyo inatusumbua kiasi cha kushindwa kuishi vizuri na kuchukua hatua kwa wakati ambao tunao.

Tunapata wasiwasi mkubwa kwa kesho, lakini sasa hakuna kikubwa tunachoweza kubadili leo kwa kuhofia kesho.
Njia pekee ya kuwa na kesho bora, ya kuweza kukabili chochote kitakachotujia kesho, ni kuishi vizuri leo.

Hivyo rafiki, hakuna haja ya kuruhusu muda wetu upotee kwa kuhofia keaho, hakuma haja ya kushindwa kuishi vizuri leo kwa sababu ya kesho.
Utaikuta kesho ikishafika hiyo kesho, lakini leo, fanya kila unachoweza kufanya, tumia vizuri muda wako wa leo.

Kama utaishi vizuri leo, huna haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itakuja na itakukuta ukiwa bora zaidi.
Lakini kama utakuwa na wasiwasi kuhusu kesho, na hilo likakufanya usichukue hatua sahihi leo, utaikuta kesho ukiwa hovyo zaidi na mambo yatakuwa mabaya zaidi.

Ili kesho iwe bora kwako, ishi vizuri leo, achana na kila hofu kuhusu kesho na kazana kuchukua hatua leo, kwa wakati ulionao sasa.
Una mengi ya kufanya leo, usikubali kesho ikuzuie kuchukua hatua leo.

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha