“The price you will offer yourself to the world, is how much they will buy you.” – Lailah Gifty Akita
Ni siku nyingine nzuri, siku bora na ya kipekee ambapo tumepata fursa nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UTALIPWA UNACHOTAKA DUNIA IKULIPE…
Chochote unacholipwa sasa, iwe ni kwenye ajira au biashara, ndiyo kiasi ambacho wewe mwenyewe umeitaka dunia ikulipe, siyo zaidi na siyo pungufu.
Hivyo kama unacholipwa ni kidogo, jua kabisa tatizo siyo anayekulipa, bali tatizo ni wewe mwenyewe, kwamba umekubali kupokea kidogo na umeridhika nacho, hujataka kupata kikubwa zaidi.
Dunia inatoa kile ambacho watu wanataka, kile ambacho wanakipigania. Na dunia huwa haimbembelezi yeyote, bali inatoa kulingana na uhitaji wa wengine.
Hivyo rafiki, kama unachopata au kulipwa sasa hakikutoshi, huna haja ya kuhangaika na yeyote, bali anza na wewe binafsi.
Anza kwa kujiuliza kwa nini umeridhika na kiasi hicho kwa muda wote huo?
Halafu nenda ujiulize ni hatua zipi za kuchukua ili kuongeza kipato chako zaidi?
Dunia inafuata kile unachoiambia, kama unaiambia umeridhika na hupambani tena inakuacha ulivyo.
Kama unaendelea na mapambano itafika mahali na kukupa chochote unachotaka.
Leo nenda kaiambie dunia ni kiasi gani unastahili kulipwa, kisha weka juhudi na maarifa yanayoendana na kiasi hicho.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha