Habari rafiki,

Hili ni darasa la falsafa ya Ustoa ambalo liliendeshwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Kutokana na umuhimu wa falsafa hii na jinsi inavyoweza kutusaidia kwenye maisha, nimewashirikisha wote darasa hili ili tuweze kujifunza na kuchukua hatua. Kujifunza zaidi karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA.

UTANGULIZI KUHUSU FALSAFA.

Tangu enzi na enzi kumekuwepo na falsafa mbalimbali hapa duniani.

Falsafa imekuwa ni njia ambayo wanadamu wamekuwa wakiitumia kuielewa dunia, kuyaelewa maisha na kujua kwa nini wapo hapa duniani.

Maisha yetu sisi binadamu ndiyo maisha ya viumbe ambao hawajaandaliwa kuendana na mazingira tunayoishi, hivyo inatuhitaji sisi kutumia uwezo wa tofauti tuliopewa ambao ni fikra zetu kuweza kutumia yale mazingira ambayo tumewekwa.

Kwa kutumia falsafa, watu wameweza kuyaelewa dunia na maisha na kujitengenezea misingi ambayo imewawezesha kuweza kuishi hata kwenye mazingira magumu.

Kumekuwa na falsafa nyingi sana hapa duniani, kulingana na mazingira ya watu na tamaduni zao. Lakini siyo falsafa zote zimeweza kudumu kwa muda mrefu, kadiri maisha yamekuwa yanabadilika, falsafa za watu pia zimekuwa zinabadilika.

Dini zote ni mfumo wa falsafa, lakini siyo falsafa zote ni dini.

Dini kama Ukristo, Uislamu, Ubudha na nyinginezo zimejengwa juu ya mfumo fulani wa kifalsafa, ambao unawaongoza watu kuweza kuwa na maisha bora hapa duniani na hata baada ya kuondoka hapa duniani.

Kila mmoja wetu kuna falsafa anayoishi, ukiacha dini ambazo wengi wetu ni wafuasi, kuna ile misingi ya maisha, ambayo huenda umejifunza kwenye jamii au umeiga kwa wengine namna ambavyo wanaishi.

Changamoto ni kwamba, wengi hatujui ni falsafa gani tunaishi na ina manufaa gani kwetu.

Hivyo kwenye darasa la leo tunakwenda kujifunza kuhusu falsafa ya Ustoa na namna tunavyoweza kuitumia kuwa na maisha bora.

Falsafa ya Ustoa imeweza kudumu kwa zaidi ya miaka 2500 hii ikionesha kwamba ni falsafa ambayo inafaa kwenye nyakati zote. Pia tofauti na falsafa nyingine za kidini, ustoa siyo dini, bali ni mfumo wa maisha ambao mtu unachagua kuishi, ili maisha yako yawe bora.

Huhitaji kujiunga na kikundi chochote ili kuwa mstoa, wala huhitaji kumwambia yeyote kwamba wewe ni mstoa. Unachohitaji ni kuijua misingi ya ustoa na kuiishi, kisha kufaidi matunda ya falsafa hii ambayo ni kuwa na maisha bora na yenye furaha wakati wote.

Karibuni sana kwenye darasa hili la falsafa ya ustoa, tuweze kujifunza kuishi falsafa hii bora kabisa kwetu.

KARIBU KWENYE DARASA LA FALSAFA YA USTOA;

ustoa2

  1. HISTORIA FUPI YA FALSAFA YA USTOA NA WANAFALSAFA WANNE WALIOIKUZA FALSAFA HII.

Falsafa ya ustoa ilianzia kwenye mji wa Anthens ugiriki, miaka ya 300 kabla ya kristo na baadaye kuhamia Roma.

Falsafa hii ilianzishwa na mwanafalsafa Zeno, ambaye kabla ya kuwa mwanafalsafa alikuwa msimamizi wa biashara ya familia, akiwa safarini na meli, alisimama Anthens kwa ajili ya matengenezo ya meli. Akiwa Anthens alikuwa na muda wa ziada, hivyo akaingia kwenye maktaba na kukutana na maandiko ya mwanafalsafa Socrates. Alipenda maandiko yale, na kumuuliza mhusika wa maktaba wapi anaweza kupata mafunzo zaidi kama hayo ya Socrate, wakati huo alikuwepo mwanafalsafa mwingine anayeitwa Crates ambaye alikuwa mwanafalsafa wa falsafa ya Cynics. Mhusika wa maktaba alimwambia mfuate huyo, na alimfuata kwenye mafunzo yao na aliyapenda.

Falsafa ya Cynics ilikuwa falsafa ya kuishi maisha kama vile ni siku ya mwisho kuishi, hivyo hawakujisumbua na umiliki wa vitu au mali, bali kuishi maisha bora kwao. Jina la Cynic kwa kigiriki lilimaanisha Mbwa hivyo wanafalsafa hao waliishi kama Mbwa, asiye na makazi maalumu.

Baada ya kujiunga na Falsafa hii, Zenu hakurudi tena kwenye biashara ya familia. Badala yake alitumia muda wake kujifunza kutoka kwa wanafalsafa mbalimbali.

Kufika mwaka 300 kabla ya kristo, Zeno alikuwa ameshajifunza vya kutosha, na alichoshwa na falsafa ya Cynic ambayo ilikuwa na mtazamo mwembamba kuhusu maisha. Hivyo alianzisha darasa lake la falsafa ambapo alikuwa akikaa chini ya mti unaoitwa Stoa na kujadili falsafa na kila aliyejali kusikiliza.

Kwa sababu falsafa hii ilikuwa ikifundishwa chini ya mti wa Stoa, wanafalsafa wa falsafa hii walianza kuitwa Wastoa, na hapo ndipo jina na falsafa ya ustoa ilipoanzia.

UTATU WA MAFUNZO YA USTOA.

Zeno alifundisha utatu huu kwenye maisha na kuielewa dunia.

Kwanza ni kuielewa asili ya dunia (fizikia)

Pili kuelewa akili na uwezo wa kufikiri (logic)

Tatu kuishi misingi ya maadili (ethics)

USTOA WA ROMA.

Falsafa ya ustoa ambayo ilianzia Ugiriki, baadaye ilisambaa na kufika Roma, ambapo kwa wakati huo Roma ilikuwa dola imara na yenye nguvu kubwa.

Kufika Roma falsafa hii ilipokelewa na watu ambao waliikubali na kuiishi maisha yao yote. Wengi wa wanafalsafa wa ustoa wa Roma waliuawa au kulazimishwa kujiua kutokana na kukataa kuishi kinyume na misingi ya falsafa hiyo.

Baadhi ya wanafalsafa wa ustoa wa Roma walikuwa Cato, Cicero, Musonius Rufus, Seneca, Epictetus na Marcus Aurelius.

WANAFALSAFA WANNE WALIOKUZA FALSAFA YA USTOA NA BAADHI YA MISINGI WALIYOISHI NA KUFUNDISHA.

ZENO.

Hutu ndiye baba wa falsafa ya ustoa, na kama tulivyoona kwenye historia ya falsafa hii hapo juu, alijifunza kupitia falsafa mbalimbali kisha kuja na mfumo wa falsafa ya ustoa, ambao unamwezesha mtu kuishi maisha bora kwake.

Lengo kuu la falsafa ya ustoa limekuwa kuwapa watu uhuru juu ya maisha yao, kuishi kulingana na sheria za asili na kutokuweka mategemeo na furaha zao kwenye mambo ya nje.

Falsafa ya ustoa imekuwa ikihusishwa na watu kutokuwa na hisia au kukandamiza hisia zao, lakini ukweli ni kwamba, kupitia falsafa hii, watu wanazielewa hisia zao na kutokuruhusu ziwazuie au kuwaharibia maisha yao.

Kwa sababu changamoto kubwa kwenye maisha huwa zinaanzia kwenye hisia.

Zenu hakuwa mwandishi mzuri, ila alipenda kufundisha na kujadili falsafa. Zipo kazi chache sana za Zeno ambazo zimeweza kupona katika kipindi hicho kirefu, na kazi hizo ni maandiko ambayo wanafunzi wake waliandika wakati akifundisha.

zeno of citium

SENECA.

Seneca, alikuwa ni mmoja wa viongozi wa serikali ya Roma na mtu aliyeheshimika sana enzi zake.

Ni mmoja wa wanafalsafa walioiishi falsafa hii kwa vitendo na kutokana na misingi yake ya maisha aliweza kuchaguliwa kuwa mwalimu wa Mfalme mdogo wa Roma aliyekuwa anaitwa Nero.

Nero alikuwa kijana mdogo ambaye hakuwa na misingi lakini alirithi kuwa mfalme wa dola hii. Hivyo kwa kipindi ambacho Seneca alikuwa mwalimu wake, Roma ilienda vizuri sana.

Baadaye Seneca alishutumiwa kutumia vibaya madaraka na Nero aliamuru auawe. Seneca aliomba ajiue mwenyewe ili kusimamia misingi ya falsafa ya ustoa. Hivyo alijikata na kutokwa damu mpaka kufa.

Seneca ni mmoja wa wanafalsafa ambao wamechangia sana kukua kwa falsafa ya ustoa. Ni mwanafalsafa ambaye aliandika sana na kazi zake nyingi zipo mpaka sasa.

Moja ya maandiko yake muhimu ni Barua za kifalsafa ambazo alikuwa akimwandikia rafiki yake Lucilius ambazo zilijadili karibu kila kitu kuhusu maisha. Kuanzia falsafa, kushinda hasira, kujenga tabia nzuri na hata mahusiano.

Baadhi ya misingi ambayo Seneca alifundisha na kuishi ni hii;

Falsafa ndiyo njia pekee ya watu kuwa pamoja na jamii kuendelea.

Ishi kulingana na asili, kazi ya falsafa ni kuwa na maisha bora.

Kuwa mwanafalsafa siyo sifa wala maonesho, badala yake kuishi kulingana na misingi.

Ukweli hauwezi kuhodhiwa, yeyote anayetafuta ukweli ataupata.

Mahitaji ya msingi ya maisha ni rahisi kila mtu kuyapata, ni anasa ndiyo zinafanya maisha yetu kuwa magumu.

Kila kitu kinategemea maoni, vile mtu alivyo ni jinsi anavyojiona yupo, maisha yako ni matokeo ya maoni uliyonayo juu yako.

Siyo kwamba hatuna muda, bali tuna muda mwingi mpaka tunaupoteza ndiyo maana tunakosa muda wa kufanya yale muhimu.

seneca_quote

EPICTETUS.

Epictetus ni mwanafalsafa mwingine wa Ustoa ambaye alichangia sana falsafa hii kukua. Epictetus alikuwa mtumwa wa mtumwa, wakati wa Roma watu walikuwa wanamiliki watumwa, na watumwa hawakuwa na haki yoyote kama watu, bali walimilikiwa kama vitu.

Licha ya kuwa mtumwa, pia Epictetus aliumia mguu na hivyo kuwa kilema, hivyo hakuwa na nafasi yoyote ya kuweza kuwa na maisha bora, ni kama dunia ilikuwa imeshamtenga na maisha mazuri.

Lakini kupitia falsafa ya ustoa, Epictetus aliweza kujifunza na kuwa mmoja wa wanafalsafa bora na wenye maisha mazuri.

Kwa kuwa alikuwa mtumwa, mchana alijifunza falsafa na usiku kufanya kazi, mpaka pale alipoweza kununua uhuru wake. Kwa kuishi misingi ya Ustoa, Epictetus aliweza kushinda utumwa na kushinda kilema cha mwili na kuweza kuwa na maisha bora.

Kwenye mafundisho yake Epictetus alikuwa akisisitiza sana kwamba kitu pekee ambacho mtu ana uhuru nacho, na hakuna anayeweza kukichukua kwa mtu ni uwezo wa kufikiri. Akisema kwamba kama kila mtu atatumia vizuri uwezo wake wa kufikiri, basi hakuna anayeweza kutawaliwa na mtu yeyote au kuzuiwa na mazingira yoyote magumu.

Epictetus alipenda kufundisha ila hakuwa mtu wa kuandika, hivyo kazi zake zilizoweza kusalia mpaka sasa ni zile ambazo wanafunzi wake waliandika kutokana na mafundisho yake.

Baadhi ya misingi ambayo Epictetus alifundisha na kuishi ni kama ifuatavyo;

Kinachotufanya sisi binadamu kuwa tofauti na viumbe wengine wote ni uwezo watu wa kufikiri na kufanya maamuzi.

Kama furaha na uhuru wako unategemea vitu vya nje, mara zote utakuwa mtumwa wa wale wanaoweza kukupa au kukunyima kile unachotegemea.

Mstoa ni yule ambaye; anaumwa na ana furaha, yupo kwenye hatari na ana furaha, anakufa na ana furaha, amefungwa na ana furaha, yupo kwenye matatizo na ana furaha. Kwa mstoa furaha haina uhusiano wowote na kinachoendelea kwenye maisha ya mtu, furaha ni matokeo ya fikra ambazo zimetulia na kufuata misingi ya falsafa. Hivyo hata kama mstoa anajua anakufa, bado anakuwa na furaha kwa zile dakika ambazo bado yupo hai.

Kinachomfanya mtu kuwa mzuri ni kuwa wa haki, kuwa na kiasi na kuwa mvumilivu.

Kama mtu hana furaha, ni kwa sababu ya matatizo yake mwenyewe, na hakuna yeyote anayehusika na kukosa kwake furaha.

Maisha ni sanaa ya kuishi, kila unavyoishi ndivyo unavyojifunza kuishi vizuri zaidi.

Kila ambacho kimekuja hapa duniani, kitaondoka pia, hakuna chochote kinachodumu, kwa kujua hili, hupaswi kung’ang’ana na chochote wala kuogopa chochote.

Watu hawasumbuliwi na kitu, bali wanasumbuliwa na mtazamo au fikra walizonazo juu ya kitu hicho. Kwa mfano kifo hakimtishi yeyote, kwa sababu kila mtu atakufa, ni vile mtu anavyotafakari kifo ndiyo kunamtisha.

circumstances-epictetus-quotes

MARCUS AURELIUS.

Kwenye Ustoa wa Roma, mmoja wa wanafalsafa bora kabisa wa Ustoa alikuwa Marcus Aurelius, kitu kimoja kuhusu Marcus ni kwamba licha ya kuwa mwanafalsafa wa ustoa, pia alikuwa mfalme wa Roma.

Marcus alikuwa mtu mwenye nguvu sana kama mtawala wa Roma, na anahesabiwa kama mmoja wa watawala bora kabisa wa Roma. wakati wa utawala wake, aliishi falsafa ya ustoa na hii ilimwezesha kuweza kutawala vizuri kwa kipindi chote cha utawala wake.

Licha ya kuwa mfalme na kuwa na nguvu ya kuwalazimisha watu wafanye chochote, hakuwahi kuwalazimisha watu wawe wastoa, wala hakuwahi kuwaambia watu yeye ni mstoa.

Kazi moja ya ustoa ambayo imemwezesha Marcus kuchukuliwa kama Mstoa aliyekuwa na ushawishi ni andiko lake la Meditations. Hili ni andiko ambalo yeye Marcus alikuwa akindika kila siku, akielezea siku yake ilivyokuwa, aliyojifunza na jinsi ya kuwa bora zaidi.

Hakuandika andiko hili kwa kusudi la kuwa kitabu, ila ilikuwa kwa matumizi yake binafsi. Andiko hili lilikuja kujulikana baadaye sana baada ya kifo chake, na limekua andiko ambalo limeyafanya maisha ya wengi kuwa bora sana. Ni moja ya maandiko yenye nguvu sana, ambalo limebadili maisha ya wengi.

Baadhi ya misingi ambayo Marcus alifundisha na kuishi ni hii;

Kila unapoianza siku jiambie leo naenda kukutana na watu wasumbufu, wajinga, wasio na shukrani, wakorofi na wasiojali. Na yote hayo ni matokeo ya watu kutokujua tofauti ya ubaya na uzuri. Ukianza siku yako kwa fikra hii, hakuna anayeweza kuiharibu siku yako.

Sisi binadamu tumeumwa kushirikiana, kama miguu ilivyo miwili, macho yalivyo mawili, mikono ilivyo miwili. Hivyo kufanya jambo lolote baya kwa mwingine ni kwenda kinyume na asili.

Maisha ya mwanadamu ni kitu kinachobadilika kila wakati, na msingi pekee ni kuishi falsafa.

Ondoa dhana kwamba “nimeumizwa” na hakuna atakayeweza kukuumiza.

Mtu mwema ni yule anayefanya jambo sahihi, na kuendelea kufanya jambo jingine sahihi badala ya kutangaza kwamba amefanya jambo zuri. Kama ambavyo nyuki hawatangazi wametengeneza asali tamu, tunapaswa kufanya wema siyo kwa ajili ya kuonekana au kujitangaza, bali kwa sababu ndiyo maisha tuliyochagua kuishi.

Kama mtu anaweza kunishawishi na kunionesha kwamba nimekosea, nitafurahi na kuwa tayari kubadilika. Ukweli haujawahi kumuumiza yeyote, bali ujinga na kung’ang’ana na mazoea kumeumiza wengi.

Pale unapoona wengine wanakosea, wape maelekezo sahihi, na kama huwezi kuwapa maelekezo sahihi, basi kaa kimya.

Quotation-Marcus-Aurelius

  1. MISINGI MIKUU MINNE AMBAYO FALSAFA YA USTOA INASIMAMIA.

Falsafa ya ustoa imekuwa inaongozwa na misingi mikuu minne ya kifalsafa ambayo ni kama ifuatavyo;

MOJA; HEKIMA.

Kama ilivyo kwa falsafa nyingine, lengo kuu la falsafa ya ustoa ni watu kuwa na hekima, inayowawezesha kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yao.

Hivyo kwa kuwa mwanafalsafa wa ustoa, unahitaji kupenda hekima, kupenda kujifunza na kujua zaidi kuhusu asili, akili na maadili.

MBILI; UTHUBUTU.

Falsafa ya ustoa inatutaka tuwe na uthubutu wa kuishi misingi ya falsafa hii na kusimamia ukweli hata kama tupo kwenye hatari. Wanafafalsa wengi wa ustoa walifukuzwa kwenye nchi zao na wengine kuuawa au kulazimishwa kujiua pale walipokataa kukubaliana na tawala ambazo zilikuwa na udhalimu.

Kwa mfano mwanafalsafa Cato aliamua kujiua kuliko kukubaliana na utawala dhalimu wa Julius Caesar.

Unahitaji uthubutu kuwa sahihi wakati ambapo wengi hawapo sahihi. Unahitaji uthubutu kuishi misingi ya falsafa ya ustoa wakati wengine wanaishi kwa mazoea. Kwa sababu utaonekana wa ajabu na wa tofauti.

TATU; HAKI.

Bila ya haki, maisha hayawezi kwenda vizuri hapa duniani. Falsafa ya ustoa inatutaka tufanye yale ambayo ni sahihi na mema kwa wengine, kwa sababu hiyo ndiyo maana ya kuwa binadamu.

Unapofanya jambo lolote ambalo siyo haki kwa wengine, unakua umechagua kuacha kuwa binadamu. Kila mtu akiishi kwa asili ya watu tunavyopaswa kuishi, maisha yatakuwa bora sana.

NNE; UVUMILIVU NA KIASI.

Kila kitu kwenye maisha kinataka kiasi, kukosa kiasi ni moja ya mateso ambayo watu tumekuwa tunajitafutia sisi wenyewe.

Wastoa wanasema, mahitaji ya msingi kabisa ya maisha ni rahisi sana kupata, chakula, malazi na mavazi, lakini pale tunapotaka vitu hivyo viwe anasa, viwe kwa ajili ya kuonekana na siyo kwa ajili ya kuishi, hapo ndipo maisha yanapokuwa magumu.

Kwa mfano unapovaa nguo kwa ajili ya kusitiri mwili, hutajali sana nguo gani unavaa. Lakini unapovaa nguo kwa ajili ya kuonekana na wengine, hapo ndipo unapoanza kujitesa, unafikiria uvae nguo ipi, au kuingia gharama kununua nguo ambazo huhitaji ili tu na wewe uonekane una nguo hizo.

  1. MFUMO WA MAISHA KWA WANAFALSAFA WA USTOA, AMBAO UNAKUANDAA KUKABILIANA NA MAGUMU YA MAISHA.

Lengo kuu la falsafa ya ustoa ni kuweza kukabiliana na ugumu wa maisha, kuweza kuwa na furaha hata kama kuna mambo magumu kiasi gani yanaendelea kwenye maisha yetu. Na pia kuhakikisha hisia haziwi kikwazo kwetu kuishi maisha tunayoyataka.

Kwenye falsafa ya ustoa, ipo misingi na mazoezi ambayo ukiyafanya, yanakusaidia kuwa imara bila ya kujali unapitia magumu kiasi gani.

Kwa kuijua na kuiishi misingi ya ustoa, wakati wote utakuwa na furaha na maisha yako yatakuwa bora iwe una fedha au huna, una watu wanakubaliana na wewe au la.

Yafuatayo ni mazoezi manne ambayo kwa kuyaishi yanakupa mfumo bora wa maisha ya ustoa.

MOJA; KUJENGA TASWIRA HASI.

Kila kitu ambacho tunacho kwenye maisha yetu, kina mwisho wake. Hakuna chochote kinachodumu, hata sisi wenyewe. Lakini tumekuwa tunajidanganya kwamba kila kitu kinapaswa kuendelea kuwepo milele. Na ndiyo maana tunapopoteza vitu, tunaumia, tunalia na kulalamika, tukisema kwa nini mimi.

Kwenye ustoa, lipo zoezi la kutufanya tusiumie pale tunapopoteza chochote. Zoezi hili ni kujenga taswira hasi.

Kila siku, jipe muda wa kufikiria kwamba kile kitu au watu unaowapenda sana kwenye maisha yako, wameondoka na hutawaona tena. Kama unapenda kazi au biashara yako, pata taswira kwamba huna tena kazi au biashara yako. Kama unawapenda wazazi au watoto wako, pata taswira umeamka na kupata taarifa wamekufa. Kadhalika kwenye mali zako na vitu vingine.

Zoezi hili halikufanyi utake vitu hivyo vitokee, bali linakuandaa kwa mambo mawili;

Kwanza linakuandaa kujua kwamba mambo hayo yanaweza kutokea, hivyo yanapotokea haiwi mshangazo kwako, kwa sababu ulijua itatokea na hivyo unakuwa na maandalizi.

Pili zoezi hili linakufanya uvipe vitu thamani yake. Kama ukiamka na kufikiria kwamba wale unaowapenda wamekufa, kwa kuwaona tena inakufanya uwajali, kwa kujua huenda muda ulionao leo ndiyo muda wa mwisho kuwaona. Hivyo una nafasi ya kuwaambia kiasi gani unawapenda, kiasi gani unawajali.

Binadamu tumekuwa na unafiki mkubwa pale ambapo hatuishi falsafa hii. Mtu akiwa hai hatumwambii namna gani tunampenda wala tunajali, lakini akishakufa ndiyo sifa zinakuja kemkem. Ukiishi falsafa ya ustoa, na kupata taswira kwamba chochote unachopenda kinaweza kupotea muda wowote, utakijali na kukipenda.

Seneca alikuwa akifanya zoezi hili kwa uhalisia zaidi, kwa kuigiza kama amekosa kile alichozoea. Kwa mfano aliweza kuchagua kulala chini hata kama ana kitanda, kutembea peku hata kama ana viatu na kukaa na njaa na kiu hata kama ana chakula. Yote hiyo ilikuwa kumwandaa na mazingira yanayoweza kujitokeza na akakosa hivyo alivyozoea.

MBILI; AINA TATU ZA UDHIBITI.

Kosa jingine kubwa ambalo tumekuwa tunafanya kwenye maisha, ni kuhangaika na mambo ambayo yapo nje ya uwezo wetu kwenye kuyadhibiti. Tunahangaika na mambo ambayo hatuwezi kuyabadili, yanatupotezea muda na nguvu na kushindwa kuhangaika na yale yaliyopo ndani ya uwezo wetu.

Falsafa ya ustoa inatufundisha kwamba, mambo yote yanayotokea kwenye maisha yetu yamegawanyika kwenye makundi matatu;

Kundi la kwanza ni yale mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu kuyathibiti na kuyabadili. Na mambo hayo ni mawazo yetu, hisia zetu, maamuzi yetu na mtazamo tulionao juu yetu na wengine pia.

Kundi la pili ni mambo ambayo tunaweza kuyaathiri kwa kiasi, tunaweza kuyabadili kwa kiasi fulani ila hayapo ndani ya uwezo wetu kabisa. Na mambo hayo ni kama kazi na biashara tunazofanya, tabia za wengine na mafanikio kwenye jambo lolote kimaisha.

Kundi la tatu ni mambo ambayo yapo kabisa nje ya uwezo wetu, mambo ambayo hatuwezi kuyaathiri au kuyabadili kwa namna yoyote ile. Mambo haya ni kama hali ya hewa, maamuzi ya wengine, asili ya dunia.

Msingi wafalsafa ya ustoa kwenye udhibiti ni hii; kwenye kila jambo unalokutana nalo kwenye maisha, lina jawabu au halina jawabu, kama lina jawabu tafuta jawabu hilo, na kama halina jawabu achana nalo.

Njia nyingine ya kueleza msingi huu ni kwa jambo lolote linalotokea kwenye maisha yako, jiulize kama lipo ndani ya uwezo wako, kama ndiyo litatua, na kama lipo nje ya uwezo wako achana nalo na songa mbele.

Kujisumbua na jambo ambalo huwezi kuliathiri, hata kulifikiria tu ni kupoteza muda wako.

TATU; NJIA TATU ZA KUKABILIANA NA UKOSOAJI WA WENGINE.

Watu watakukosoa kwa chochote utakachofanya, iwe ni kizuri au kibaya, sahihi au siyo sahihi. Huwa hatupendi kukosolewa, hivyo watu wanapotukosoa huwa tunapata hisia ambazo matokeo yake huwa siyo mazuri. Labda huwa ni kukata tamaa au kuwachukia watu hao.

Zipo njia tatu za kukabiliana vizuri kifalsafa na wanaokukosoa;

Njia ya kwanza; kujidharaulisha zaidi. Kama mtu amekukosoa kwa jambo fulani ulilofanya, unaweza kumwambia hicho anachokosoa ni kidogo sana, kama angejua makubwa zaidi unayofanya, basi anachokosoa sasa kisingekuwa na maana. Hii inamfanya mtu akose sababu ya kuendelea kukukosoa.

Njia ya pili; kupuuza, hapa unachukulia kama hujasikia au hujaelewa kile ambacho mtu amekosoa, unaendelea na mambo yako kama vile mtu hajasema chochote, hii pia inamkosesha mtu nguvu ya kuendelea kukosoa.

Tatu; kuchukulia kama unamwelekeza mtoto. Kuna watu ambao ni wasumbufu kwenye maisha, na hiyo ni kwa sababu kuna vitu walikosa walipokuwa watoto hivyo wanakuwa wakiwa na mitazamo fulani ambayo siyo mizuri kwao. Unapokutana na watu wa aina hii kwenye maisha, chukulia kama unamwelekeza mtoto, na hivyo unakuwa mvumilivu.

NNE; TAHAJUDI YA JIONI.

Zoezi la nne la kistoa tunaloweza kufanya na likafanya maisha yetu kuwa bora ni kufanya tahajudi ya JIONI. Kila siku jioni, kabla ya kulala, tenga muda na kaa sehemu tulivu, funga macho na pitia siku yako nzima, tangu ulipoamka mpaka hapo ulipofikia unataka kulala. Ona kila ulichokifanya, ona kila uliyeongea na kuwasiliana naye. Kisha jiulize yapi umefanya sahihi na yapi umekosea. Kwa yale uliyofanya sahihi unayaendeleza, kwa yale uliyokosea unayarekebisha.

Unaweza kufanya zoezi hili kwa kuwa na kijitabu ambacho unaandika kila siku, kama alivyokuwa anaandika mwanafalsafa Marcus Aurelius.

Ukifanya zoezi hili, kila siku, utakuwa na kitu cha kurekebisha kwenye maisha yako na kazi zako na kila siku utazidi kuwa bora kabisa.

  1. JINSI UNAVYOWEZA KUITUMIA FALSAFA YA USTOA KWENYE MAISHA YA KILA SIKU.

Falsafa ya ustoa ni falsafa ya vitendo (PRACTICAL PHILOSOPHY), siyo falsafa ya kubishana kipi sahihi na kipi siyo sahihi, bali ni falsafa ya kuishi maisha sahihi na yanayoendana na asili.

Epictetus anatuambia usibishane mtu sahihi anapaswa kuishije, bali kuwa mtu huyo.

Na Marcus Aurelius anatuambia Kama kitu siyo kweli usiseme, kama siyo sahihi usifanye.

Seneca anakazia zaidi na kusema usijitangaze kuwa mwanafalsafa, bali ishi maisha ambayo watu wakikuangalia wanasema mtu huyu ni mwanafalsafa, mtu huyu anafanya kilicho sahihi.

Jumbe hizi tofauti kutoka kwa wanafalsafa tofauti wa ustoa zote zinatupeleka eneo moja; TUNAPASWA KUCHAGUA KUISHI FALSAFA HII KWENYE MAISHA YETU YA KILA SIKU.

Hivyo anza kuishi falsafa hii, anza kujifunza, anza kuchagua misingi sahihi unayoishi kila siku na ishi misingi hiyo.

Jua yale ambayo yapo ndani ya uwezo wako kuyakabili, na jua yaliyo nje ya uwezo wako na achana nayo.

Mwisho kabisa, kwa kuwa tupo kwenye KISIMA CHA MAARIFA, msingi wetu wa maisha ya mafanikio, NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA, ni msingi ambao umebeba vizuri falsafa ya ustoa.

Hivyo anza kuishi falsafa ya ustoa sasa, endelea kujifunza na fanya mazoezi muhimu ya falsafa hii. Kwa kuwa mstoa, kila wakati una sababu ya kuwa na furaha, kwa sababu unajua wakati ulionao sasa hautajirudia tena. Hivyo kazana kuishi kwenye kila wakati unaoupata.

  1. MJADALA, SHUHUDA, MASWALI NA MAJIBU.

Darasa letu limekuwa refu kidogo kutokana na umuhimu wa falsafa hii na kuwepo kwa mengi ya kujifunza, hata hivyo haya tuliyojifunza ni ule utangulizi muhimu, ambao unabeba yale muhimu. Tutaendelea kujifunza kwa undani zaidi kuhusu falsafa hii kadiri tunavyokwenda.

Karibuni sasa kwa shuhuda, maswali na hata majibu kuhusu falsafa hii.

Wapo wenzetu wengi ambao wamekuwa wanaishi falsafa hii, karibuni mtushirikishe jinsi imefanya maisha yenu kuwa bora.

Pia kwa wale ambao mna maswali au kutaka ufafanuzi zaidi kuhusu falsafa hii, karibuni sana.

SWALI; Richard Kaganda: Mi naomba kujua wanafalsafa wote ni watu waliokuwa ni wana mahesabu au wanasayansi ?

JIBU; KOCHA; Falsafa kipindi cha nyuma, kabla ya mapinduzi ya sayansi yaliyotokea kwenye karne ya 15, walikuwa wanaweka kila kitu ndani ya siasa.

Kwa mfao ukiangalia ustoa, utaona sayansi ipo ndani yake, imani ipo ndani yake na maadili yapo ndani yake.

Ni baada ya kukua kwa sayansi ndiyo kidogo imekuwa tofauti na falsafa, lakini zamani sayansi, hesabu na falsafa ilikuwa kitu kimoja.

Kwa mfano kama unajua ile kanuni maarufu ya hesabu, PYTHAGORAS THEOREM, iligunduliwa na mwanafalsafa Pythagoras, ambaye alikuwa na shule yake ya falsafa kabisa.

SWALI; Jilala Joseph: Mimi nataka Ufafanuzi kuhusu Dini ni falsafa sijaelewa Kocha

JIBU; KOCHA; Nimesema dini karibu zote zinaendeshwa kwa misingi fulani ya falsafa. Lakini siyo kila falsafa ni dini.

Kila dini ina misingi yake, na misimamo yako, hiyo ndiyo falsafa iliyopo kwenye dini.

JIBU; Deo Kessy: Habari jilala, kama ulikuwa umesoma vizuri kwenye utangulizi basi, dini zote ni mfumo wa falsafa lakini siyo falsafa zote ni dini. Dini tulizonazo zimejengwa katika mfumo fulani wa kifalsafa ambao unawaongoza au kuwawezesha watu kuweza kuwa na maisha bora hapa duniani na hata baada ya kuondoka hapa duniani yaani kabla na baada. Asante sana

Hillary Mrosso: Swali, Hii falsafa ya Ustoa haina mwanamke ambaye naye aliishi au kujifunza?

JIBU; KOCHA; Moja ya changamoto na mapungufu ya falsafa nyingi ambayo watu wamekuwa wanatoa ni maeneo mawili;

Moja; wanawake

Mbil; watumwa.

Kipindi cha zamani wanawake hawakuwa wanapata nafasi kubwa kwenye jamii. Na pia swala la kumiliki watu kama watumwa lilikuwa la kawaida.

Lakini falsafa ya ustoa iliweza kupambana na hilo, kwa sababu haikuwa na ubaguzi wa nani anaweza kujifunza.

Ndiyo maana Epictetus pamoja na kuwa mtumwa, aliweza kuwa mwanafalsafa wa Ustoa.

Sasa kwa upande wa wanawake, hakuna kazi za wanafalsafa wa kale wa ustoa ambao walikuwa wanawake, lakini mwandishi wa falsafa wa zama hizi Ryan Holiday anasema kuna watu wengi sana waliishi ustoa enzi hizo, lakini hawakuandika wala kufundisha, na maisha yao yalikuwa bora sana. Hivyo walikuwepo wanawake walioishi falsafa hii.

Pia Seneca kwenye barua zake, zipo barua ameandika kwa mama yake akimsaidia kuondokana na majonzi kwa kuishi falsafa.

Hata kazi ya kumfundisha Nero ambayo Seneca alipewa, alipewa na Agripina, mama yake Nero.

SWALI; Felix Rumisha: Binafsi bila najiona naiishi falsafa hi kwa sehemu kubwa… Swali langu ni je kuna wastoa wa zama hizi au tunapokea mabadiliko tu bila kujijua?

JIBU; Deo Kessy: Wastoa wa zama hizi wapo mmojawapo ni wewe mwenyewe unayeiishi. Falsafa hii hutakiwi kujitangaza ila kama ni mstoa utakua unajua tu mtu fulani maisha yake anayaendesha kwa misingi gani. Kwa mfano, Nelson Mandela alikuwa mstoa lakini hakuwahi kujitangaza. Watu wengi wanatumia mbinu za falsafa hii bila wao kujijua na hata kama mtu ni mstoa huruhusiwi kujitangaza ila watu wanajifunza kupitia matendo yako. Asante sana.

JIBU; KOCHA; Wapo wastoa wengi sana kwenye zama hizi.

Na kwa sababu ya changamoto kubwa za zama hizi, falsafa ya ustoa imepata umaarufu mkubwa kipindi hichi kuliko wakati mwingine wowote.

Wapo waandishi wa zama hizi ambao wanaishi sana falsafa hii,

Mfano;

Ryan Holiday, amabaye ameandika vitabu vinginna vizuri, kuhusu ustoa na hata strategy

Tim Ferris ambaye anajiita human guinea pig, anasema falsafa hii ndiyo imemuokoa, maana alifika mahali akataka kujiua.

Nasem Nicholaus Taleb, huyu ni mtu mbishi sana wa zama hizi, nitashare uchambuzi wa moja ya vitabu vyake wiki ijayo.

Wapo viongozi wengi ambao ni wafuasi wa falsafa hii. Inawawezesha kuishi na kuvuka changamoto za zama hizi.

SWALI; John Matiku: Asante sana Kocha kweli hili ni darasa adhimu sana, naomba msaada hasa pale kwenye kubadili ninavyoviweza na kuachana na nisivyoviweza msingi hasa tumeona ni kama jambo lina jawabu au halina Ustoa unasema nini kuhusu matumaini yasiyo na uhakika mfano unataka kubadili tabia flani ya mtu wako muhimu unaamini katika njia flani flani lakini huna hakika hata pale unapojaribu njia hizo zikaleta matokeo yenye matumaini bado mtu huyu anarudia tabia zile ambazo unaona zinampeleka/zinawapeleka kwenye maangamizo.

JIBU; KOCHA; Karibu John,

Kama nilivyoeleza, Falsafa hii inatupa hatua za kuchukua kwenye udhibiti.

Kama kitu kipo ndani ya uwezo wako na unaweza kukibadili, basi kibadili. Na vitu vya aina hii ni vile ambavyo vinakuhusu wewe tu.

Lakini kama kitu hakipo ndani ya uwezo wako yaani huwezi kuvibadili, basi inabidi uachane navyo, yaani visiendelee kukusumbua, hivyo unaweza kuvikubali kama vilivyo na ukasonga mbele.

Kwenye kuwabadili wengine, ipo ndani ya uwezo wetu kwa kiasi, tunaweza kuwashauri kipi bora kwao kufanya, tunaweza kuwaonesha kwa mfano kwa sisi wenyewe kufanya, lakini hatuwezi kuwalazimisha kufanya.

Hivyo kwa falsafa ya ustoa unahitaji kufanya sehemu yako, kisha kuwaachia wenyewe wachague wanafanya nini. Kama watafanya ulichowaelekeza ni sawa na kama hawatafanya pia kwako ni sawa, wewe umeshafanya sehemu yako, hivyo haipaswi kukusumbua tena.

USHUHUDA; Felix Rumisha: Kuna wakati huwa najishangaa sana… Mfano nikipata habari yoyote mbaya huwa sipati mshtuko.. Naona kawaida sana.. Au mtu akiniongelea vibaya au kunitukana mi naona kama kichekesho najikuta nacheka bila hasira. Au mtu akininenea mabaya namwambia hayo mbona kidogo tu mi nina makubwa zaidi ya hayo

SWALI; KELVIN ALOYCE KINYAGA: Nianze kwa kukushukuru kocha hakika nimejifunza mengi Sana na Sasa naweza Sema nitaendelea kutenge Muda Mara kwa Mara kujifunza falsafa hii na naona kuwa kisima cha maarifa tu tayari safari ya kuishi falsafa hii inaanza. SWALI Umezungumzia kuhusu udhibiti na Aina Tatu umezitaja Kuna moja ni kuyakubali mambo yaliyo nje ya uwezo wetu kama maamuzi ya wengine hii ina maana kwakuwa hatuwezi kuyabadilisha basi tuyakubali je ukimtoa Seneca ambaye alilazimishwa alitakiwa kuuwawa japo kwa njia ngumu pengine kutufundisha kuwa haogopi kifo je hao waliojiua kwa sababu ya kutokubaliana na viongozi dhalimu walikuwa kinyume na ustoa? Au nini tunajifunza kwao?

JIBU; Deo Kessy: Falsafa ya ustoa ni falsafa ambayo inahitaji uthubutu, huyo aliyejiua aliamua kujiua kwa sababu falsafa ya ustoa inakutaka kusimamia ukweli, hivyo MTU anaona ni bora kufa kuliko kukubali kitu ambayo hakipo katika msingi wa ukweli ambao ana unasimamia.

Kwa mfano, Thomas more alikuwa katika utawala wa Uingereza na mwenzake fish walikubali kufa kuliko kupotosha ukweli. Unasimamia ukweli hata ukiambiwa kufa uko tayari kutetea ukweli. Asante sana

SWALI; KELVIN ALOYCE KINYAGA: Asante Sana, je niko sahihi kuwaza kuwa lengo la Seneca kuchagua kifo cha kujikatili mwenyewe ni funzo la kuwa hatupaswi kuogopa chochote au Kuna lingine?

JIBU; KOCHA; Kipindi cha zamani, tawala zilikuwa ni za kutumia nguvu kubwa na mabavu.

Na wanafalsafa walikuwa ni watu ambao walikuwa wanawafundisha watu jinsi ya kuwa huru, kufikiri na hata kuhoji.

Hivyo karibu kwenye kila utawala, wanafalsafa walikuwa maadui wa utawala.

Ndiyo maana wengi walifungwa, walifukuzwa nchini kwao (exile) na hata wengine kuuawa.

Mfano Socrates, aliuawa kwa sababu alishutumiwa kuwaharibu vijana, kwa kuwafundisha kuwa kinyume na utawala.

Utaona hilo kwa Yesu pia, aliuawa kwa sababu alifundisha watu kiwa huru na kutofungwa na tawala zilizopo.

Seneca alifukuzwa nchi, na baadaye kuja kulazimishwa kujiua.

Epictetus alifukuzwa nchi na sehemu kubwa ya maisha yake alikuwa uhamishoni.

Cato alijiua ili tu kuondokana na manyanyaso ya utawala wa Caesar,

Wapo wanafalsafa wengi, wa ustoa na hata falsafa nyingine ambao walisumbuliwa sana na watawala.

Angalau zama tunazoishi sasa, ni zama salama sana kuwa mwanafalsafa, hasa pale unapoishi misingi ya kifalsafa na kuacha wengine wahangaike na mambo yao.

SWALI; Peter Michael Hhera: Asante sana Kocha Amani ,nimejifunza na kuchukua mengi.Na swali nayo ni Uamuzi aliouchukua mstoa Seneca wa kujiua siyo ishara ya kukata tamaa juu ya falsafa .

JIBU; KOCHA; Karibu Peter,

Hili ulilouliza ni moja ya mambo ambayo watu wamekuwa wanasema kama mapungufu ya falsafa hii, kwamba watu wanayakimbia matatizo badala ya kuyakabili, kwa kujiua.

Lakini kwa jinsi falsafa hii ilivyo, kama kitu huwezi kukibadili, basi usikubali kikusumbue.

Kwa mfano Seneca alihukumiwa kifo, lakini hakutaka mtu mwingine amuue, aliomba ayatoe maisha yake mwenyewe, kama ishara ya kuishi falsafa aliyodumu nayo maisha yake yote.

Hakuna namna angeweza kubadili adhabu yake ya kifo, hivyo aliamua kuichukua nafasi hiyo kutimiza falsafa ya ustoa.

USHUHUDA; Lawrence Leon: Asante sana kocha na wanamafanikio wote kwa nafasi na elimu hii adimu. Binafsi naipenda na najifunza kuishi falsafa hasa ustoa. Nimeona mengi ambayo ni tofauti na mtazamo wa jamii. Mfano unaweza kukuta ndugu wawili wakigombana juu ya kitu kidogo hususan Mali kama mashamba. Hapo ndipo napo ona thamani ya falsafa kwa jinsi ambavyo tungeweza kuepuka vitu kama hivi kama tungekuwa na uelewa hata kidogo juu ya ustoa. Lakini zaidi ni amani ya ndani na uwezo wa kutatua changamoto za kawaida bila kuathiri maisha ya wengine vibaya.

Nimeona wazi kwamba kwenye jamii yetu hasa kwenye ofisi nyingi za umma kama unaishi ustoa jiandae kukubaliana na matokeo kwa kuwa Mara nyingi utaonekana hufai kuwa kwenye system sababu system Mara nyingi zinahitaji uwe mnafiki na mwongo kiasi Fulani, ukiona ubaya usiseme, ukiona dhuluma useme hujaona lolote na mengine mengi. Jiandae kusukumwa pembezoni endapo umeamua kuwa mstoa.

KOCHA; Asante sana Leon.

Ni kweli kabisa, kuishi Ustoa kunatuepusha na mengi, lakini pia kunatufanya tuhukumiwe na kuonekana wa ajabu.

Lakini hilo halipaswi kutufanya sisi tuache falsafa hii.

Kwa sababu mwisho wa siku, hata wale wanaokusema hufai, kuna shida fulani wakipata wanakuja kwako, kwa sababu wanajua wewe pekee ndiye unayeweza kuwasaidia kuitatua, kwa sababu kuna misingi unaiishi.

Watu wengi wangependa sana kuishi misingi fulani ya kifalsafa, lakini hawana uthubutu, hivyo watamsema anayeiishi, lakini wakiwa na shida, wataenda kwa yule wanayemsema.

Mstoa wa zama zetu anatuambia “If you see fraud and do not say fraud, you are a fraud.” — Nassim Nicholas Taleb

USHUHUDA; Tumain Jonas: Asante sana kocha Dr. Makirita Amani kwa darasa zuri kabisa na muhimu la leo. Hakika falsafa ya ustoa ni falsafa bora kabisa ya kila mtu kuweza kuishi na haitofautiani sana dini zetu. Binafsi nimekuwa naiishi kwa sehemu tangu nilipojiunga na Kisima cha Maarifa. Nimeona mabadiliko mengi sana kwenye maisha yangu ya kila siku.

Wakati tunaanza darasa hili la leo, nilikuwa kwa rafiki yangu ambaye alifiwa na mtu wake wa karibu ili kumpa pole lakini cha ajabu alianza kupoteza ile furaha tena na kuanza kulia. Hapo nikajisemea moyoni kweli falsafa ya ustoa inahitajika kwa wengi ili kuwawezesha kuwa na maisha bora na furaha. Asante sana kocha Dr Makirita Amani kwa elimu hii ya falsafa ya ustoa na nitaendelea kuiishi falsafa hii kila siku ya maisha yangu.

KOCHA: Maana halisi ya UTHUBUTU kwenye ustoa ni kwamba hakuna la kuogopa.

Mfano kwenye Meditations, Marcus anaandika;

Book 8.5: This is the chief thing: do not be disturbed. All things are in accordance with the nature of the universe, and in a little while you will be nobody and nowhere, like Hadrianus and Augustus. Next, focus steadily on your work and at the same time remember that it is your duty to be a good man. Do what Nature demands without turning aside. Speak as it seems to you most just, but with an even disposition and with modesty and without hypocrisy.

HITIMISHO;

Asanteni sana wanamafanikio.

Baada ya darasa hili, sasa sisi wote ni WANAMAFANIKIO, WANAFALSAFA WA USTOA.

Tuendelee kuishi falsafa hii, tuendelee kujifunza zaidi.

Tutaendelea kushirikishana hapa kila siku.

Nakazana sana TAFAKARI zetu za asubuhi ziwe za kifalsafa, ili kila siku tukumbuke na kuishi misingi yetu.

Nitaweka vitabu vya falsafa hii pia.

MAKALA ZA USTOA; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/?s=ustoa

MAKALA ZA USTOA; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/category/falsafa-na-imani/falsafa-ya-ustoa/

Link hizo zina makala zaidi kuhusu falsafa ya ustoa ambazo zipo kwenye KISIMA CHA MAARIFA, tuendelee kusoma zaidi.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

KARIBU UJIUNGE NA KISIMA CHA MAARIFA.

KISIMA CHA MAARIFA ni blog maalumu ya mafunzo na hamasa kwa ajili ya kufikia mafanikio makubwa. Blogu hii inaambatana na kundi maalumu la wasap ambapo unapata mafunzo mbalimbali kila siku kwa kuwa ndani ya kundi hilo.

Hivyo unapojiunga na KISIMA CHA MAARIFA, unapata nafasi ya kusoma makala kwenye blog, makala za maisha, mafanikio, biashara, uwekezaji, falsafa na kadhalika. Makala hizi huwezi kuzipata sehemu yoyote ile duniani ila tu kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

Ndani ya kundi la wasap la KISIMA CHA MAARIFA, kila siku utaianza na TAFAKARI yenye funzo na hamasa kubwa ya kukusukuma siku hiyo kuchukua hatua. Kila jioni utajifunza kupitia wengine na yale waliyojifunza. Kila wiki utapata nafasi ya kushiriki darasa linalohusu maisha na mafanikio. Pia kila mwaka kuna semina mbili zinazoendeshwa kwa njia ya mtandao kupitia kundi la wasap na semina moja ya kukutana ana kwa ana.

Pia kwa kuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, kila mwezi unapata maswali ya kujifanyia tathmini yatakayokufanya uone pale ulipo sasa, kule ulikotoka na hata unapokwenda. Maswali haya yatakufanya uone wapi unakosea na wapi unapatia, pia hatua zipi za kuchukua ili uweze kufika pale unapotaka kufika.

Yote hayo unayapata kwa kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, ambapo unalipa ada ya shilingi 50,000/= (elfu 50 pekee). Hiyo ni ada ya mwaka, ambapo ukilipa utalipa tena baada ya mwaka kuisha tangu ulipolipa. Ukishalipa ada hiyo unapata mafunzo yote hayo bila ya gharama za ziada, isipokuwa tu semina ya kukutana ana kwa ana ndiyo unalipia malipo ya ziada.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, lipa ada, tsh 50,000/= kwa namba zifuatazo; MPESA – 0755 953 887, TIGO PESA/AIRTEL MONEY – 0717 396 253, majina kwenye namba hizo ni AMANI MAKIRITA. Ukishatuma ada, tuma ujumbe wenye majina yako kamili, namba ya simu pamoja na email kwa ujumbe wa wasap kwenda namba 0717396253 kisha utaunganishwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

Kama upo hapa duniani, na upo makini na maisha na mafanikio yako, basi kuna sehemu moja ambayo unapaswa kuwa, nayo ni KISIMA CHA MAARIFA. Ninakuambia hili nikimaanisha, kwa sababu najua ukiwa ndani ya KISIMA CHA MAARIFA, hutabaki hapo ulipo sasa, nakuhakikishia hilo, lazima utajikuta unasonga mbele zaidi, hata kama unaona umekwama kiasi gani.

Karibu sana kwenye KISIMA CHA MAARIFA, karibu sana tuwe pamoja, tujifunze na kuhamasika kila siku, na kuweza kuyafikia mafanikio ambayo ni haki yetu ya kuzaliwa.