Rafiki yangu,

Juma namba 18 la mwaka huu 2018 siyo juma letu tena, juma limetuacha, lakini ni imani yangu kwamba juma hili halijatuacha kama tulivyokuwa kabla.

Kama ambavyo nimekuwa nakusisitiza, kila juma lipangilie, kila juma fanya kitu cha tofauti, na kila juma jifunze kitu ambacho kinayafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Ni katika msisitizo huu, kila mwisho wa juma nimekuwa nakuandalia tano za juma, ambapo nakushirikisha yale mambo matano muhimu niliyokutana nayo ambayo kwa kukushirikisha kuna mambo unayoweza kufanyia kazi na maisha yako yakawa bora zaidi.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Karibu kwenye tano za juma hili la 18, soma haya ninayokushirikisha, fanya maamuzi na chukua hatua.

#1 KITABU NILICHOSOMA; JINSI YA KUTOA KAZI INAYODUMU KWA VIZAZI.

Kila wiki huwa nasoma angalau vitabu viwili, lakini huwa najitahidi kwenda zaidi ya hapo, na kama muda unabana kabisa, basi ni lazima nisome hata kitabu kimoja.

Juma hili nimesoma vitabu viwili na moja ya vitabu hivyo ni kitabu PERENNIAL SELLER ambacho kimeandikwa na Ryan Holiday. Hichi ni kitabu ambacho kinaeleza mchakato mzima wa kutengeneza kazi ambayo itadumu vizazi na vizazi.

Nani ambaye hapendi biashara anayoanzisha idumu miaka 10, 50 na hata zaidi ya 100? Ni msanii gani anapenda akitoa wimbo upigwe wiki moja halafu upotee kabisa. Mwandishi gani ambaye hapendi kazi yake isomwe kwa miaka mingi hata baada ya kufa?

Ukweli ni kwamba tunapenda kazi zetu zidumu, lakini tunakosea sehemu moja, hatuweki kazi inayohitajika ili kazi hiyo iweze kudumu.

Kwenye kitabu cha PERENNIAL SELLER, Ryan anatupa mchakato mzima wa kufanya hivyo, ambao unahusisha hatua nne.

Hatua ya kwanza ni kuweka kazi kuja na kitu cha pekee kitu cha tofauti na kinachofanya maisha ya wengine kuwa bora kabisa. Unahitaji kuwa tofauti sana hapa, la sivyo hutafika mbali.

Hatua ya pili ni kukamilisha kazi yako ambayo umeifanya, hapa sasa unawaangalia wale ambao umewalenga kwa kazi yako, unawafikiaje na utawashawishije waweze kununua kazi yako.

Hatua ya tatu ni kutangaza na kusambaza kazi yako. Kwanza kazi yako inapaswa kuwa bora sana, pili unahitaji kuweka juhudi kubwa mno kuitangaza na kuisambaza, hasa kwa siku za mwanzoni. Baada ya hapo unahitaji kuwafanya watu waizungumzie muda wote.

Hatua ya nne ni kuwa na jukwaa, la watu ambao ni mashabiki wako wa kweli, ambao wapo tayari kufanya chochote kupata kazi zako. Jukwaa hili linatengenezwa, na unahitaji kuanza na mashabiki 1000 wa kweli kabisa, hao watayafanya maisha yako kuwa rahisi na kuwafikia wengine wengi.

Kwenye makala ya uchambuzi wa kitabu ya juma la 19 utaweza kusoma hatua hizo nne kwa undani, na hatua moja ya ziada ambayo sijaiweka hapo.

#2 MAKALA YA WIKI; FALSAFA BORA YA KUISHI MAISHA YAKO.

Maisha unayoishi sasa, ni ya kifalsafa, kama kwa kusikia hivi umestuka basi nina habari mbaya kwako, umekuwa unaishi falsafa ambayo hujiui na hicho ndivyo chanzo cha matatizo mengi kwenye maisha yako.

Wengi tunaposikia falsafa, huwa tunafikiria kukaa darasani na kuanza kubishana kipi sahihi na kipi siyo sahihi. Huo ni mtazamo potofu wa falsafa.

Falsafa ni mfumo wa maisha na maisha bora ni yale yanayoendeshwa kwa falsafa.

Ipo falsafa moja bora sana ya kuishi kwenye maisha yako, ambayo ukiielewa na kuiishi basi utakuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa.

Falsafa hiyo ni USTOA, falsafa yenye zaidi ya miaka 2500 lakini misingi yake ni muhimu sana kwenye maisha ya sasa.

Kwenye makala ya wiki kwenye AMKA MTANZANIA, nimekushirikisha mwanzo mwisho darasa la falsafa ya ustoa. Kama hutasoma chochote leo au hata wiki nzima ijayo, basi soma makala hii na ielewe kisha anza kuishi misingi ya ustoa, utakuja kunishukuru baadaye, kwa namna maisha yako yatakavyokuwa bora.

Unaweza kuisoma makala hiyo hapa; Darasa La Wiki; Falsafa Ya Ustoa Na Matumizi Yake Kwenye Zama Tunazoishi. (Au fungua link hii; https://amkamtanzania.com/2018/05/04/darasa-la-wiki-falsafa-ya-ustoa-na-matumizi-yake-kwenye-zama-tunazoishi-2/ )

#3 TUONGEE PESA; KAMARI UNAYOCHEZA NA HELA ZAKO.

Kipengele cha tatu kwenye TANO ZA JUMA nimekuwa nakushirikisha yale niliyojifunza au kukutana nayo. Na mara nyingi nimekuwa nakushirikisha yale ambayo nimeona yakitokea. Lakini siku hizi nimekuwa mbali sana na habari kiasi kwamba sijui vingi vinavyoendelea. Mfano wiki hii ningetamani kukushirikisha kuhusu sakata la wafanyakazi kutegemea waongezewe mshahara siku ya sherehe za wafanyakazi, lakini hawakuongezewa na wengi kulalamika. Nilitamani niseme maneno makali sana kwa wale ambao wanalalamikia kutokuongezewa mshahara, lakini sina taarifa za kutosha, maana sijafuatilia kabisa hilo, nasikia tu watu wakisema.

Kuanzia sasa, kipengele hichi cha tatu kitakua ni #TUONGEE PESA, kwa sababu naona watu wengi mno wanafanya makosa ya kifedha ambayo yapo wazi kabisa. Na bila kusahau, fedha ni muhimu, na sehemu kubwa ya changamoto zetu zinaanzia kwenye fedha.

Juma hili nataka nikuoneshe kamari unayocheza na fedha zako na uache kuicheza haraka sana.

Una fedha zako, labda umeweka akiba, au umestaafu kazi na ukalipwa mafao yako. Anakuja ndugu, jamaa au mtu wa karibu, anakuambia kuna fursa nzuri sana, inayotengeneza faida nzuri, hivyo umpe fedha, yeye akaifanyie kazi fursa hiyo halafu atakupa nusu ya faida, huku mtaji wako ukiwa salama.

Unafikiria, huyo ni ndugu yako, mtu mnayeheshimiana, hawezi kukutapeli, na amekupa mifano ya waliofanikiwa kwenye fursa hiyo. Basi unatoa fedha, unampa, akazungushe kwenye hiyo fursa, na wewe usubiri faida, huku mtaji wako ukiwa salama.

Nikuambie kwa herufi kubwa; UNACHEZA KAMARI, na ukipoteza fedha zako zote usimlaumu yeyote.

Kamwe usitoe fedha zako na kumpa mtu mwingine akazifanyie kazi kisha akupe faida, hata kama ni mwaminifu kiasi gani. Kila mahali ambapo unaweka fedha yako, hakikisha una usimamizi wa asilimia 100. Kama huwezi kuwa na usimamizi wa aina hiyo, nakushauri bora uweke fedha zako chini ya godoro na uzilalie, au uchague njia nyingine nzuri ya kuzipoteza. Kumpa mtu mwingine fedha zako afanyie kazi, huku wewe unasubiri faida, ni kamari. Labda kama unatoa kwenye taasisi ambayo unaendeshwa kisheria, ambapo kuna njia ya kupata kilicho chako, au unaweza kufuatilia kila kinachoendelea. Ila yale makubaliano ya kindugu, kirafiki au kijamaa, kaa mbali na fedha zako.

Najua hutaelewa hili, utafuatwa na fursa za kufirika utashawishika kweli, utasema lakini hii ni tofauti na aliyosema Kocha, utaweka fedha zako, na siku utakayopata matokeo ya kwamba mtaji wako umezama, utakumbuka hili vizuri na utakuwa umejifunza vyema.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; JAWABU LA CHANGAMOTO ZA KILA SIKU.

Kila siku mpya ya maisha yako ni siku inayokuja na changamoto zake. Watu wamekuwa wakifikiri maisha ni kukazana kutatua changamoto zote ili uzimalize. Lakini ukweli ni kwamba changamoto za maisha ni kama darasa, ukimaliza changamoto moja, inakuja nyingine kubwa zaidi.

Ili kuwa kwenye mtazamo sahihi wa kukabiliana na changamoto za kila siku, unahitaji kuianza siku yako kwa usahihi. Na njia bora ya kuianza siku yako ni kuwa na kitu chanya unachotafakari, ambacho kinaifanya akili yako kuwa imara na kuwa chanya.

Hichi ndiyo unachopata kwenye KUNDI LA WASAP LA KISIMA CHA MAARIFA, ambapo kila siku asubuhi unapata TAFAKARI nzuri ya kuianza siku yako. Tafakari hii inakuweka kwenye mtazamo sahihi wa kuweza kukabiliana na chochote kitakachotokea mbele yako.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, unakosa sana TAFAKARI hizi ambazo zinakufanya uwe bora kila siku. Jiunge sasa na utaianza kila siku ukiwa na silaha za kukabiliana na changamoto yoyote utakayokutana nayo.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma ujumbe wenye neno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717396253 na utapata maelekezo.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; MABADILIKO YANAVYOKUUA.

Cause change and lead;

Accept change and survive;

Resist change and die.

– Ray Norda

Ukisababisha mabadiliko, unakuwa kiongozi wa mabadiliko, unakuwa kwenye nafasi kubwa ya kufanikiwa.

Ukikubaliana na mabadiliko, unapona kwenye mabadiliko hayo, hutakuwa kiongozi, lakini pia mabadiliko hayatakupoteza.

Ukiyapinga mabadiliko, mabadiliko yanakuua, yanakupoteza kabisa.

Hivyo mabadiliko yoyote unayoyapinga au kuyakataa kwenye maisha yako, yanakuua, yanakupoteza kabisa.

Popote ulipo, kuwa chanzo cha mabadiliko na mara zote utakuwa mbele na kufanikiwa. Lakini unapochelewa na ukakuta mabadiliko yameshatokea tayari, kubaliana nayo haraka ili usipotezwe.

Uwe na juma bora sana linalokuja, lipangilie vyema na chukua hatua kuwa bora zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Rafiki, kama ungependa kujifunza zaidi kupitia mafunzo ninayotoa, karibu ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Hii ni blog maalumu inayoenda na kundi maalumu la wasap ambapo kila siku unajifunza na kuhamasika, kila wiki kuna madarasa ya mafanikio na kila mwaka kuna semina tatu nzuri sana kwa mafanikio yako.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa wasap kwenda namba 0717396253 au fungua hapa;  www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji