Fanya chochote unachotaka kufanya na wapo watakaosema unakosea, hata kama unaona unafanya kitu sahihi kiasi gani. Hata kama utachukua fedha zako na kwa roho yako moja ukaamua kugawa kwa wengine, wapo watakaokuambia bora ungefanya nazo kitu kuliko kugawa.

gold coins

Hivyo basi, kutaka kila mtu akubaliane na wewe, ni moja ya mambo ya ajabu sana unayoweza kuwa unafikiria, na kuamua yakurudishe nyuma. Kwa sababu halitatokea hilo, hakuna chochote utakachofanya na kila mtu akakubaliana na wewe.

Hata wale ambao hawakuambii chochote, wengi hawana tu muda wa kuanza kukueleza kwa nini unachofanya siyo sahihi, hata kama ni kizuri kiasi gani.

SOMA; UKURASA WA 859; Ujasiri Unahitajika Pia…

Unapochagua kipi cha kufanya, chagua kwa namna unavyojua ni sahihi na kwa namna ambavyo ni muhimu kwako. Ukishatimiza hivyo viwili, watu wanafikiria au kuchukuliaje siyo juu yako tena.

Usitake kusubiri mpaka kila mtu akubaliane na wewe ndiyo ufanye kitu. Usitake kukosa watu wa kukupinga kabisa. Fanya kile ambacho ni sahihi na ni muhimu. Na wale sahihi na muhimu wataambatana na wewe.

Ukifanya kile ambacho ni sahihi, na ukasimamia kile unachoamini, mwisho wa siku hata wale ambao hawakubaliani na wewe, watakuheshimu kwa hatua unazochukua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog