Kila mmoja wetu ana rafiki au marafiki katika maisha yake. Tunatakiwa kuwa na marafiki wenye tabia njema, maadili mema na wanaokubalika na jamii yako inayokuzunguka.

Wazungu wanasema tell me your friend and I will tell you who you are wakimaanisha kuwa niambie rafiki yako nani na nitakwambia wewe ni mtu wa namna gani.

Katika zama hizi za taarifa tumekuwa na mitandao ya kijamii inayotukutanisha na marafiki mbalimbali karibu kila pembe ya dunia. Na watu wamekuwa wanaitumia hii mitandao ya kijamii kwa faida na wengine kwa hasara.

Tumeifanya mitandao ya kijamii kuwa ni sehemu ya kuanika mambo yetu hadharani. Watu wamekuwa wanaanika hata mambo yao ya siri katika mitandao ya kijamii. Kwa kuwa tunaunganisha na marafiki wengi katika mitandao ya kijamii tunajua kwamba kila rafiki ambaye tuko nao kwenye mitandao ya kijamii hata wale ambao hatupo nao kwenye jamii kila mtu anafaa kumwambia siri zetu.

umbeya

Je tunatengenezaje mazingira ya sisi wenyewe kuonekana hayawani katika zama hizi za taarifa? Tunaruhusiwa kuwa na marafiki wengi katika maisha yetu lakini unaruhusiwa kumwamini mmoja tu katika siri zako. Unajitengenezea mazingira ya wewe kuwa hayawani pale unapomfunulia siri zako kila mtu. Ukimfunulia kila mmoja siri zako wewe unakuwa hayawani tena na hufai.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; SKIN IN THE GAME (Kukosekana Kwa Usawa Kulikojificha Kwenye Maisha Ya Kila Siku).

Ni wangapi sasa siku hizi walivyokuwa hawafai na mitandao ya kijamii imewafanya kuwa hayawani? Watu wamekuwa wanajiachia tu kumwaga siri zao hadharani wakiamini kila mtu anastahili kuambia hapana, unatakiwa kuwa na marafiki wengi lakini unayetakiwa kumfunulia siri zako ni mmoja tu tena unayemwamini na ni mwaminifu kweli.

Lakini siku hizi, imegeuka kawaida tu watu wanaona ni kitu cha kawaida sana kuanika siri za ndani katika mitandao ya kijamii na baadaye watu wanakuja kutumia hizo taarifa kuwafanya kuwa watumwa wa hali ya juu.

Kama kila mtu anajua mambo yako au siri zako zote unakuwa unatofauti gani na mtu ambaye anatembea uchi? Kuwa makini sana na marafiki wa zama hizi siyo kila mtu anapaswa kujua mambo yako bali rafiki mmoja tu unayemwamini kwa sababu rafiki unayemwamini ni mtu wa karibu kwako, siku hizi watu wanatembea na vipaza sauti ukiwaambia siri zako ni kama vile unamnong’oneza mtu huku ukiwa umeshika kipaza sauti mdomoni.

SOMA; Kitu Pekee Ambacho Mtu Mwenye Wivu Hana

Hatua ya kuchukua leo, unatakiwa kumwamini mtu mmoja tu katika siri zako.Ukimfunulia kila mmoja siri zako basi wewe unakuwa hayawani na hufai. Kuwa makini sana katika zama hizi uhuru wa kimtandao usije kukufanya kuwa mtumwa maisha yako yote.

Hivyo, basi, shabaha yangu siyo kukuambia usiwe na marafiki hapana kuwa nao lakini mtu wa kumshirikisha siri zako siyo kila rafiki bali awe mmoja tu tena mwaminifu. Unageuka hayawani pale unapomfunulia kila mtu siri zako.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu, kwa kutembelea tovuti  hii  hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana !